Friday, March 28, 2008



Norway kusaidia bilioni 1.8/-

sekta ya asasi za kiraia


Daily News; Friday,March 28, 2008 @00:04


SERIKALI ya Norway kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje, imekubali kutoa Dola za Marekani 1,578,747 ( Sh 1,881,082,554) kwa ajili ya kusaidia Taasisi ya Mfuko wa Vyama vya Kiraia (Foundation for Civil Society) katika kuimarisha sekta ya asasi za kiraia nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, John Ulanga, msaada huo ambao umelenga kuziimarisha asasi nchini kwa miaka mitatu, upo katika mkataba uliosainiwa kati ya Balozi wa Norway, Jon Lomoy na Ulanga mwenyewe.

“Kiwango hicho kilichokubaliwa kitatolewa kwa awamu kufuatana na maombi yatakayotolewa na taasisi hii na kiwango cha kwanza cha NOK 1,500,000 kitatolewa mara tu baada ya kusaini mkataba,” alisema Ulanga. Alisema Norway ni miongoni mwa wafadhili wakuu wa taasisi hiyo tangu mwaka 2004, na hadi mwaka jana, ilikuwa imeshaisaidia Taasisi hiyo Dola za Marekani 945.951.

Taasisi hiyo hujenga uwezo wa asasi za kiraia kwa mwelekeo wa kuziwezesha kuchangia katika kuwashirikisha wananchi vyema katika mchakato wa kidemokrasia na kuwafanya waelewe, wadai na wapate haki zao, alisema.

Alisema tangu mwaka 2003 ilipoanzishwa taasisi hiyo hadi Desemba 2007, imeidhinisha ruzuku yenye thamani ya Sh bilioni 20 na kati ya hizo Sh bilioni 14 zimeshatolewa kwa wafadhiliwa wa taasisi hiyo.


No comments: