Saturday, February 23, 2008

Rostam afichua

siri kubwa


Baada ya kutajwa kumiliki kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, Mbunge wa jimbo la Igunga, Rostam Aziz hatimaye amefichua siri nzito kuhusu sakata hilo....


Mbunge huyo alifichua siri hiyo alipozungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu akiwa jimboni mwake mwanzoni mwa wiki hii.

Rostam alisema kuna mambo mengi ndani ya sakata hilo ambayo yatajulikana muda mfupi ujao, hivyo aliwataka Watanzania kutulia na kusubiri muda muafaka.

“Wananchi watulie kwani ukweli wa mambo utajulikana siku chache zijazo,” alisema Rostam bila kusema utajulikana kutoka kwa nani, au mamlaka ipi.

Alisema ni vigumu kupata ukweli wa mambo katika hali ya kunyoosheana vidole na kuomba subira ichukue nafasi ili maslahi ya taifa yaweze kulindwa.

Aidha, Rostam aliwashukuru wananchi wanaolitazama sakata la Richmond kwa upana na kuwataka wanaohukumu bila ushahidi wa kina wasifanye hivyo.

Rostam, alitajwa kuhusika katika sakata hilo, hasa baada ya kubainika kuna uhusiano kati ya Kampuni ya Dowans (inayoendesha shughuli za Richmond kwa sasa) na ile ya Caspian anayoimiliki.

Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa inachunguza kashfa hiyo, ilibaini Kampuni ya Dowans na ile ya Caspian zinatumia anuani zinazofanana, ikiwa pia baadhi ya wafanyakazi wa Caspian kufanya kazi Dowans, hivyo kutia shaka uhusiano wa aina hiyo.

Mbali na kuonekana ana mkono wake katika Dowans, Rostam alitajwa kuiunganisha Richmond na asasi moja ya mambo ya uhusiano ili iweze kuisafisha kampuni hiyo mbele ya jamii.

Kampuni hiyo ya mambo ya uhusiano inamilikiwa na Salva Rweyemamu, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ambaye pia alikiri kukutana na Rostam, pamoja na Dk. Gideon Shoo. Salva kwa sasa amejiondoa katika kampuni hiyo.

Hata hivyo, vyanzo vyetu vya habari vya kuaminika vinasema kuwa Rostam na wenzake waliotajwa kuhusika na ufisadi huo, walitumiwa na baadhi ya vigogo wengine wa serikali katika kunusuru mambo yaliyokuwa yameharibika.

“Awali ulikuwa ni mpango wa kundi la vigogo kutengeza pesa kupitia Richmond, mambo yalipoharibika, ikabidi ianze kutafutwa nusura ya haraka.

“Watu kadhaa wakatumiwa ili kuweka mambo sawa,” kilisema chanzo chetu bila kutaja majina ya waliotumiwa kama ni Rostam au wale mawaziri waliojiuzulu.



No comments: