
Kabila lisilobadilika
kiutamaduni tangu kale
Ikunda Erick
Daily News; Friday,March 14, 2008 @00:04
![]() |
| Wasichana wa kibarbaig wakiwa wamevalia mavazi yao ya ngozi |
Moja ya utamaduni wao ambao haubadiliki ni kuvaa mavazi yatokanayo na ngozi halisi za wanyama. Wanawake wao huvaa ngozi ya mbuzi au ng’ombe iliyokaushwa na kutengenezwa vizuri kwa kuchangangwa na urembo wa shanga.
Miguuni huvaa kandambili za kutengenezwa na magurudumu ya magari. Wanaume wa Kibarbaig kwa kawaida hutembea wameshika mkuki na huvaa mavazi ya ngozi. Tabia hiyo haitofautiani sana na ile ya kabila la Wamasai.
Kufanana kwa makabila hayo mawili, huweza kumfanya mtu kuhisi kuwa Wabarbaig na Wamasai ni kabila moja. Lakini kuna tofauti kubwa, hasa kwa mtindo wao wa utoboaji masikio na uvaaji, ambapo Wamasai mavazi yao ni lubega na shanga, ambapo nyingi ni za rangi nyekundu , wakati Wabarbaig wao huvaa ngozi iliyochanganywa na shanga zenye rangi ya chungwa na njano.
Kabila la Barbaig lina historia ndefu, ambapo hadi leo ni moja ya makabila machache yenye kufuata utamaduni wa kuwa na uongozi wa familia kwa ngazi za marika.
Rika linalolingana hukaa pamoja na kuwa na mambo au kazi zao, ambapo pia kwa upande wa mila na taratibu za ndoa, mwanamume anaweza kuwa na wake watatu, ambao hukaa pamoja na kushirikiana bila kugombana.
Utamaduni wao huo wa kutobadili mavazi yao, licha ya utandawazi na mabadiliko ya teknolojia, umefanya kabila hilo kuwa moja ya makabila machache nchini yanayodumisha utamaduni wao.
Wabarbaig wanaishi katika Ukanda wa Mlima Hanang, wenye kuvutia kwa mandhari yake na Ziwa Balangida, lenye maji baridi lililoko katika mharara wa Mulbadow, ambao hata ukame utatokea, chemchemi zitokazo mlimani husaidia kulisha mifugo yao na kujaza maji katika ziwa hilo, hivyo kuendeleza uzuri wa eneo la Wabarbaig.
Kwa kawaida Wabarbaig ni warefu kwa kimo na hugawana kazi kulingana na rika kama ilivyo kwa Wamasai, ambapo mgawanyo huo hujulikana kama (doshinga) ambapo utawala wake ni juu ya haki ya kumiliki vyanzo vya maji na malisho. Pia pamoja na kufanana kwa makabila hayo ya Wabarbaig na Wamasai, kabila hilo la Wabarbaig linajulikana kwa majina kadhaa.
Wamasai huwaita Wabarbaig kama Wambulu, yaani watu waliotoka Kusini mwa eneo la Wamasai. Upande mwingine wa jamii ya Wabarbaig ni Mang’ati, ambao ni watu kutoka upande wa Mashariki mwa Afrika.
Hata hivyo jina Bargaig limetokana na maneno bar, likimaanisha kupiga na baig, likimaanisha na fimbo. Katika ugomvi watu wa jamii hiyo kwa kawaida hutumia fimbo kama silaha yao muhimu ya kujihami. Utamaduni huo ni wa zamani sana na unaoendelea kutumiwa na jamii hiyo hadi sasa.
Kabila hilo la Barbaig ni moja ya makabila 19, ambayo yametokana na mchanganyiko wa watu ambao wao huita Datooga au Tatoga. Mchanganyiko huo unafanana na wa Wamasai na Wakalenjin wa Kenya. Lugha yao hujulisha kuwa wanatokana na jamii moja iliyopo katika Bonde la Nile nchini Sudan.
Pia jina Barbaig lina maana ya neno Mungu au Aseeta, ambalo linafanana na jamii ya Kalenjin, ambao wao huitwa Asiie, likiwa na maana ya jua. Maeneo hayo yote yanatokana na chimbuko au asili yake kuwa ni Mungu mzuri wa Misri wa kale, aitwaye Asis.
Jamii hiyo ya watu wa Datooga ambao ni wahamiaji kutoka pande za Kusini, wanaaminika kwamba walianza kuishi kwenye eneo hilo kuanzia miaka 3000 iliyopita. Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, Jangwa la Sahara lilipanuka na kuwa na eneo kubwa lenye ukame.
Hata hivyo, inaaminika kwamba katika Karne ya 15, Datooga walifika kwenye eneo la Mlima Elgon kwenye mpaka wa Kenya na Uganda. Walikaa hapo hadi ilipofika Karne ya 18 walipoanza kuhamia Kusini hadi kufika Tanzania.
Jamii hiyo ya Datooga waliingia nchini na kuanza kuishi kwenye eneo la Ngorongoro, kabla ya kuhamia Kusini kwenye eneo la Wamasai na hapo ndipo mgawanyo wao ukaanza wa makabila hayo.
Silika na tabia yao ya kuhamahama, bado inaendelea hadi leo, ambapo kuhamahama huko kumewafanya kupoteza maeneo yao ya malisho na mashamba ya maua, ambayo yametengeneza Hifadhi za Taifa za Serengeti na Tarangire.
Tabia za kabila hilo kuhamahama kumelifanya kuwa moja ya makabila yaliyo nyuma kimaendeleo nchini. Watu wa jamii hiyo ni wagumu wa kubadili utamaduni wao, ambao mwingine hauna manufaa. Vifo vya watoto ni vingi kutokana na kuwa na magonjwa mengi yanayowaandama.
Kwenye utafiti wake kuhusu kabila la Barbaig, Dk. Augustin Hatar wa Idara ya Sanaa na Michezo ya Kuigiza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema pamoja na kabila hilo kudumisha utamaduni wao, bado linakabiliwa na changamoto nyingi, kama vile unyanyasaji wa kijinsia, ukosefu wa elimu kwa watoto wa kike na ukeketaji.
Kwenye utafiti huo, Dk. Hatar anasema kwamba katika jamii ya Wabarbaig suala la mwanamke kuolewa kwa nguvu ni kitu cha kawaida.
Pia, anasema kupigwa kwa mwanamke na watoto ndani ya familia, hutokea mara kwa mara, hivyo vikundi mbalimbali vya ushauri na maendeleo vimeanzishwa wilayani Hanang ili kubadilisha mitazamo ya jamii hiyo.
Mojawapo ni Kikundi cha Wanawake cha Maendeleo na Ushauri cha Hanang (HAWOCODA) ambacho kilianzishwa mwaka 1993, kwa lengo la kuelimisha Wabarbaig kuhusu umuhimu wa elimu na maendeleo katika jamii yao.
Anasema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, zaidi ya kesi 400 zinazohusiana na matatizo ya wanawake na watoto zimepatiwa ufumbuzi. Zaidi ya kesi 200 za ubakaji ziliwasilishwa na kusikilizwa na pia kesi za miradhi, ndoa za utotoni, talaka, vipigo na nyinginezo ziliwasilishwa na kutafutiwa ufumbuzi. Vikundi hivyo vya kijamii na kimaendeleo, vimesaidia kubadilisha kwa kiasi fulani fikra za kabila hilo.
Hivi sasa kuna mwamko kidogo wa kuwapatia watoto wa kike elimu. Pia, ufahamu wa sheria na msaada wake, kama njia ya utatuzi wa matatizo yanayoikabili jamii, umeanza kueleweka, ingawa kubadili utamaduni wao wa mavazi na mila nyingi bado umebaki pale pale.

No comments:
Post a Comment