MZIGO mzito wa kimaamuzi unaonekana dhahiri kumlemea Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ambaye amelazimika kuviongoza vikao viwili vizito vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, vinavyofanyika Butiama bila ya kuwapo kwa nguzo zake kuu kisiasa.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumapili unaonyesha kwamba, kukosekana kwa wajumbe kadhaa muhimu wa kudumu wa vikao vya CC na NEC ya CCM, kunaweza kwa kiwango kikubwa kutia doa kama si kuathiri baadhi ya maamuzi mazito ambayo yamekuwa yakitarajiwa kufikiwa.
Miongoni mwa watu hao muhimu ambao kukosekana kwao kumeshaanza kuibua hali ya wasiwasi na kuonekana kupwaya kwa uzito wa vikao hivyo vya Butiama vinavyofanyika kwa mara ya kwanza eneo alikozaliwa na kuzikwa, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ni marais na wenyeviti wastaafu wawili wa chama hicho, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Wadadisi wa mambo kadhaa wa ndani ya chama hicho waliozungumza na Tanzania Daima kutoka Butiama, wanakielezea kitendo cha kukosekana kwa Mkapa na Mwinyi kuwa jambo ambalo litasababisha kulemewa kwa Kikwete na pengine kukosekana kwa nguvu ya kufikiwa kwa maamuzi mazito yanayogusa mustakabali wa wakati huu wa chama hicho.
Aidha, wakati kukosekana kwa viongozi hao wawili ambao ni wajumbe wa maisha wa CC na NEC ya chama hicho kunachagizwa na kupewa uzito mkubwa, na kutokuwapo kwa Rais mstaafu wa Zanzibar, ‘Komandoo’ Dk. Salmin Amour Juma.
Kama hiyo haitoshi, vikao hivyo vinafanyika Butiama wakati pia akikosekana mwanadiplomasia adhimu nchini, Dk. Salim Ahmed Salim, ambaye naye ni mjumbe wa CC na NEC kwa pendekezo la Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho.
Mbali ya Dk. Salmin, kikao cha NEC kilichoanza jana jioni majira ya saa 11 kutokana na kuchelewa kwa kikao cha CC, pia kinafanyika pasipo kuwapo kwa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Kutokuwapo kwa Dk. Salmin na Dk. Salim katika vikao hivyo viwili, kunalifanya suala la kupatikana kwa ufumbuzi wa kudumu kuhusu hali ya kisiasa ya Zanzibar, na hususan kufikiwa kwa muafaka wa kisiasa visiwani humo kati ya vyama vya CCM na CUF kuwa ni wenye mashaka makubwa.
Baadhi ya wajumbe wa NEC waliozungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa majina yao magazetini, wanakielezea kitendo cha kukosekana kwa viongozi hao wawili wanaotoka Zanzibar kuwa jambo ambalo linaweza kuyafanya maamuzi kuhusu muafaka kuwa magumu.
Jambo gumu kwa chama hicho na hususan kwa Rais Kikwete kuhusu kukosekana kwa viongozi hao wa juu muhimu wanne, ni wasiwasi ambao umeshaanza kuzingira vikao hivyo, unaoonyesha kwamba huenda wazee hao wamekosekana si kwa sababu ya kuwa safari kama inavyodaiwa na uongozi wa juu wa CCM, bali kutoridhishwa kwao na mwenendo wa mambo serikalini na ndani ya chama.
Wana CCM waliozungumza na Tanzania Daima kuhusu hili, wanaielezea hatua ya watu hao kukosekana kuwa ni dalili ya mwanzo ya CCM ya Kikwete kuanza kukosa ushawishi ndani ya mioyo ya viongozi wakuu wastaafu, ambao sasa wanakiona chama kikipoteza misingi yake ya kihistoria ya kushika hatamu.
“Kumekuwa na wasiwasi kwamba, Kikwete amekuwa akifikia maamuzi mazito pasipo kwanza kukitaarifu chama na badala yake amekuwa akifanya hivyo kwa kutumia Bunge na ushauri wa kundi dogo la watu. Hali hii inaonekana kutowafurahisha wazee,” alisema mfuatiliaji mmoja wa karibu wa siasa za ndani ya CCM.
Lakini pengine pigo kubwa kwa Rais Kikwete lilizidi kuonekana dhahiri jana baada ya Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Mzanzibari, kulazimika kuondoka katika vikao hivyo kutokana na kufariki dunia kwa mama yake mzazi.
Kuondoka kwa Dk. Shein, kiongozi wa pili kwa mamlaka katika serikali na mtu aliyetokea kuwa mshauri wa karibu kikatiba na kikazi wa Rais Kikwete, kunayafanya maamuzi kuhusu siasa za Zanzibar kuzidi kuwa magumu.
Kutokana na hali hiyo basi, Rais Kikwete atalazimika kutumia ushauri wa Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wake, Amani Abeid Karume, Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi mstaafu Gharib Bilal na Wazanzibari wengine wasio na ushawishi mkubwa katika kueleza kwa kina athari za kisiasa, kijamii na kiuchumi za kuhitimishwa kwa muafaka ambao unatarajia kutoa baraka za kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa visiwani.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba, watu hao muhimu, Mwinyi, Mkapa, Dk. Salmin, Dk. Salim na Dk. Shein wanakosekana katika vikao wakati moja ya ajenda inayosubiriwa kwa hamu na Wazanzibari ni hiyo ya kufikiwa kwa suluhu ya kudumu ya kisiasa huko visiwani.
Mbali ya hilo la mwafaka, kukosekana kwa Mkapa kwa mfano kunaufanya mjadala kuhusu masuala kama lile la Kashfa ya EPA na mengine yanayomgusa yeye binafsi kushindwa kujadiliwa kwa kina.
Hali hiyo inakuja baada ya watu kuwa na imani kwamba, vikao hivyo vya Butiama vinavyofanyika hatua chache kutoka alipozikwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, vilikuwa vikitarajia kupata majibu ambayo yangekisadia chama hicho kupata majibu kamili kuhusu nini kilitokea katika EPA zama za Mkapa akiwa Rais na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.
Kama ilivyo kwa Mkapa, kukosekana kwa Mwinyi, kiongozi ambaye kimsingi ndiye anayeweza kubeba mzigo wa kuwa mrithi wa kiuongozi wa taifa baada ya kuondoka kwa Mwalimu Nyerere, kunaufanya mjadala wa masuala kama lile la Richmond lililosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri kupwaya na kukosa mashiko.
Wafuatiliaji wa mambo wanakuona kukosekana kwa Mwinyi kuwa ni pengo ambalo litamwia vigumu Kikwete kuliziba wakati huu chama hicho kikiwa katika mazingira magumu kuvunja kuimarika na kuibuka kwa makundi mengi zaidi ndani ya chama hicho, yaliyoibuka baada ya masuala ya EPA na Richmond kuibuka.
“Kwa namna yoyote ile sisi kama chama tulihitaji sana hekima za wazee wetu kama Mwinyi na Mkapa katika kuhitimisha haya masuala ya EPA na Richmond, ambayo hayajapata kujadiliwa kwa kina,” alisema mwana CCM mmoja aliyezungumza na Tanzania Daima Jumapili jana.
Baadhi ya minong’ono inayosikika kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo inaeleza kwamba, Mkapa hakuhudhuria vikao hivyo kwa sababu ya kuchukizwa kwake na hatua ya kuhusishwa moja kwa moja na ukiukaji wa maadili wakati akiwa madarakani.
Inaelezwa kuwa, ingawa Mkapa alimuunga mkono Kikwete katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, kutajwa kwa jina lake sana katika masuala mbalimbali, ni jambo analoliona likiwa na baraka kamili za viongozi wa juu serikalini wenye malengo yao binafsi.
Baadhi ya wadadisi wanahofu kwamba, upo uwezekano mkubwa kuwa baadhi ya viongozi wakuu wastaafu wameanza kuiona serikali ya sasa kuwa iliyopoteza uwezo na umadhubuti wa kuhimili mikiki mikiki na hivyo wakaamua kukaa kando.Kutoka Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment