Wednesday, March 19, 2008



Wateja TANESCO wabambikiwa bili




IMEDHIHIRIKA kwamba Shirika la Umeme nchini (TANESCO) limekuwa likikusanya mabilioni ya fedha kutoka kwa wateja wake, baadhi yao wakiwa wamebambikiwa bili za mabilioni.

Kutokana na hali hiyo wateja wengi wamekuwa wakilalamika kwamba matumizi yao ya umeme yanapishana mno na viwango vya gharama za umeme wanazotakiwa kulipa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba shirika hilo la umeme sasa limo kwenye ugomvi mkubwa na baadhi ya wateja wakubwa na hata wadogo hasa baada ya kuanza kampeni ya kata umeme Januari mwaka huu. Wateja wanadai ama kubambikiwa bili kubwa ama kupelekewa bili zisizokuwa zao.

Hata Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, ambaye amekuwa mhogo mchungu kwa wakwepaji kulipa bili za umeme, Dk. Idris Rashid amekiri kwamba fedha hizo zinazodaiwa ni kitu kama sh bilioni 100 hivi na kwamba baadhi yake haiwezekani kuzidai kwa sababu ni za kubambikiwa na zimelimbikizwa kwa muda mrefu unaofikia miaka 10.

Dk. Rashid ambaye alikuwa akizungumza na gazeti moja jana alisema hali hiyo imesababishwa na uwekaji takwimu mbovu na baadhi ya wafanyakazi wasiokuwa waaminifu.

"Nyingi haziwezi hata kudaiwa kwa sababu nyingine wateja walibambikiwa. Unakuta mtu ana kibanda kidogo, lakini amewekewa deni la Shilingi milioni kumi, jambo ambalo haliwezekani," amekaririwa akisema.

Wakati kampeni ya kata umeme imeanza Januari mwaka huu, tayari TANESCO imeingia kwenye ugomvi mkubwa na wateja wake.


Mjini Morogoro magari 22 ya TANESCO yalikamatwa kwa amri ya mahakama wiki iliyopita baada ya shirika hilo kukikatia umeme kiwanda cha Morogoro Canvas Mill kwa madai ya kushindwa kulipa bili ya sh milioni 600 ambayo kiwanda hicho kinadai ni ya kubambikiwa.

Wiki iliyopita Mahakama Kuu kitengo cha Biashara ilikataa kurejeshwa kwa magari hayo ikiitaka TANESCO kwanza iwakilishe ombi lake kwa maandishi. TANESCO ilidai kwamba inachelewa kurudisha umeme hadi kwanza ifunge mita mpya katika kiwanda hicho.

Shirika hilo la umeme limekumbwa na dhahama kubwa kwa siku za karibuni huku makampuni mengi yaliyosaini mkataba wa kibiashara yakisakamwa kwa kusaini mikataba ya kifisadi na kuzidi kudidimiza kampuni hiyo kimapato.

Wafanyakazi wa shirika hilo siku chache zilizopita walitishia kuandamana wakidai kwamba shirika lao limekuwa kapu la kuchotea fedha kuneemesha watu wachache kwa manufaa yao binafsi.

Wakatoa mfano wa kampuni ya Net group Solution ambayo wakati wa enzi za utawala wa Benjamini Mkapa waliipinga lakini ikaingizwa kimabavu kwa nguvu za dola.

Pia walitoa mfano wa mikataba ya IPTL na Richmond ambayo walisema yote ililenga kulifilisi shirika na kuwaacha wafanyakazi hao katika lindi la umaskini.

No comments: