*Ukosefu wa vifaa ni tatizo sugu
*JK atuma salamu za rambirambi
Na Said Njuki, Mererani
*JK atuma salamu za rambirambi
Na Said Njuki, Mererani
KAZI ya uopoaji maiti ndani ya migodi ya tanzanite, Mererani wilayani hapa, imezidi kuwa ngumu na hata kukwama kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuopolea zikiwamo pampu za kuvutia maji kutoka mashimoni.
Hali hiyo imetokana na kwamba takriban miili 67 bado imo ndani ya migodi hiyo, huku miili sita tu ndiyo ikiwa imeopolewa juzi asubuhi huku viongozi wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bw. Henry Shekifu, wakiunda kamati kadhaa.
Baadhi ya kamati hizo ni ya Operesheni Okoa itakayoongozwa na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Kamishna Venance Tossi, ya Maafa ambayo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Bw. Khalid Mandia na Katibu wake ni Ofisa Madini wa Kanda, Bw. John Nayopa.
Kamati nyingine ni ya wataalamu ambayo wengi wa wajumbe wake ni wachimbaji madini.
Lakini wakati kamati hizo zikiendelea kujipanga, baadhi ya wachimbaji walionesha wasiwasi wao juu ya uwezekano wa kuopoa miili hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, mchimnbaji Sokota Mbuya, alisema mbali na vifaa kupatikana, Serikali inatakiwa kutoa msaada moja kwa moja wa chakula na posho kwa wachimbaji wazoefu, kwani eneo hilo limekumbwa na baa la njaa na hivyo kuingia mgodini na njaa ni vigumu.
Alisema maiti hawawezi kuopolewa na wataalamu wa Jiolojia peke yao, kwani hata katika maafa ya mwaka 1998 wataalamu hao na vikosi vya majeshi, walisaidiwa kupanda juu baada ya kuingia na kushindwa kutoka.
Mama Stella Shayo, ambaye pia ni mchimbaji, aliwahoji kwa kejeli viongozi wa Serikali akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Bw. Philip Marmo; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Lawrence Masha na Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja, kwamba Serikali Kuu ilifuata nini pale badala ya kuendelea na vikao huku miili ikiendelea kubaki mashimoni.
Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Shekifu pamoja na kuwataka wachimbaji kushirikiana katika kadhia hiyo, pia alisimamisha kwa muda usiojulikana shughuli zote za uchimbaji katika migodi hiyo ya vitalu A, B, C na D.
Akizungumzia hatua hiyo, Mkaguzi Mkuu wa Madini nchini, Bw. Edwin Ngonyani, alisema Serikali hufanya kazi kwa mujibu wa sheria ya usalama migodini, inayoipa mamlaka ya kufunga migodi na moja ya sababu ni kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika shughuli hiyo.
Waziri Marmo kwa upande wake, alisema Serikali inafanya kazi na kamati mbalimbali za maafa za ngazi zote na atapokea mapendekezo ya kamati husika ili naye atoe mchango wake.
Lakini wakati yote hayo yakiendelea, tayari wataalamu kutoka mgodi wa dhahabu wa Barrick waliripotiwa kutua Mererani, ili kuongeza nguvu za uopoaji huku wajumbe wa moja ya kamati wakiwa migodini tangu asubuhi kutathmini ugumu wa kazi hiyo.
Kamati hiyo inaundwa na wachimbaji, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wana usalama, Polisi.
Jumla ya wachimbaji 166 ndio waliodaiwa kuingia katika migodi hiyo huku 93 wakitoka salama na 67 wakiaminika kuwa bado hawajaopolewa. Ajali hiyo ilitokea juzi kwa mashimo kujaa maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za pole Mkuu wa Mkoa na wananchi wa Mkoa wa Manyara, kutokana na maafa hayo.
Taarifa ya Ikulu kutoka Butiama, Musoma jana, ilisema Rais alipokea kwa masikitiko, huzuni na mshtuko mkubwa taarifa za janga hilo kubwa.
Alihuzunishwa kwa upotevu wa maisha ya watu ambao mpaka sasa imethibitika kuwa wamepoteza maisha.
Rais pia aliwaombea wachimbaji ambao taarifa zao hazijathibitika waweze kupatikana haraka wakiwa hai na salama na pia aliwaombea wote walioumia katika ajali hiyo wapone haraka.
Alitoa pole kwa familia ambazo zimeathirika na janga hilo na kuzihakikishia kuwa yuko pamoja nazo katika wakati huu wa majonzi na huzuni.
Kutoka Tanga Bakhya Said, anaripoti kuwa kivuko cha Mto Pangani, mv Pangani kilizama juzi saa moja asubuhi wakati kikipakia gari lililokuwa limebeba marobota ya mkonge yenye uzito wa tani nane na kusababisha mlango wa kivuko hicho kukatika.
Akizungumzia juzi mchana baada ya ajali hiyo katika eneo la tukio, katika gati la ng'ambo ya Bweni, Mkuu wa kivuko hicho, Bw. Marko Manyala, alidai kuwa chanzo cha ajali ni uchakavu wa milango ya kivuko hicho.
Bw. Manyala alisema katika ajali hiyo hakuna abiria wala mfanyakazi aliyepata madhara kwa kuwa kilizama katika gati kabla ya abiria kuingia.
"Tulianza kazi saa 12 asubuhi na tulivusha basi na abiria, lakini dereva wa gari lililobeba marobota aina ya Mitsubishi T 416 AMG lililokuwa na uzito wa tani nane kabla ya abiria kupanda, tulimruhusu aingize gari lake na baada ya kuingiza tairi za mbele alifunga breki ghafla na uzito wote ukawa nyuma ya mlango, ukakatika likabaki linaning’inia na sehemu kubwa ya kivuko ikawa imeshikilia majini," alisema Bw. Manyala.
Alisema maji yalivyozidi kujaa kivuko hicho kilizidi kufunikwa na maji lakini walivuta gari hilo ambalo nusu lilikuwa nchi kavu kwenye gati na nusu kwenye kivuko.
Wakati hali hiyo ikitokea Naibu Waziri wa tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bi Selina Komba alikuwa katika ziara ya siku tatu kutembelea miradi mbalimbali ya wananchi na kusikiliza maoni na kero zao na alipangiwa kuvuka ng’ambo ya pili ya Mto Pangani, ambako ndipo ilipo sehemu kubwa ya Wilaya.
Naibu waziri huyo alilazimika kuvuka kwa kutumia boti na pia alijionea hali halisi ya kivuko hicho na amekiri kuwa malalamiko ya wananchi na viongozi wa wilaya ya Pangani yana msingi sana.
Wakati haya yakitokea, msafara huo wa Naibu Waziri pia uliongozana na Mbunge wa Pangani, Bw. Rished Abdallah.
Jana mafundi wa kivuko hicho walikuwa wamefunga mapipa na kuweka pampu za kutolea maji, ili kukifanya kiweze kuelea ili waanze ukarabati wa bodi na mashine ambazo zimeingia maji ya chumvi.
No comments:
Post a Comment