Tuesday, March 04, 2008


Hamisi: Natamani

kwenda shule, uwezo sina



"Natamani sana kusoma lakini kutokana na uwezo wa familia yangu naona suala la kwenda shule litakuwa ndoto.Wakati mwingine najisikia vibaya kuona wengine wanakwenda shule, roho inaumia sana!"

"Nahisi kwamba matatizo niliyonayo hayataisha mpaka kufa kwangu ikiwa sitapata nafasi ya kwenda shule. Naomba Mungu anisaidie, ili siku moja niwe katika kundi la watu waliokwenda shule. Kwa sasa najua kusoma kidogo, bibi yangu ananifundisha ninapokuwa nyumbani,".

Hivyo ndivyo anavyoeleza mtoto Hamisi Bakari (11) anayeishi katika mazingira magumu kwenye kitongoji cha Kigamboni, Dar es Salaam baada ya kukimbia nyumbani kwa wazazi wake Tanga.

Hamisi anasema amekuwa akitegemea msaada wa fedha kutoka kwa watu anaowaomba barabarani, ili aweze kupata chakula cha mchana anapokuwa maeneo ya Posta Mpya katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Yapo mambo mengi yalimfanya Hamis akimbie nyumbani kwa wazazi wake na kuja Dar es Salaam, ambako alifikia Kigamboni kwa bibi yake ambaye ni mzee na hana uwezo wa kumsaidia katika mahitaji muhimu yakiwemo ya kupata elimu.

"Maisha yangu yamekuwa ya kubahatisha baada ya kukimbia mateso nyumbani kwa wazazi wangu," anasema Hamisi

"Nilikuwa napigwa hata kama sina kosa, nikaamua nitoroke na kuja Dar es Salaam kwa bibi kwakuwa nilihisi wazazi wangu hawapendi kuona nikiishi kwa fufaha," anasema na kuongeza kuwa hiyo ndiyo sababu leo hii amekuwa omba omba.

Anasema japo hafurahishwi na hali hiyo ya kuishi maisha magumu ya kuomba watu fedha kwaajili ya kununulia chakula, lakini hafikirii kurudi Tanga kwa wazazi wake mpaka mambo yake yatakaponyooka.

"Kwa sasa naomba watu wanisaidie nipate elimu ili niwe na masiha mazuri baadae. Natamani kuwa dereva lakini ndoto hiyo haitatimia bila elimu," anasema mtoto huyo na kusisitiza kuwa hataki kuwaona wazazi wake hadi pale atakapokuwa na kazi nzuri.

Mtoto huyo anasema matatizo mengine anayokutana nayo katika maisha yake ya kila siku mbali ya kukosa elimu, ni kuwa na maisha ya wasi wasi kutokana na baadhi ya vitendo anavyofanyiwa na wahuni wa mitaani.

Anasema siku nyingine ananyang'anywa fedha na wahuni wakati ambao muda wa kuomba unakuwa umekwisha na hivyo analazimika kurudi nyumbani bila kitu mfukoni.

"Wahuni wamekuwa wakitumia udogo wangu kunionea kwani wakati mwingine wananipora fedha na kunitishia kuwa nikisema kwa watu watanipiga, kwa bahati mbaya sina la kufanya na wala pa kusemea," anasema Hamisi

Anasema kukimbizana na mgambo wa Jiji la Dar es Salaam kwake ni tukio la kawaida kwakuwa mara kwa mara yeye pamoja na watoto wenzake wamekuwa wakifukuzwa eneo hilo la Posta Mpya.

Hata hivyo Hamis anasema ni vigumu kuondoka eneo hilo ingawa wanafukuzwa kwakuwa maisha yake yanategemea zaidi kuomba watu, na hasa wanaopita eneo hilo.

Hamis anasema akiona mgambo hao wamekaa katika eneo hilo, anaondoka kwa muda na kuvizia na punde wakiondoka naye anarudi kuendelea kuomba.

Anasema muda mzuri wa kupata fedha ni mchana, "mchana mambo yananyooka ndio muda mzuri, ni wakati wa chakula hivyo nikisema njaa inauma, watu wananionea huruma," anasema Hamisi.

Mtoto huyo anasema siku mambo yanapokuwa mazuri anapata hadi sh.4,000 lakini mara nyingi amekuwa akipata fedha isiyozidi 2,500 kwa siku.

Anasema mbali ya kutumia fedha hiyo wakati wa mchana anapokuwa mitaani, lakini pia ndiyo inayosubiriwa na bibi yake nyumbani.

"Bibi hana kazi, hivyo nikiomba fedha tunaitumia pamoja nyumbani. Sifurahi kuomba lakini jinsi mazingira yalivyo nalazimika kufanya hivyo. Wazazi wapo lakini hawana msaada kwangu," anasisitiza Hamis.

Alipoulizwa kama anapata msaada wowote kutoka Serikalini anasema kuwa hajawahi kumuona kiongozi wa aina yeyote akienda kuzungumza naye au anayetafuta sababu ya yeye kuwepo mtaani.

Hata hivyo anasema kama atapata bahati ya kukutana na Rais Jakaya kikwete, ombi lake kubwa litakuona msaada wa kupatiwa elimu.

"Siku nikipata nafasi ya kuonana na Rais Kikwete, nitamwomba anipeleke shule, nahisi nikikiwa na elimu yangu, mambo yatakuwa mazuri na nitaweza kumsaidia bibi. Pia nitamsimulia jinsi watoto tunaoishi maisha ya kuomba tunavyoteseka sana," anasema.

Alipoulizwa kama anakumbuka siku au tarehe aliyofika Dar es Salaam akitokea Tanga, anasema hana kumbukumbu kwani muda mrefu umepita lakini anakumbuka basi alilopanda.

"Nilipotoroka sikumuaga baba wala mama, niliwatoroka kwa sababu nilikuwa napakumbuka kwa bibi. Nilipanda basi na kuingia usiku. Nililala kituo cha mabasi Ubungo na siku iliyofuata nilikwenda Kigamboni kumtafuta bibi," anasema.

Kuhusu muda anaondoka eneo la Posta Mpya kurudi kigamboni anasema hana muda maalumu na kuongeza kwamba inategemea siku hiyo amepata fedha kwa kiasi gani.

No comments: