Monday, March 03, 2008



Mtoto wa Rais matatani

akidaiwa kutapeli



Na Pauline Richard

MTOTO wa Rais Mstaafu wa Zanzibar Munir Amor (35), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya Ilala kujibu shitaka la kujipatia fedha taslimu Sh3 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Inspekta wa Polisi Denis Mujumba alidai mbele ya Hakimu Janeth Kinyage kuwa Februari 8 mwaka huu, saa 10.00 jioni katika ofisi za Mkali and Company Advocate zilizopo Mtaa wa Garden na Ohio, jijini Dar es Salaam mshitakiwa akiwa na wenzake ambao hakufikishwa mahakamani hapo walijipatia kiasi hicho cha fedha toka kwa Angela Mtimbili.

Mujumba alidai kuwa washitakiwa hao wanadaiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha baada ya kumdanganya Angela kuwa wangempangisha nyumba iliyopo Mikocheni A jijini Dar es Salaam wakati ni uongo.

Hata hivyo mshitakiwa baada ya kusomewa shitaka alikana na mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Machi 5, mwaka huu itakapotajwa tena na upande wa mashitaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, mshitakiwa yupo nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

Wakati huo huo, mkazi wa Tabata Liwiti Ruben Katindasa (53), amefikishwa mahakamani hapo akituhumiwa kumpiga na kumjeruhi Matilda Katindasa kwa panga kichwani.

Inspekta wa Polisi Mussa Gumbo alidai mbele ya Hakimu Mwanaisha Chande kuwa Februari 14 mwaka huu, saa 4.30 usiku mshitakiwa alitenda kosa hilo.

Hata hivyo mshitakiwa baada ya kusomewa shitaka alikana na Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Machi 4, mwaka huu itakapotajwa tena kwa kuwa upande wa mashitaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamlika.

No comments: