Wednesday, March 19, 2008


Maulid njema


LEO saa 2.30 usiku Maulid ya Mtume Muhammad (SAW) yatasomwa kitaifakatika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwake Mtume (SAW).

Kisomo hicho kitafuatiwa kesho saa 10 jioni na Baraza la Maulid litakalosomwa pia mjini Tanga, huku mgeni rasmi akiwa ni Rais Jakaya Kikwete.

Umuhimu wa sherehe hizo, unafanya kesho kuwa siku ya mapumziko kwa Watanzania ambapo Waislamu wataungana na wananchi wenzao katika sherehe hizo.

Kama ilivyo kawaida, kisomo cha Maulid kinapofanyika usiku, waumini hujumuika pamoja na kusoma kwa pamoja na kesho yake hufanya hivyo hivyo na kuhitimisha sherehe hizo.

Kwa siku zote hizo ni wazi kuwa watu watalazimika kutoka majumbani saa za usiku na kesho yake alasiri, hali ambayo mara nyingi huwa ni tete kiusalama wao na wa mali zao.

Hivyo ni vizuri wakati wa sherehe hizi kama ambavyo imekuwa ikihimizwa na Jeshi la Polisi nchini, kuhakikisha kuwa kuna watu wanabaki majumbani kulinda mali.

Lakini pia ni wakati ambao wenye vyombo vya moto vya kusafiria kuhakikisha kuwa wanakuwa waangalifu kwa vyombo vyao, lakini pia kwa waendao kwa miguu barabarani.

Kwa kuwa huu ni wakati wa furaha, ni wazi kuwa kila mmoja angependa afurahie kiwango chake, lakini kwa kawaida kila kitu kinapozidi kipimo huwa na madhara.

Hivyo tunawashauri wale ambao wanaamini katika kupata kinywaji nyakati kama hizi, basi waangalie kipimo cha kinywaji wasije kujikuta wanaingia katika matatizo yasiyotarajiwa. Tunakutakieni mapumziko mema.

No comments: