Saturday, February 23, 2008

Wanaharakati

waitetea

Jambo Forums





na George Maziku


WANAHARAKATI wa haki za binadamu nchini, wamesema kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata vijana wanaoendesha mtandao wa Jambo Forums kinakiuka katiba ya nchi na misingi ya haki za binadamu.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen Kijo Bisimba, alisema katiba ya nchi inatoa hakikisho la kila mtu kuwa na uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, na uhuru wa kupokea habari.

“Nimesoma habari za kukamatwa kwa vijana wa Jambo Forums katika magazeti, lakini kituo chetu hakioni kosa lolote la jinai walilotenda kama polisi wanavyodai.

“Kitendo cha kuwakamata ni kuingilia uhuru wao wa kujieleza na uhuru wa habari bila sababu za msingi, kinyume cha katiba ya nchi na haki za binadamu,” alisema Bisimba.

Alisema kuwa kituo chake kinaiona hatua hiyo ya polisi kuwa jaribio la kuwatisha na kuwashona midomo Watanzania ili waogope kuhoji mambo mbalimbali yanayohusu nchi yao, kisiasa, kiuchumi na kijamii.

“Mtandao wa Jambo Forums umesaidia Watanzania wengi sana kujua mambo mengi kuhusu nchi yao. Hata kashfa za Richmond na BoT kwa mara ya kwanza zilichapishwa kwenye mtandao huu,” alisema mtendaji huyo wa LHRC.

Alisema kituo chake kinalifuatilia kwa karibu tukio hilo, na kwamba kipo tayari kutoa msaada wa kisheria kwa wahusika ili kuhakikisha haki inatendeka.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa chama cha Wanahabari wa Haki za Binadamu nchini (Journalists for Human Rights-JournoRights), Christopher Kidanka, alilaani kitendo cha polisi kuwakamata wanahabari wa Jambo Forums na kukielezea kuwa ukandamizaji wa uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza.

“Tunalaani kukamatwa na kuzuiliwa kwa saa 14 kinyume cha sheria, kwa wanamtandao wa Jambo Forums na tunatoa wito wa kufutwa mara moja mashitaka dhidi yao,” alisema Kidanka katika taarifa yake ya ukurasa mmoja kwa vyombo vya habari.

Kidanka alisema kuwa kitendo hicho cha polisi kinathibitisha kuwa, watawala wamejiandaa kuuminya kwa haraka uhuru wa kujieleza unaoanza kuchanua miongoni mwa Watanzania.

Alisema kuwa mtandao wa Jambo Forums umekuwa mstari wa mbele kutangaza maoni ya watu na kufichua uozo unaoikabili nchi, hivyo kuwakamata wanamtandao hao kwa tuhuma za uchochezi, ni kuifutilia mbali heshima ya Tanzania kama nchi ya kidemokrasia.

Jumatano wiki hii, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema alizungumza na wanahabari, ambapo pamoja na mambo mengine, aliwapa taarifa kuwa jeshi lake lilikuwa limewakamata na kuwazuia wanamtandao wa Jambo Forums kwa tuhuma za kutenda uhalifu kwa kutumia mtandao wao huo.

Hata hivyo, si Kamanda Mwema mwenyewe wala taarifa yake kwa vyombo vya habari, aliyefafanua uhalifu uliotendwa na vijana hao, zaidi ya kauli za jumla kuwa wanatangaza taarifa za kihalifu.

Wakati huo huo, habari zilizotufikia zinasema kuwa Jeshi la Polisi nchini limewaachia kwa dhamana wanamtandao wa Jambo Forums na watu wengine tisa waliokuwa wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za ugaidi.

No comments: