Sababu 5 kwa nini Tanzania
ina Rais Bora Afrika
Ndugu zangu,
Leo Machi 11, 2008 nataka niongelee nionavyo mimi juu ya Rais wetu, Jakaya Mrisho Kikwete! Hayo ni maoni yangu, yanaweza kutofautiana na ya mtu mwingine yeyote maana binadamu tuna mitazamo tofauti. Bahati mbaya sana hapa nyumbani ili mtu uonekane Mwandishi jasiri na shujaa lazima uwe na uwezo wa kuandika mabaya juu ya watu! Ikitokea ukampa mtu sifa, machoni pa wachache au wengi utaonekana mwoga msaliti au unayetaka kujipendekeza au kumsafisha mtu, tabia hii ndio inawafanya watu wengi kushindwa kutoa sifa hata pale wanapotakiwa kufanya hivyo kwa kuogopa kupewa sifa zilizoko hapo juu!
Sijui nitaitajwe baada ya makala haya, hilo si muhimu sana kwangu, muhimu ni kufungua mdomo na kusema kilichomo ndani. Leo nataka niseme kwamba, sisi Watanzania itatuchukua miaka mingi kufahamu ukweli kwamba hivi sasa tuna Rais bora pengine kuliko mwingine yeyote katika bara letu la Afrika na sababu ya kusema maneno haya ingawa Nabii
hana sifa kwao ni hizi zifuatazo:
1. Ni Rais anayeweza kuwasaliti rafiki zake sababu ya watu wake masikini; Nina uhakika kila mmoja wetu anafahamu urafiki uliokuwepo kati ya Rais wetu Kikwete na aliyekuwa Waziri Mkuu wetu wa tisa Mhe. Edward Lowassa! Lakini kwa yaliyojitokeza hivi karibuni nchini mwetu kuhusiana na suala la fedha za wananchi kwenye mkataba wa Kampuni hewa ya Umeme ya Richmond, alimruhusu ajiuzulu na kubeba aibu yote ambayo bila shaka itamwandama mpaka kaburini! Hivi kuna mtu anayefikiri Rais hakuwa na uwezo wa kumezea na hata kwa kutumia ushawishi wake, kuifanya kamati iamue kama alivyotaka? tukapiga kelele hadi kunyamaza na tusifanikiwe? Kwani huko nyuma ilitokeaje? Kwani Kamati ya aina ya Mwakyembe ilikuwa ya kwanza? Wakati wa utawala wa Mkapa hapakuwa na kamati wala tume ya kuchunguza kashfa mbalimbali nchini? Nini kilifanyika? Mimi nawaelezeni ndugu zangu Watanzania, itatuchukua miaka mingi kufahamu kuwa tunaye Rais bora pengine kuliko wote waliotangulia.
2. Ni Rais anayeweza kuwakamua matajiri akawalisha masikiniJambo hili linathibitika kwa namna alivyoshughulikia suala la Benki Kuu na fedha za EPA! Hili pia alikuwa na uwezo wa kulinyamazia kuwalinda matajiri na rafiki zake ambao ni Mafisadi, Rais wetu hakufanya hivyo! Badala yake hivi sasa anahakikisha fedha hizo zipatazo bilioni 133 zinarejeshwa serikalini ili zihudumie watu masikini wa nchi hii katika huduma za Afya, Elimu, miundo Mbinu nk. Anawakamua kwa waliojitajirisha na kuwarudishia masikini wa nchi hii kilicho chao, je, huyu si Rais bora Afrika? Binadamu hatujatimia, hakuna aliyekamilika lakini wakati mwingine imetupasa kuyaondoa makengeza na kuuona ukweli, TUMPENI RAIS WETU NAFASI YA KUTULETEA MAENDELEO badala ya kuanza kumchafua na kumvuja moyo.
3. Anapendwa na asilimia kubwa ya watu; Ndugu zangu, Tukubali ama tukatae, chini ya jua kuna watu wenye mvuto wa kuzaliwa nao, wenzetu Wazungu huwaita watu hawa Charismatic people, ambao kwao hata kama tutawapaka matope usiku na mchana watang’ara tu! Miongoni mwa watu wenye Charisma ni Rais wetu pamoja na mtu aitwaye Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini. Rais wetu anapendwa, tangu tupate uhuru wa nchi yetu, hapajawahi kuwepo ziara ya Rais wa Taifa la Marekani kama iliyofanyika hivi karibuni hapa nchini kwetu, jambo hili ni ushahidi tosha kuwa Rais wetu anakubalika na dunia nzima! Hebu angalia yaliyotokea nchini Kenya hivi karibuni ambako Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan alishataka kukusanya mabegi yake aondoke baada ya mgogoro kuonekana kuwa mgumu kwake, lakini alipoingia Rais wetu suluhu kati ya Mwai Kibaki na Raila Odinga ikapatikana, wote wakatia saini! Wakenya wanatushangaa sana tunapombeza Rais wetu Kikwete.
4. Anakerwa na umasikini wa watu wake; Ndugu zangu, Hapa duniani kila mtu anapoishi anajitengenezea jina fulani kutokana na tabia yake. Rais wetu anaweza kusemwa kwa ubaya wowote lakini kuna sifa moja ambayo mtu hawezi kumnyima nayo ni; Moyo wa Huruma, Upole na ukarimu! Ni mtu anayejali sana maisha ya watu waliomzunguka! Katika hili anafanana kabisa na Hayati Baba wa Taifa letu, Mwalimu J.K Nyerere. Mara nyingi utamwona akikiuka taratibu za usalama wake na kumsogelea mtu masikini kumpa msaada, hii ni huruma na ushahidi kwamba Rais wetu anakerwa na umasikini wa watu wake.
Ndio maana muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani, alichokifanya ni kupeleka shilingi Bilioni moja kila mkoa, ili kuwawezesha watu wake kutoka kwenye umasikini! Ingawa bado kuna mapungufu katika mpango wenyewe, nia ya kusaidia Rais wetu anayo na bila shaka kuna watu wamefaidika na mpango huo! Kama utaboreshwa utasaidia Watanzania wengi. Kwa hili la kuwajali watu wake, nawaelezeni ukweli tuna Rais bora Afrika, tumuungeni mkono.
5. Hana tamaa ya utajiri; Mpaka hapa tulipo leo naweza kusema kwa kujiamini maneno yaliyoko hapo juu na ninawaelezeni wazi kama Rais wetu ‘angekuwemo’ kwenye ‘dili’ la Richmond lazima angejisikia kushtakiwa kwa hatua alizowachukulia hata rafiki zake. Hii inanionyesha ni kiasi gani Rais wetu mpaka hapo alipo ni msafi na anakerwa sana na uchafu, akibadilika baadaye tutasema!
Kauli yake ya kuwataka wanasiasa kujitenga na biashara ni uthibitisho wa jambo hili, bila shaka Rais wetu ni mfuasi sana wa Baba wa Taifa, Rais wetu ni kijana wa Nyerere! Hataki kufanya biashara akiwa Ikulu mambo ambayo viongozi waliomtangulia waliyafanya na kujitajirisha, maana kuongoza ni kuonyesha mfano, yeye mwenyewe angetaka kufanya biashara asingekemea jambo hilo!
Ndugu zangu, sitaki kusema mengi sana, ninachofahamu ni kwamba mpaka leo Machi 11, Watanzania tuna Rais bora katika Afrika na huyu ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete, tumuungeni mkono katika juhudi zake za kutuletea maendeleo.
Ahsanteni kwa kunisoma.
Kutoka Global Publishers Tanzania.
No comments:
Post a Comment