
Mtoto wa Salmin Amour
aachiwa huru
Na Tausi Ally
MTOTO wa rais mstaafu wa Zanzibar Salmin Amour, Amin Amour (36) na mwenzake Munir Juma (35) waliokuwa wanakabiliwa na shitaka la kujipatia dola 6,000 ( Sh69, milioni) kwa njia ya udanganyifu wameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, Rose Kangwa jana aliwaachia huru washitakiwa hao baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili ambao ni wafanyakazi wa serikali na kila mmoja alisaini dhamana ya Sh7 milioni.
Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi Boniface Edwin alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na Hakimu Kangwa aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 26, mwaka huu itakapotajwa tena.
Machi 7, mwaka huu washitakiwa walisomewa shitaka hilo kwa mara ya kwanza na kupelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana.
Awali ilidaiwa Februari, mwaka huu Mikocheni wilayani Kinondoni, washitakiwa hao kwa pamoja na wengine ambao bado hawajakamatwa walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Ilidaiwa kuwa Februari Mosi, mwaka huu, saa 10:30, Mikocheni A washitakiwa hao walijipatia kwa njia ya udanganyifu dola 6,000 toka kwa Baosheng Ge baada ya kumdanganya kuwa wananyumba kwenye kiwanja namba MKC/MCA 1207 Mikocheni A na kwamba wangempangasha wakati si kweli.
No comments:
Post a Comment