Monday, March 03, 2008



Mkataba wa Mkono

BoT wasitishwa


*Ni wa kiutetea mahakamani

*BoT yatangaza zabuni mpya

*Gavana asema wamekubaliana

* Asema wanatafuta unafuu

Na Ramadhan Semtawa


KATIKA haraka zake za kujisafisha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesitisha mkataba kati yake na Kampuni ya Uwakili ya Mkono.

Kufuatia uamuzi huo, BoT mwishoni mwa wiki ilitangaza zabuni ya kutafuta kampuni ya uwakili ambayo itakuwa ikifanya kazi mbalimbali za benki hiyo kwa kushirikiana na wanasheria wake.

Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu aliithibitishia gazeti hili jijini Dares Salaam kuhusu uamuzi huo wa kutangaza zabuni ya kutafuta kampuni mpya.

Kampuni ya Uwakili ya Mkono inaongozwa na Nimrod Mkono mbunge wa Musoma Vijijini, ambaye amekuwa akiitetea serikali katika kesi ya Valambhia ambaye aliuzia vifaa vya kijeshi.

Hata hivyo, Mkono pia amekuwa akitajwa na wapinzani kwamba amekuwa akilipwa zaidi ya sh 500,000 na BoT kwa sasa moja katika kesi hiyo.

Akizungumzia uamuzi huo, Profesa Ndulu alisema BoT imetangaza zabuni hiyo kutafuta unafuu.

Hata hivyo, Profesa Ndulu alipoulizwa iwapo unafuu huo anaozungumzia unatokana na kuona gharama za Kampuni ya Mkono kuwa kubwa, alijibu: "Si unajua ukitangaza zabuni unakuwa na unafuu, ushindani unasaidia kuleta unafuu."

Alisema kabla ya uamuzi huo pande mbili zilikutana na kukubaliana.

"Ndiyo tumesimamisha mkataba, lengo ni kujipanga upya na vizuri, na hayo ni makubaliano ya pande zote mbili, si uamuzi wetu kwa kuwa mkataba unazihusisha pande zote mbili (BoT na Kampuni ya Uwakili ya Mkono," alisisitiza.

Alisema mara nyingi inapotangazwa zabuni katika mfumo wa ushindani, huchangia punguza gharama za kazi katika mkataba.

Alifafanua kwamba, mkataba uko wazi kwamba upande mmoja unaweza kusimamisha mkataba wakati wowote baada ya kukaa na kukubaliana.

Kuhusu kampuni hiyo kuendelee kuitetea serikali katika rufaa yake dhidi ya Valambhia, alisema pia wamesimamisha.

Aliongeza kuwa kuna taratibu ambazo zimekwishafanyika katika utetezi wa kesi hiyo akasema si sahihi kuzungumzia kwa undani kwani iko mahakamani.

Chini ya uongozi wa gavana Daud Ballali, BoT ilikuwa na taswira ya ufisadi mbele ya Watanzania huku makampuni na watu mbalimbali wakijitoe mamilioni ya shilingi kwa njia mbalimbali.

Uamuzi huo wa BoT chini ya uongozi wa Profesa Ndulu kuisaifisha benki, kuanzia kwa wakurugenzi wake na hatimaye kusimamisha mkataba huo, unaonekana kama pambazuko jipya kuelekea kuitakasa taasisi hiyo nyeti ya umma ambayo imechafuka kwa tuhuma za ufisadi.

Wakati hayo yakiendelea tayari mchakato kurejesha zaidi ya Sh133 bilioni, zilizoibwa katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya benki hiyo unaendelea, hadi mwisho mwa wiki iliyopita zilishakusanywa Sh50 bilioni.

Wiki iliyopita vigogo watano wa vitengo mbalimbali vya benki hiyo walisimamishwa kazi katika hatua ya kuhakikisha kuwa benki hiyo inasafishwa.

Sambamba na hilo pia alipangua safu ya Wakurugenzi wa matawi yote nchini isipokuwa Mwanza.

No comments: