Tuesday, March 04, 2008

Richard Bukos na Issa Mnally


Stadi wa Muziki wa Taarab nchini, Mzee Yusuf na dada yake, Hadija, usiku wa Ijumaa iliyopita Februari 29, 2008 waliwaacha watu midomo wazi, baada ya kulishana keki kwa midomo, hivyo kutoa taswira ya kupeana denda ‘laivu’. Mzee na Hadija ambao nyota zao kimuziki zinang’ara kwa sasa kupitia Kundi la Jahazi Modern Taarab, walifanya kituko hicho ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam, wakati wa sherehe ya kutimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa kikundi hicho...


Wakati wakifanya kioja hicho, wasanii hao ambao ni ndugu wa damu kwa baba na mama, walishuhudiwa na mzazi wao wa kike, Mwanajuma Mzee huku maelfu ya mashabiki wa muziki wao, wakiwa wamefurika ukumbini humo.

Ijumaa Wikienda ambalo lilikuwa kamili ukumbini humo, awali lilishuhudia onesho hilo likianza kwa shoo ya utangulizi, iliyoporomoshwa kutoka kwa wakongwe wa Taarab kutoka Kundi la JKT, Patricia Hillary na Bi. Shakira Said.

Milango ya saa tano usiku, Mzee Yusuf ambaye ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa Jahazi, aliwasili Diamond Jubilee akiwa kwenye gari ya kifahari, aina ya Lincoln Limousine na kupokewa kwa hoi hoi na mashabiki.

Baada ya mkurugenzi huyo kuwasili, shoo hiyo ambayo mgeni wake rasmi, alikuwa ni Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azan, ilikolea zaidi hasa lilipofikia zoezi la kulishana keki ambalo liliongozwa na Mzee.

Katika zoezi hilo, Azan ndiye aliyekuwa wa kwanza kulishwa keki na Mzee, kabla ya mbunge huyo kupokea na kumlisha mwanamuziki huyo galacha.

Baadaye, Mzee alimlisha Mwanajuma, Hadija, bibi yake ambaye ni mkongwe wa Taarab nchini, Fatma Baraka ‘Bi. Kidude’, pamoja na wake zake wawili, Leila Rashid na Chiku Hamis.

Aidha, baada ya Mzee kumaliza, Hadija naye alikata kipande cha keki hiyo iliyokuwa na umbo la jahazi, kisha kukiweka mdomoni mwake kabla ya kumfuata Mzee na kumlisha, kitendo ambacho kilishangiliwa na watu wengi.

Hata hivyo, pamoja na sehemu ya watu kuonekana kushangilia tukio hilo, kundi kubwa lilishangazwa na kuchukizwa kutokana na kile walichokisema kuwa kitendo cha Mzee na Hadija kulishana keki hakishabihiani na maadili yetu Watanzania.

Mmoja kati ya waliokemea ni Jasmin Hamdun (36) wa Magomeni Mapipa, Dar es Salaam ambaye alisema kuwa Mzee na Hadija wanapotea.

“Astaghafirullah, yaani Mzee Yusuf na Hadija wanafikia kufanya uchafuu hadharani kweli, basi hawa vijana wamepotea,” alisema Jasmin huku akiwa ametoa macho kwa mshangao.

Mwingine aliyelaani ni Shaibu Shemazi wa Ilala Boma, jijini ambaye alisema, kitendo cha Mzee kukubali kulishwa keki kwa mdomo na Hadija hakina picha nzuri, pia kinaweza kuzua hali ya wivu kwa wake zake.

Alisema: “Wake zake amewalisha kwa uma, halafu anakubali kulishana kwa mdomo na dada yake, unajua hiyo inaweza kuwafanya wale wanawake wajihisi unyonge kwa kuona amewashusha thamani mbele ya dada yake.

Akiongea na mwandishi wetu juzi (Jumamosi), Mzee alisema kuwa Hadija alimlisha keki kwa mdomo ili kumshangaza (surprise).

“Ni hali ya kawaida, kwa sababu yule mimi dada yangu toka nitoke, na kuhusu kwanini nisiwalishe keki wake zangu kwa mdomo, badala yake iwe ni kwa Hadija hiyo ni hiyari ya mtu,” alisema Mzee.

Mbali na tukio hilo, shoo hiyo ya Birthday ya Jahazi ilifana kwa burudani ya kukata na shoka kutoka wanamuziki ambao walionesha uwezo wao wa kukonga nyoyo za mashabiki, pia iliweka rekodi kwa kuhudhuriwa na umati mkubwa watu.


No comments: