Wednesday, February 27, 2008


Lowassa Usijifananishe na

Mzee Mwinyi- Kiula..




Waziri wa zamani wa ujenzi wa serikali ya awamu ya pili ya muungano wa Tanzania,Mh Nalaila Kiula pichani,akizungumza na waandishi wa habari leo ukumbi wa idara ya habari Maelezo jijini Dar es Salaam kuhusiana na ripoti ya tume ya Mwakyembe iliyokua inachunguza mkataba wa Richmond, akizungumza leo Mh Nalaila Kiula,ambaye aliwahi kushtakiwa kwa tuhuma za ufisadi wa kuingizia hasara serikali ya Sh3.2 bilioni katika ujenzi wa barabara. Mh Kiula alishitakiwa kwa tuhuma za rushwa za ujenzi wa barabara za New Bagamoyo/ Chanika/Mbagala, na kudaiwa kuingiza serikali hasara ya Sh 3.2 bilioni, lakini alishinda kesi. Mh Kiula, alisema Lowassa hawezi kujifafanisha na mzee Mwinyi kwani mazingira ya tuhuma zao ni tofauti.

Akizungumza kwa msisitizo,alifafanua kwamba Mwinyi alijiuzulu kwa tuhuma wakati akiwa amekaa ofisini Dar es Salaam huku tukio likitokea Shinyanga, lakini Lowassa alikuwa akishiriki mchakato wa Richmond katika hatua mbalimbali.

"Kujiuzulu kwa Mwinyi hakuwezi kufafanishwa na Lowassa, Mzee Mwinyi alikuwa ofisini Dar es Salaam tukio limetokea Shinyanga, lakini Lowassa alikuwa akishiriki kila hatua za mkataba wa Richomnd, " alisisitiza.

Kiula aliipongeza Kamati ya Bunge na Bunge lenyewe kwa kazi nzuri waliyofanya na kutaka Watanzania wote, kuungana kupambana na ufisadi.

Waziri huyo wa zamani, alihoji uhalali na msimamo wa Jaji Joseph Warioba kumtetea Lowassa, kwamba hakupewa nafasi ya kusikilizwa na kumtaka aache kuzungumza vitu huku akisahau rekodi yake.

Kiula alifafanua kwamba, haielewi mantiki ya Jaji Warioba kusema Lowassa alinyimwa haki ya kusikilizwa wakati hata yeye (Warioba) alishindwa kumtendea haki (Kiula) katika Ripoti yake Kuhusu Mianya ya Rushwa ya mwaka 1996, ambayo ilisababisha kufunguliwa kesi ya rushwa ya Sh3.2 bilioni dhidi ya Kiula bila ya (yeye Kiula) kupewa haki ya kusikilizwa.

Alisema Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Edward Hosea na wasaidizi wake, wanapaswa kung'oka kwani wanamuweka Rais Jakaya Kikwete pabaya.

"Hivi ukimkuta baba yako kakaa vibaya, utamuangalia, utamwambia au utakimbia usiendelee kumwona, sasa Rais Kikwete kakaa vibaya, Hosea na wenzake wanazidi kumwangalia badala ya kuondoka," alisisitiza Kiula.

Aliongeza kwamba, Hosea amepoteza sifa za kuwa mkuu wa Takukuru na kuongeza kwamba taasisi hiyo inahitaji mtu ambaye si wa kujipendekeza na mwenye msimamo na kusisitiza:, "Hosea anapaswa kwenda na maji".

Alisema maadili ya uongozi katika nchi yameporomoka na kuhoji uhalali wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa kufanya biashara Ikulu huku akikopa dola 500,000 kutoka NBC LTD bila dhamana, lakini yeye (Kiula) alishatakiwa kwa mkopo wa Sh12milioni tena wenye dhamana kwa madai ya kuibia nchi.

Huku Kiula akieleza hilo, Baraza la Vijana ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limemuonya Lowassa kutoendelea kujifananisha na Mwinyi kwani kufanya hivyo ni kumchafua Rais huyo mstaafu.

"Lowassa akumbuke kuwa Mwinyi hakujiuzulu kwa tuhuma za ufisadi au matumizi mabaya ya madaraka aliyofanya yeye katika nafasi yake bali watumishi katika eneo lingine kabisa ingawa walikuwa chini yake, Mwnyi hakujiuzulu kwa shinikizo kama Lowassa," ilisema taarifa ya Baraza hilo.Habari hii Ramadhan Semtawa na Festo Polea.

No comments: