Tuesday, March 25, 2008


Rostam: Simshangai Mtikila


*Alisema Nyerere anatoka Rwanda, Mkapa Msumbiji
*Aunga mkono hoja ya kutenganisha biashara, siasa

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Igunga, Rostam Aziz, amesema hashangai hatua ya Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, kusema yeye si raia wa Tanzania.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii kutoka Tabora ambako amekwenda kwa ajili ya mapumziko ya Pasaka na kutembelea wapiga kura wake, Rostam alisema Mtikila ametambua umuhimu wake kisiasa na kijamii ndiyo maana amesema hayo aliyoyasema.

Mtikila ametambua umuhimu wangu katika taifa hili hadi akaamua kuniweka kundi moja na Mwalimu Nyerere na Mheshimiwa Mkapa.

Huyu rafiki yangu Mchungaji ambaye si Afisa wa Uhamiaji, aliwahi kusema Nyerere ni Mnyarwanda na pia akasema Mkapa ni wa Msumbiji, sasa anasema Rostam ni Muirani. Ni dhahiri manesi wa Ndala Mission walioshuhudia nikizaliwa watakuwa wameshangaa sana kusoma maneno ya Mtikila, alisema Rostam.

Kuhusu uhusiano wake na Kampuni ya Richmond, alisema siasa za Tanzania zinatumika vibaya. Alisema yeye anafanya biashara ya ukandarasi, amejenga miradi mingi hapa nchini, lakini huo wa Richmond asiokuwa na uhusiano nao hata kidogo ndiyo unaochukuliwa kama kashfa dhidi yake.

Kama nilivyosema mwanzo naendelea kusema kuwa sihusiki na Richmond. Na bado nasema ungekuwa mradi wangu nisingeshindwa kuujenga kwa mwaka kampuni zangu zinalipa kodi serikalini zaidi ya Sh bilioni 100. Kwa maana hiyo kodi tu ninayolipa ndani ya miezi 12 ingetosha kabisa kuutekeleza mradi wa Richmond, alisema na kisha akaongeza:

Siasa ni mchezo wa ajabu sana. Richmond ambayo sihusiki wananibambikia kwamba ni kampuni yangu, lakini mradi wanaousifia sana kwenye Ripoti ya Kamati ya Mwakyembe wa Watsila Ubungo, nimeujenga mimi mwaka huu upo next to (karibu na) Dowans, ambapo pia niliomba kazi lakini sikupata. Huo wa Watsila ambao wanausifu hawanihusishi nao.

Alimshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyoteuliwa na Spika Samuel Sitta kuangalia taratibu za zabuni ya kupata kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, Harrison Mwakyembe wakati akifanya majumuisho bungeni hakumhusisha Rostam na umiliki wa Richmond.

Mwakyembe alisema bayana kuwa Richmond si yangu, lakini wapi bwana, bado watu wanaendelea tu. Huu ni mchezo wa kisiasa tu, alisisitiza Rostam.

Kuhusu wazo la Rais Jakaya Kikwete la kutenganisha biashara na siasa, Rostam alisema yeye anakubaliana na wazo hilo, kwasababu katika nchi nyingi za dunia ya tatu mifumo haijakomaa kutenganisha biashara na siasa hivyo dawa pekee ni hiyo aliyokuja nayo Mheshimiwa Kikwete.

Alisema wapo baadhi ya watu wanaoingia kwenye siasa kwa nia ya kujiongezea pato au kuboresha biashara zao, badala ya kutumikia wananchi.

Sina tatizo na mwelekeo wa rais katika hilo. Kuna dhana nyingi hapa, nyingine sahihi na nyingine si kweli. Wapo wanaoingia kwenye siasa kufanya biashara, na wengine ni wafanyabiashara lakini wanaingia kwenye siasa kwa mapenzi yao ya siasa au kutumikia wananchi au vyote viwili.

Rostam alisema wafanyabiashara wote ni wajanja, na hakuna mfanyabiashara unayeweza kumfuatilia ukamkosa. Awe Rostam, Mengi, Mbowe au Bakhresa, utakuta vitu vinavyoonekana ni kashfa katika siasa, kumbe ni ujanja wa biashara. Katika siasa vitu hivi vinatumika kuvuruga mtazamo wa watu.

Angalia suala la (Freeman) Mbowe (la kukopa NSSF na hatimaye kuingia mgogoro nao hadi kufikishana mahakamani). Kibiashara ni kitu cha kawaida. Ndiyo ujanja wa biashara, lakini unapokuwa kiongozi hasa anayetafuta urais kama Mbowe, kisiasa inakuwa ni kashfa, alisema Rostam.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa ni muhimu kutenganisha biashara na siasa, kwani baadhi ya wafanyabiashara si waaminifu na matatizo haya ndiyo yamelifikisha pabaya taifa la Kenya.

Matatizo ya Kenya pamoja na ukabila hili la biashara limechangia sana. Wanasiasa wengi wao Kenya, wanatafuta madaraka kuneemesha biashara zao. Rais yuko sahihi. Hili lisiposhughulikiwa linaweza kuleta madhara Baadaye, alisema Rostam.

Alisema hashangai kwa nini yeye aandamwe kwani anajua yapo makundi matatu yanayomwandama muda wote. Aliyataja makundi hayo kuwa ni wafuasi wa vyama vya upinzani ambao yeye ni mwiba nambari moja kwao, kundi la walioumizana ndani ya CCM wakati wa mchakato wa urais na siasa za walikotoka mikoani na wengine ni kundi la wanasiasa wenye hulka ya wivu.

Rostam alikuwa akihojiwa na gazeti hili kutokana na tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake siku za karibuni.

No comments: