Wednesday, February 27, 2008

WAHUSIKA WIZI WA BOT

WAZUIWA KUSAFIRI NJE


BAADHI WABANWA, WAANZA KUREJESHA FEDHA

SERIKALI, imezuia hati za kusafiria (pasipoti) za baadhi ya vinara wa ufisadi wa zaidi ya bilioni 133/- kutoka akaunti ya madeni ya nje ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefahamika.

Vyanzo vya ndani kutoka serikalini vimeeleza kwamba nyaraka hizo za kusafiria za wakurugenzi na baadhi ya wanahisa wa kampuni 22 ambazo zililipwa mabilioni ya shilingi kwa njia za kifisadi na BoT zimechukuliwa na mamlaka husika kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusiana na kashfa hiyo.

Mbali ya kuwanyang’anya pasipoti, vinara kadhaa wa wizi huo wamezuiwa kabisa kusafiri nje ya nchi hata kwa njia zisizo rasmi, kwani inahofiwa kwamba baadhi wanaweza kufanya hila na kutoroka.

Kwa niaba ya uchunguzi uliofanywa wakurugenzi kadhaa wa kampuni hizo wamelazimika kusaini mkataba wa makubaliano na serikali, unaowabana kisheria kurejesha fedha zote walizolipwa kifisadi na benki hiyo katika kipindi maalum

Chanzo cha ndani kimetanabahisha kwamba baadhi ya watuhumiwa hao wamesharejesha mabilioni ya shilingi serikalini ambayo yaliibwa kutoka katika chumbo hicho kikuu cha fedha.

“Mpaka sasa, mabilioni kadhaa ya shilingi yamesharejeshwa serikalini kutoka kwa wahusika waliojichotea kupitia akaunti ya madeni ya nje ya Benki Kuu (EPA)”, kilisema chanzo hicho.

Baadhi ya wanahisa na wakurugenzi wa kampuni ambazo zilinufaika na fedha hizo kutoka BoT ni pamoja na mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu zaidi kama Jeetu Patel, ambaye ni mmiliki wa kampuni tisa kati ya 22 ambazo zimetajwa kwenye kashfa hiyo kubwa

Kampuni zinazomilikiwa na Jeetu Patel Navycut Tobacco (T) Limited, Ndovu Soaps Limited, Bina Resorts Limited, Bencon International limited, Maltan Mining company limited, Bora Hotels & Apartments Limited, Venus Hotels Limited BV & Associates company limited

Watu wawili ambao sio maarufu sana, John Kyomuhendo na Francis William, wametajwa kwamba ndio wanahisa wa kampuni tata ya Kagoda Agriculture Limited, ambayo ililipwa kitita cha dola za Marekani milioni 30.8 (takriban 40/-) kutoka kwenye akaunti ya EPA

Vyanzo vinasema wapelelezi wa serikali tayari wameshawabaini wahusika halisi wa malipo yaliyofanywa kwa kampuni ya Kagoda, ambapo mmojawapo ni mfanyabisahara marufu lakini akiwa anajihusisha kwa siri katika biashara haramu.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti dada la THISDAY umegundua kwamba Kyomuhendo na William walikuwa ni chambo tu waliotumiwa na wafanyabiashara hao maarufu ili kuficha uwepo wao. Wakili mashuhuri jijini Dar es Salaam, Beredy Sospeter Maregesi, amedajwa katika kampuni mbili ambazo zimetajwa katika kashfa ya BoT Maregesi Law Chambers na G&T International Limited.

Mfanyabiashara mmoja maarufu wa Dar es Salaam, Johnson Mutachukurwa Lukaza, ambaye anamiliki kampuni ya ujenzi wa majumba na biashara nyinginezo, ametajwa kama ndiye mwanahisa mkuu wa kampuni ya KERNEL Limited, kampuni nyingine ambayo imetajwa kwenye orodha ya kashfa hiyo. Ndugu wa Johnson, Mwesugwa Rutakyamilwa Lukaza, pia ametajwa kwenye nyaraka za kampuni hiyo kama mwanahisa.

Mtu mwingine anayetajwa kwenye kashfa hiyo ya BoT ni Elisifa Ngowi ambaye anaelezwa kwamba ni Ofisa Usalama wa Taifa Mwandamizi jina la Ngowi limo kwenye rekodi za kampuni mbili zilizojinufaisha na fedha za EPA- Clayton Marketing Limited.

Wanahisa wa Excellent services Ltd, ambayo ilisajiliwa mwaka 1992, ni Ngowi, Emily Samanya, Peter Sabas, Lecis Msiko na Massimo Feneli.

Charies Isaack Kissa anatajwa kwamba ni mmiliki wa kampuni ya Kiloloma and Brothers Limited, wakati ambapo kampuni nyingine iliyonufaika na fesha hizo ni Money Planners & Consultants Limited, ambayo inawataja Paul Tobias Nyingo na Fundi Hayesh Kitunga kama ndio wamiliki wake.

Pia katika orodha hiyo ya ufisadi ya EPA kuna kampuni nyingine mbili Njake Enterprises Limited (iliyosajiliwa mwaka 1984) na Njake Hotels and Tours Limited (iliyosajiliwa mwaka 2003). Wamiliki wa Njake Enterprises Ltd walioorodheshwa ni Japhet Laiyandimilema, Anna Japhet Leman na Laiyandumi Njake Lema wa mkoani Kilimanjaro.

Kwa upande mwingine Japhet Laiyandumi Lea, Anna Japhet Lema, Abel Japhet Lema, Derick Japhet Lema na Bernard Japhet Lema wametajwa kwamba ndio wamiliki wa Njake Hotels and Tours Ltd ya Arusha.

Kampuni nyingine inayotajwa kwenye EPA ni Changanyikeni Residential Complex Limited ya Dar es Salaam ambayo wamiliki wake ni Jose van Der Merwe (yawezekana ni raia wa Afrika Kusini), Samson Mapunda na Charles Mabina.

Mibale Farm pia ilinufaika na fedha hizo ambapo inatajwa kwamba Kizza selemani na Farijala Hussein ndio wamiliki wake.

Rais Jakaya Kikwet mwezi uliopita aliagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnston Mwanyika, kuongoza timu ya kuchunguza wahusika wote katika kashfa hiyo ya EPA.

Rais pia alimteua Mkuu wa jeshi la Polisi, Saidi Mwema, na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Dk. Edward Hoseah kushirikana na Mwanasheria Mkuu kuchunguza ufisadi huo na kukamilisha kazi kwa miezi sita. Mamlaka zinazohusika zinasema kwamba kurejeshwa kwa fesha ya BoT zilizoibwa ndiyo kipaumbele cha kwamba katika kuchunguzi huo, huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa kufikishwa kortini kwa wahusika wenigne muhimu baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo.

Mahali alipo kwa sasa gavana wa zamani wa BoT, Dk. Daudi Ballali, ambaye alifukuzwa kazi kutokana na kashfa hiyo kufichuliwa na kampuni moja ya ukaguzi wa hesabu, bado kuna utata. Tayari Marekani imemnyang’anya viza yake ya kibalozi.

KUTOKA GAZETI LA KULIKONI, 26/2/2008)

No comments: