Saturday, March 15, 2008

Mwanyika hana budi

kutujibu maswali haya



Lula wa Ndali-Mwananzela

BAADA ya kusoma taarifa ya Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika kuhusu maendeleo ya uchunguzi kuhusu EPA, iliyotolewa siku ya Jumapili, badala ya kupata majibu ya hoja nilizoibua wiki iliyopita, nimejikuta nikiongezewa maswali juu ya maswali.

Nilipojaribu kuelewa Bw. Mwanyika alikuwa anajaribu kutuambia nini, nikajikuta badala ya kutoa majibu ndio ameongeza maswali zaidi.

Ndipo nikaamua kuwa badala ya kuyaacha maswali hayo yaniumize kichwa kwanini basi nisimuulize mtu pekee anayeweza kunipatia majibu. Ninaamini maswali yote haya nitakayoyauliza yana majibu na Mwanasheria Mkuu, ambaye ni msomi, nina uhakika, akijisikia vizuri, anaweza kutoa majibu. Na sitashangaa kuwa watu wengine na wenyewe wana maswali kama haya. Na kwa vile Bw. Mwanyika amesema “wanahabari” wasiwe na haraka, nimeona na miye nisichelewe!



MWANASHERIA Mkuu, Johnson Mwanyika

Kwanza kabisa, kwa nini Bw. Mwanyika alikubali kuwemo kwenye tume/kamati/task force ya kuchunguza uhalifu ambao tayari Rais keshasema ni “uhalifu”? Kama Rais wa Jamhuri ya Muungano na Amiri Jeshi Mkuu amesema kuwa mabilioni yaliyochotwa EPA yalichukuliwa “kiuhalifu” kwa nini basi Mwanasheria Mkuu anasema “watuhumiwa wa upotevu wa fedha” kana kwamba fedha zilikuwepo halafu zikapotea kama mazingaombwe?

Uchunguzi wa Ernst & Young umeonesha fedha hazikupotea, zimechukuliwa na watu wanaojulikana, na kiasi hadi senti ya mwisho kinajulikana. Kwa nini basi iwe “upotevu” kana kwamba hatujui fedha zimepoteaje?

Pili, Kwa nini Mwanasheria Mkuu alisubiri hadi Rais aunde kamati ndiyo na yeye ashirikishwe kwenye uchunguzi huo? Je, Bw. Mwanyika hawezi kuanzisha uchunguzi wa kosa lolote la kihalifu kwa mujibu wa sheria iliyounda ofisi yake na ile ya DPP? Kwa nini Mwanasheria Mkuu asubiri hadi Rais aagize ndiyo na yeye aonekane kufanya kazi ambayo angeifanya miezi michache iliyopita?

Je kama Rais asingeagiza kuundwa kwa timu hii ya Inspekta Jenerali, Mkurugenzi wa TAKUKURU na yeye Mwanyika, ingekuwa mwisho wa suala hili?

Na swali la tatu linaendana na hilo la pili. Je Mwanasheria Mkuu ana madaraka ya kuchunguza jambo lolote bila ya kuomba kibali toka Ikulu? Kama haoni ulazima wa hatimaye kuzungumza na watunga sheria wetu wampe madaraka hayo? Kama anayo (au anaamini anayo) ni kwa nini hadi hivi sasa hajafungua uchunguzi wa Richmond hadi kina Mwakyembe wafanye hilo?

Kwa nini hajafungua uchunguzi wa kihalifu wa Meremeta, Mwananchi Gold, Tangold, na Deep Green? Au anasubiri “aitwe Ikulu” au kina Ernst and Young wengine waje ndio na yeye achangamke?

Swali la nne ambalo ningependa Mhe. Mwanyika atupatie majibu ni suala zima la EPA. Hadi hivi sasa uchunguzi wa Ernst & Young umeangalia mwaka mmoja tu wa 2005/2006 na umegundua wizi huo. Je Bw. Mwanyika haoni haja ya kuanzisha uchunguzi kwa miaka kumi iliyopita kwenye akaunti hiyo? Au anasubiri hadi Rais na Bunge vifanye hivyo?

Kama hana uwezo wakufanya hivyo hadi mtu alalamike (kama ile Sekretariati ya Maadili ya viongozi) anaonaje kutoa pendekezo la kisheria la kufungua upelelezi na uchunguzi kwenye Benki Kuu?

Katika maelezo yake ya Jumapili, Bw. Mwanyika alisema hivi: “Tunapenda kuueleza umma kwamba uchunguzi wetu hadi hivi sasa unaonyesha kwamba wahusika wakuu ni makampuni. Kisheria, makampuni hayo ni mtu yaani ‘Legal Person’. Hata hivyo, makampuni hayo ni tofauti na mtu wa kawaida. Kampuni katika maana hii, inajitegemea yenyewe.”

Tatizo katika mawazo haya ya Mwanasheria Mkuu ni kwamba yanagongana na taarifa ya awali ya Rais Kikwete. Taarifa ya awali ya Rais ilisema hivi kuhusu hii EPAL: “Kuchunguza na kuchukua hatua zipasazo za kisheria kwa makampuni na watu waliohusika na uhalifu huu.” Msisitizo hapo uko kwenye “makampuni na watu”. Hivi Bw. Mwanyika anafikiri kuwa hakuna Mtanzania anayejua maana ya kampuni kisheria?

Hivi katika taarifa yake hiyo, ambayo haikuonesha weledi wa aina yoyote ile, anaamini kuwa Watanzania wanaweza kuamini kuwa “makampuni” ndiyo yaliyotembea na kalamu mkononi, na kwenda kughushi Benki Kuu?

Je yawezekana kauli yake hiyo ya juzi ina lengo la kuuandaa umma kwa ‘mazingaombwe ya mwaka’ kuwa siku zitakapofika watuambie kuwa “makampuni yamefutwa, yamechukuliwa hatua na kurudisha fedha zote, lakini watu wenyewe hawakuhusika na uhalifu huo”?

Kauli yake kuhusu “makampuni” pia ina lengo la kupotosha umma. Makampuni yote hayako sawa mbele ya sheria. Na si lengo langu hapa kutoa funzo au elimu ya biashara lakini kwa msomi kama Mwanyika anaelewa wazi kuwa yapo makampuni ambayo huwezi kuyatenganisha na mmiliki wake; yaani kama kampuni ikikosea mwenye kubeba lawama na madeni ni mmiliki.

Pia yapo makampuni ambayo yana wahusika zaidi ya mmoja na yako katika mifumo mbalimbali. Hivyo siyo kweli kuwa makampuni yote ni “watu” nje ya wamiliki wake.

Isipokuwa kama Bw. Mwanyika yuko tayari kuwaambiwa Watanzania kuwa makampuni yote 22 yaliyohusika na uhalifu (maneno ya Rais siyo ya kwangu) huu yanaweza kutenganishwa na wamiliki wake. Kama mojawapo ya makampuni hayafungwi na hiyo nadharia ya “makampuni ni legal person” basi maelezo ya Bw. Mwanyika yalikuwa ni ya kupotosha.

Hata hivyo, kama tukiamini kwa dakika chache kuwa alichosema ni kweli; kimsingi anafanya kauli ya Rais ya kusema “makampuni na watu” kuwa ni ya uongo au ina makosa. Kama ni hivyo tunatarajia Bw. Mwanyika awaeleze Watanzania kuwa kauli ya awali ya Rais haikumaanisha “kampuni na watu” bali “watu na watu”!

Hata kama makampuni hayo ni “legal persons” hata hivyo kuna sheria ambazo zinatumika sehemu nyingine za kufunua pazia la wamiliki wa makampuni (piercing of corporate veil) ambapo sheria hiyo inawezesha mahakama kuwawajibisha wamiliki wa makampuni na siyo makampuni tu. Je, Tanzania tunayo sheria kama hiyo, na kama tunayo Bw. Mwanyika anaona ugumu gani kuitumia kuwapata “wabaya wetu”?

Kama hatuna haoni ni sababu tosha ya kuhakikisha kuwa kabla ya mwaka huu kwisha Tanzania inaingiza sheria hiyo kwenye vitabu vyake? Hata hivyo, kama tunayo, haoni kwamba maelezo yake kuwa “makampuni haya ni watu wa kisheria” tofauti na wamiliki wake ilikuwa na lengo la kunyamazisha hoja wakati anajua ipo sheria inayoweza kuyafunua makampuni na kuonesha wamiliki wake na hao wamiliki kubebeshwa madeni na mzigo wa makampuni yao?

Hata hivyo, kuna swali jingine ambalo limetokana na mojawapo ya kauli zake za mwisho siku ya Jumapili; Bw. Mwanyika alisema hivi “Kazi inayofanyika hivi sasa, ni uchunguzi wa kina kuhusu maafisa wa makampuni hayo ili kufahamu ni kitu gani kilichosababisha hali hiyo kutokea.” Sasa, sijui ni mimi au ndio uzee wenyewe unanijia kwa kasi. Yaani Bw. Mwanyika na timu yake wanachunguza ili kufahamu “ni kitu gani kilisababisha hali hiyo (a.k.a wizi) kutokea”?

Hivi mwizi anapoiba anasababishwa na nini? Na ukisha jua utampeleka wapi; hospitali, kumsomesha, au kumuwekea mikono?

Bw. Mwanyika tafadhali utuambie kuwa hamchunguzi ili mfahamu kuwa tamaa ya mali na utajiri wa haraka haraka ndio ulisababisha hili. Kama Rais aliunda timu hii ili kufanya uchunguzi wa chanzo cha ufisadi huu naomba niwarahisishie kazi. Walioiba EPA walifanya hivyo si kwa sababu wamepagawa na “pepo la wizi” bali kutokana na tamaa yao ya kuvuna wasichopanda na kula wasichopika. Ni tamaa ya kujipatia utajiri kwa njia ya ulaghai! Hili halihitaji miezi sita kuchunguzwa.

Pia naomba kumuuliza Bw. Mwanyika kuwa mojawapo ya maagizo ya Rais kufuatia uchunguzi wa EPA ilikuwa ni kuamuru kusitisha mara moja malipo na shughuli zote za akaunti ya EPA. Kama akaunti hii imefungwa na hakuna malipo yoyote (ya kuingia na kutoka) hivi bilioni 50 zilizorudishwa zimerudishwa kwenye akaunti ya nani na kwa misingi gani?

Na kabla sijamaliza naomba kuuliza kuwa uchunguzi huu wa timu ya Mwanyika unafanywa kwa amri ya mahakama gani, na uwezo wao wa kuwaamuru au kuwashawishi watu/makampuni haya kurudisha fedha hizi nje ya mahakama unatokana na sheria ipi?

Inawezekana sheria hiyo ipo. Kama ipo, tunaomba tuambiwe ni sheria ipi. Tusije kuwa tunafurahia watu kurudisha fedha lakini wanafanya hivyo kwa sababu ya vitisho vya nje ya mahakama. Na tukikubali kuwa kuna Watanzania wanaolazimishwa kuachilia mali yao kwa sababu ya tuhuma tu bila kuzithibitisha tuhuma hizo mahakamani, matokeo yake ni kama hayo yaliyotokea Tabata ambako kuna mtu alifikiri ana uwezo wa kuamuru kuvunja nyumba za watu kwa sababu yeye anakaa mbele ya meza moja kubwa!

Tukikubali kuwa kina Timu ya Mwanyika wanaweza kufanya wanavyofanya sasa hivi, kwa nini basi tusikubali kulivunja Jeshi la Polisi na kuanza kuunda timu za Rais za kufuatilia uhalifu?

Kama Polisi wetu wameshindwa kufanya kazi yao hadi waambiwe na Rais, kuna maana gani kuwa na jeshi hilo ambalo haliwezi kufanya jambo hadi “waitwe Ikulu”? Kama Rais ana nguvu hizo za kuamuru nani achunguzwe, bila ya shaka anazo nguvu pia za kuamuru “nani asichunguzwe”.

Kwa kadiri ninavyofahamu ni kuwa nguvu alizonazo kikatiba ni zile za kutoa msamaha kwa kosa lolote lile na kwa mtu yeyote yule. Hizi nyingine zinatoka wapi?

Na mwisho, naomba nimuulize Bw. Mwanyika; ni kwa nini Watanzania wamuamini yeye kuongoza suala hili wakati Kamati Teule ya Bunge kuhusu Richmond imemuonesha kuwa sio tu alishindwa kusimamia maslahi ya Taifa lakini ripoti yake kamati hiyo kuhusu mikataba sita ya Tanesco na makampuni kadhaa ya nishati ni mibovu kupindukia na ambayo inashangaza kama Mwanasheria wetu Mkuu hata aliipitia.

Kwa nini, Bw. Mwanyika aendelee kuongoza timu hiyo wakati Bunge lenyewe halina imani naye? Kwa nini asijiuzulu na kumpisha Mwanasheria Mkuu mpya kufanya kazi hiyo; kwani yeye tayari ana madoa na matope mengi.

Je, anaamini kuwa pasipo yeye kama Mwanyika timu hiyo haitaweza kufanya kazi zake? Kwa nini asiwe na ujasiri wa kumuomba Rais amuondoe kwenye nafasi hiyo ili Mtanzania mwingine afanye kazi hiyo pasipo kuwa na mapakacha ya ufisadi mgongoni?

Nadhani wakati umefika kwa Bw. Mwanyika kuomba kujiondoa kwenye suala hili la EPA kwani wananchi hawana imani naye kutokana na kutajwa na ripoti ya Mwakyembe kuwa kama Mwanasheria Mkuu alishindwa kuisimamia mikataba ya serikali ipasavyo na matokeo yake ni mkataba fisadi wa Richmond.

Endapo atafanya hivyo, atajijengea heshima ya kuwajibika na kuonesha kuwa cheo cha Mwanasheria Mkuu siyo cha mtu binafsi na ya kuwa ashikaye nafasi hiyo lazima awe safi siyo tu kwa kudhaniwa kuwa ni safi, bali kwa kuonekana kuwa ni safi pasipo tetesi za uchafu juu yake.

Natumaini maswali haya yatasaidia katika kutafuta ukweli kuhusu EPA.


Niandikie: lulawanzela@yahoo.co.uk



No comments: