Tuesday, March 11, 2008


Wanywa damu ya albino

baada ya kumuua


Na Paulina David, Mwanza

SERIKALI mkoani hapa, imesema inasikitishwa na vitendo vya baadhi ya watu vya kuwachinja albino, kunywa damu na kutoweka na viungo vyao.

Kauli hiyo ilitolewa jumamosi iliyopita na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk James Msekela, wakati wa madhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa ilifanyika Kata ya Buhongwa iliyopo Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Dk Msekela, alisema kitendo cha baadhi ya watu kuamua kuwachinja wenzao kama kuku, kunywa damu yao na kutoweka na baadhi ya viungo, kimemsikitisha kwa kuwa ni cha kinyama na kisichokuwa na chembe ya utu hata kidogo.

Kuna tukio la mauaji ya albino lilitokea huko wilayani Kwimba hivi karibuni, wauaji waliamua kumchinja albino, kukinga damu kisha kunywa na baadaye kumtenganisha miguu na mapaja na kutoweka na miguu," alisema Dk Msekela

Alisema tukio hilo binafsi lilimsikitisha kwa kuwa mauaji hayo ya kinyama yalifanyika wakati mabinti wawili wakiwa wamelala na albino huyo.

Mkuu huyo wa mkoa, alisema wakati unyama huo ukitendeka, walikuwa wakishuhudia namna ambavyo walikuwa wakikinga damu na kuinywa.

Dk Msekela, alisema mabinti hao walishindwa kufanya lolote kwa wauaji hao, kwani walianza kuwatisha na baadaye wakamfuata albino huyo na kumchinja kama kuku.

Alisema ingawa Jeshi la Polisi na serikali mkoani hapa vimekuwa vikifanya jitihada mbalimbali kukabiliana na mauaji ya kinyama, wakati mwingine wanashindwa

kutekeleza majukumu yao kutokana na mauaji hayo kusababishwa na imani za kishirikina, ambazo hazina ukweli wowote.

Alisema ni vigumu kumzuia mtu kwenda kwa mganga wa kienyeji maarufu kama sangoma, kwa kuwa,

imani yake ndiyo inayomtuma kuwa ndiye atakayemsaidia, hivyo, wananchi wenyewe wanapaswa kubadilika na kuona kuwa mambo yanayofanyika hayafai.

Hata hivyo, alisema mkoa hautaliacha tatizo hilo la mauaji ya maalbino kuendelea hivyo, umeandaa mdahalo utakaofanyika kati ya Machi 17 na 18, mwaka huu kujadili matukio ya mauaji ya kikatili yanayotokea Mwanza.

No comments: