Wednesday, March 05, 2008

MENEJA ALINIBAKA

NA KUNIAMBUKIZA

UKIMWI

Mwandishi, Zubagy Akilimia


Msichana mwenye umri wa miaka 14, Aisha (Sio jina lake) ameingia kwenye janga la mateso kwa kubakwa na meneja wake wa baa aliyokuwa akifanyia maeneo ya Manzese Midizini na sasa ameamua kuelezea sababu ambazo zinamfanya akiri wazi kuwa anasubiri kifo. Huku akionekana mwenye majonzi, na masikitiko makubwa anaelezea maisha yake akitokwa na machozi. Je, nini kilimkuta msichana huyu mdogo? Ungana na mwandishi akusimulie yaliyomkuta Aisha katika maisha yake.

Nimezaliwa Wilaya ya Karatu mkoani Manyara, kabila langu ni Mmbulu, nimeamua kuelezea siri inayoutesa moyo wangu kwa kipindi kirefu sasa, toka nimetoka tumboni mwa mama yangu sikutegemea yangenikuta haya yanayonitoa machonzi…” ndivyo alivyoanza Aisha na kushindwa kuendelea huku akibubujikwa na machozi kuashiria alikuwa na jambo zito moyoni, mwandishi akachukua muda kumtuliza aweze kusema kilichopo moyoni mwake jamii iweze kufahamu na kumsaidia kwa wenye uwezo wa kufanya hivyo. SASA Endelea…

Pamoja na umri wangu mdogo bado ninazo kumbukumbu nzuri nilipotoka na yaliyonikuta maishani mwangu, katika ndoto zangu sikujua iwapo ningeweza kuwa mbali na wazazi wangu, hata hivyo kwa masikitiko makubwa sana naelezea kisa hiki ambacho kila nikikumbuka niliyotendewa, moyo wangu unakosa amani ya roho hadi siku yangu yakuondoka duniani itakapofika.

Naweza kusema kuwa baba yangu alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa wilayani Karatu, (Jina tunalihifadhi), maduka na magari aliweza kuyamiliki, mama yangu hakuwa na kazi, zaidi ya kazi ndogo ndogo za nyumbani.

Nilipokuwa na umri wa miaka nane nikiwa darasa la pili, niliweza kugundua mambo mengi yaliyokuwa yakifanyika ndani ya familia yetu, mwanzo wazazi wangu waliishi kwa amani na upendo, baadaye amani na upendo ikapotea, hata hivyo sikuweza kujua ni kwanini hali hiyo ilitokea.

Kila leo baba alichelewa kurudi nyumbani na aliporejea hali yake haikuwa nzuri, alionekana amelewa kupita kiasi akitoa matusi bila kujali kuwa yeye ni baba anatakiwa kuwa mfano kwa familia.

Muda mwingi baba alikuwa akirejea nyumbani akiwa amelewa sana, tena saa tisa na wakati mwingine alirejea nyumbani asubuhi wakati tunaenda shule, alikuwa mgumu kutoa hela za matumizi na kusababisha tunywe chai kavu, yaani isiyo na hata kipande cha Andazi.

Kauli ya mama siku zote ilikuwa ni kumsihi baba apunguze ulevi na kuijali familia, baba alichukizwa sana na ushauri huo na badala yake alimuadhibu kwa kosa la kumpangia namna ya kuishi, ikawa kila anaporejea humpiga sana mama hadi kupoteza fahamu.

Hali hii ilinisikitisha sana, na kunifanya nimuonee huruma mama yangu, sikuweza kuingilia suala la wazazi wangu, licha ya kufikiria namna gani ningeweza kulitatua pamoja na umri wangu mdogo, hata hivyo nilibaki nikiishia kubabaika tu.

Siku zilivyozidi ndivyo maisha ya ndoa ya wazazi wangu yalivyozidi kuwa ya ugomvi, kuna wakati nilishindwa kuvumilia kuona baba anampiga mama kila siku bila hatia, nikamuuliza kwa uchungu nikitokwa na machozi, jibu alilonipa ni kwamba mama ana kiburi na hujifanya mjuaji kwa kila jambo huku akijaribu kumwendesha mithili ya gari bovu wakati yeye ni kichwa cha familia.

Ukweli mama hakuwa na kosa, isipokuwa alipata kipigo kufuatia tabia ya baba kulewa kupita kiasi na kuufanya mwili wa mama kuwa ngoma kwa kipigo.

Kila ugomvi ulipotokea hasara ya kuvunjika kwa Tv, Redio na simu za mkononi ilitokea, kuna wakati kutokana na akili zangu za kitoto nilimtaka mama kurejea nyumbani kwa baba.

Mama aligoma na kudai asingeweza kurudi mpaka atakapopewa talaka au kifo kitakapomkuta, kauli hiyo kwangu ilizua kilio, nilihisi ipo siku mama angeweza kuuawa au kuvunjwa mkono kama si mguu kutokana na kupigwa kila siku bila kosa.

Maisha ya mfumo dume yaliendelea ndani ya familia yetu, kila siku mama alipatwa na jakamoyo kwa mateso aliyopata kwa baba, uso wake haukuwa na tabasamu hata kidogo, alikosa raha na kwamba baba alikataa kutoa pesa za matumizi na kumtaka afanye kazi.

Miezi ilizidi kwenda ndipo baba akaoa mwanamke mwingine ambaye alipatiwa moja ya chumba kilichokuwa cha wageni, miezi sita baadaye mke mdogo niliyekuwa namwita mama mdogo akadai kuwa mama yangu anatabia ya kuleta wanaume na kufanya nao mapenzi katika chumbani walicholala na baba.

Maneno hayo yaliniumiza moyo wangu, sikuona sababu ya kwenda shule siku hiyo nilijua mama yangu angepigwa.

“Mwanangu, najua utateseka sana lakini Mungu atakulinda,” mama aliyazungumza hayo huku akitokwa na machozi, alijua ni kiasi gani angeadhibiwa na baba aliyeonekana kumpenda mke mdogo. Sikuweza kumjibu jambo lolote zaidi kuungana naye kulia.

“Mwanangu, usijali lakini Mungu anajua sijafanya jambo hili,” mama alinieleza akitokwa na machozi, sauti yake ilikauka kwa kulia muda mrefu.

Kesho yake, baba alioneshwa na mama mdogo mwanaume aliyedaiwa kuingizwa chumbani kwake, mwanaume huyo alikiri kufanya ngono na mama chumbani kwa baba na kuomba asamehewe kuwa hakujua ni mke wa mtu, na kwamba walianza uhusiano huo ambao mara nyingi walikutana kwenye nyumba za wageni.

Ukweli, siku ambayo mama mdogo alipodai kuwa mama aliingiza mwanaume nilikuwepo nyumbani na sikuona mgeni yeyote nikaamini moja kwa moja yalikuwa maneno ya uchonganishi ya kutungwa kwa nia fulani.

“LEO LAZIMA NIMUUE MAMA YAKO!” Yalikuwa maneno ya baba akiwa ameshika fimbo ndefu na Panga, niliogopa sana na kujikuta nikitetemeka mwili mzima.

Nikiwa sebuleni muda mfupi baba alivyoingia nilimsikia mama akipiga kelele akiomba msaada, sikuweza kuvumilia, nilijongea na kusimama mlangoni ambako niliendelea kusikia mama akipiga kelele akiomba asiadhibiwe kwani hakuwa na kosa, baadaye kwa kutumia jicho moja nilichungulia kupitia tundu la funguo mlangoni, fimbo zote alizochapwa ziliishia kichwani na mgongoni ambako baadaye niliona damu nyingi zikimtoka puani, midomoni, masikioni na kichwani hadi gauni zima likalowa damu.

Kuna wakati sasa mama alikosa nguvu na kudondoka chini akiomba asaidiwe kwani mauti yangemkuta, kabla ya kudondoka mama alisema maneno haya.

“Mume wangu unaniua kwa kusikiliza maneno ya uongo ya mke mwenzangu! Najua kitu gani anachotaka na keshafanikiwa…nakufa lakini utanifuata siku si nyingi, na yeye pia atakufa kama nilivyokufa mimi, nipeleke nikafie msikitini…Eeh Mungu nisaidie…” Maneno haya yalimtoka mama uso wake ukiwa umefunikwa na damu nyingi zilizomfanya ashindwe kuona vema. Nililia sana nikawa nabubujikwa na machozi, nilipojaribu kufungua mlango, baba aliufunga kwa ndani.

Je, mama Aisha atakufa? Mke mdogo atafanya nini? Tukutane wiki ijayo. Kwa maoni piga simu 0712 313191.


Toka GlobalPublishers TZ.



No comments: