Tuesday, March 11, 2008



Kiingereza kifundishwe

kuanzia chini – Wazazi


Hellen Mlacky, Moshi
Daily News; Tuesday,March 11, 2008 @00:04


SERIKALI imeshauriwa kuanzisha somo la Kiingereza katika ngazi ya chini kuwawezesha wanafunzi kuwa na uelewa zaidi wa lugha hiyo wawapo katika elimu ya juu, ikiwa ni njia mojawapo ya kuwawezesha kuyamudu masomo yao kwa ufasaha zaidi.

Wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Pasua mjini Moshi walisema pamoja na kulingana kwa mitaala katika shule za msingi na sekondari za nchi za Afrika Mashariki, lakini Tanzania imebaki nyuma katika lugha ya kiingereza.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wenzake, Agnes Youze alisema hali hiyo imekuwa ikiwafanya baadhi ya Watanzania kujijengea kasumba ya kuwapeleka watoto wao nchi za nje, zikiwamo Kenya na Uganda kusoma elimu ya msingi na sekondari kwa madai ya kufuata elimu bora katika nchi hizo.

Youze alisema ukweli ni kwamba wazazi hao wamekuwa wakikimbilia lugha katika nchi hizo bila kufahamu elimu inayotolewa hivi sasa nchini ni bora na inakidhi mahitaji ya Watanzania.

Aidha, mzazi huyo aliwashauri Watanzania kufuta dhana hiyo potofu ya kufuata elimu bora nje ya nchi, kwa madai kwamba mitaala inayotumika ni ya aina moja badala yake waisaidie serikali katika kuboresha lugha ya Kiingereza.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo, Joseph Gakinya alisema kitendo cha kuwapeleka watoto hao katika nchi hizo pia kinadumaza utamaduni wa Kitanzania na kuwafanya watoto hao waige utamaduni wa kigeni ambao ni tofauti na maadili ya taifa.

Gakinya alisema fedha zinazotumika kuwasomesha katika nchi hizo zingesaidia kuboresha zaidi kiwango cha elimu ya Tanzania na shughuli nyingine za kijamii, ikiwa ni pamoja na kuinua uchumi wa taifa.


No comments: