Sunday, March 09, 2008

Wanawake nanyi

mnapaswa kuandika

wosia


Nasra Abdallah

JANA ilikuwa Siku ya Wanawake Duniani, ambapo Tanzania iliungana na nchi nyingine kuadhimisha siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8. Lengo la kufanya maadhimisho haya ni kujenga na kuendeleza mshikamano wa wanawake wote duniani.

Siku hii maalumu pia hutoa fursa kwa taifa, mikoa, wilaya, taasisi za dini, vyama vya siasa na mashirika ya hiari ya jamii na wanawake kupima mafanikio yaliyofikiwa kimaendeleo na kutafakari zaidi matatizo na changamoto zilizopo katika kufikia azima ya ukombozi na maendeleo ya wanawake.

Tangu mwaka 1996 Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku hii katika ngazi ya mikoa kwa kaulimbiu mahususi kulingana na vipaumbele vya maendeleo vya wakati ule ambapo hata mwaka huu kila mkoa umeendelea kufanya maadhimisho haya kwa kushirikiana na halmashauri, vyama vya serikali, mashirika ya kijamii na taasisi mbalimbali.

Kaulimbiu ya maadhimisho mwaka huu ilikuwa ‘Mgawo wa Rasilimali, Fedha kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake ni Msingi wa Maendeleo.’ Hivyo basi, wananchi wanatakiwa kikamilifu kwenye maeneo yao kuifanya ajenda hii kuwa ya kudumu kivitendo na kuifanya kuwa endelevu nchini ili kuongeza ufanisi na tija kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Tanzania Daima wiki hii ilibahatika kufanya mahojiano na Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA),Victoria Mandari, ili kuweza kuzungumzia siku hii ambayo ni muhimu hasa kwa maendeleo ya wanawake.

Mandari katika maelezo yake anasema tangu kuanza kwa wiki ya wanawake, wamekuwa wakiendesha kampeni ya umuhimu wa kuandika wosia ambayo inatatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, Machi 15 mwaka huu katika viwanja vya ofisi zao zilizopo Ilala Sharif Shamba, ambapo kauli mbiu ya kampeni hiyo ni ‘Epusha Migogoro ya Mirathi Andika Wosia’. Pia sherehe hizo zitakwenda sambamba na uzinduzi wa kitabu kinachoitwa ‘Vilio vya Wajane na Watoto Yatima’.

Anasema wameamua kuendesha kampeni hii kutokana na ukweli kwamba mpaka sasa bado kuna baadhi ya watu wanaogopa kuandika wosia kwa madai kwamba ni kujiwekea uchuro wa kufa mapema, jambo linalosababisha hapo baadaye mama au watoto kushindwa kumiliki mali za baba yao au watoto kutomiliki mali za wazazi wao wote inapotokea wamefariki dunia.

“Tumekuwa tukishuhudia wanawake wajane na watoto wao wakinyanyasika na kufukuzwa katika nyumba, hasa baba anapotangulia kufariki au kama mama amefariki baadhi ya kina baba hukuta wakitumia mali vibaya kwa kuoa mwanamke mwingine ambaye naye huwanyanyasa watoto na kufika hata hatua ya kuwafukuza nyumbani huku baba akiwa kimya, hivyo kampeni hii itasaidia sana kupunguza matatizo hayo,” anasema Mandari.

Mbali na hilo, pia anasema bado jamii haijajua kama mama naye ana haki ya kuandika wosia hata kabla ya mumewe kufariki, kwani sasa hivi wanawake wengi ndani ya nyumba nao humiliki mali tofauti na kipindi cha hapo nyuma ambapo mmilikaji wa mali alikuwa akitambulika kuwa ni baba tu.

Hata hivyo, anasema sheria ya serikali sasa hivi inagundua usawa uliopo kati ya mwanamke na mwanamume katika uandikaji wa wosia, hivyo kina mama wasijiweke nyuma katika uandikaji wa wosia kwa kuhofia kwamba huenda mahakama isiikubali na pia itawaondolea usumbufu watoto wake kuja kunyanyaswa na mama wa kambo au baba yao mwenyewe au hata wakati mwingine ndugu za mama wanaozaliwa pamoja.

Anasema katika kampeni hii ambayo itadumu kwa kipindi cha miezi mitatu, watakuwa wakitoa ushauri na kufundisha taratibu za jinsi ya kuandika wosia na haitakuwa na malipo.

Wosia ni nini?

Mandari anasema wosia ni kitu muhumi sana katika jamii kwani unaondoa migogoro ya familia na kuwapunguzia matatizo wale wanaobaki baada ya mtoa wosia kufariki hasa kwa wale ambao ni warithi.

Wosia ni tamko ambalo linaweza kuwa kwa mdomo au maandishi, linalofanywa na mtu yeyote likionyesha jinsi anavyotaka mali yake igawanywe au isimamiwe baada ya kifo chake na jinsi mazishi yake yatakavyokuwa. Ni muhimu kwa kila mtu mwenye miaka 18 na zaidi kujua jinsi ya kuandika wosia.

Aina za wosia

Kuna aina kuu tatu za wosia, nazo ni wosia katika sheria za kimila ambazo nazo zimegawanyika katika makundi mawili, ambao ni wosia wa maneno na wosia wa maandishi. Katika wosia wa maneno, wosia huu unapaswa kushuhudiwa na mashahidi wasiopungua wanne na wawili kati yao lazima wawe ni wanaukoo wa huyo mwosia. Wosia wa aina hii unaweza kufutwa kwa wosia mwingine wa mdomo au wosia wa maandishi.

Wosia wa maandishi

Sifa ya wosia huu ni kwamba unatakiwa uandikwe kwa kalamu isiyofutika au upigwe chapa na ni muhimu wosia wa aina hii uwe na tarehe. Mbali na hilo, pia sifa yake nyingine ni lazima ushuhudiwe na watu wawili wanaojua kusoma na kuandika na mashahidi wote kwa pamoja lazima wawepo kwa wakati mmoja mwosia anapotia saini katika wosia wake na wote lazima watie saini zao katika wosia huo.

Aina ya pili ya wosia ni wosia katika sheria ya kiserikali. Wosia huu hauna tofauti na wosia katika sheria za kimila, ule wa aina ya maandishi, kwani katika wosia huu vipengele vyote vya wosia wa maandishi vinatumika.

Lakini katika wosia huu, mwosia anaweza kufuta au kuongeza maneno mengine kwa kuandika maandishi mengine ambayo yatasomwa pamoja na yale ya awali. Maandishi haya lazima yazingatie uandikaji wa wosia na ni lazima yawe na tarehe.

Wosia mwingine ni wosia katika sheria ya Kiislam. Kwa taratibu za sheria ya Kiislam, mwosia anaruhusiwa kuusia 1/3 tu ya mali zake zote na sehemu inayobaki, yaani 2/3 ni lazima ibaki na zitagawiwa kwa mujibu na taratibu za sheria ya Kiislam.

Mambo ya kuzingatia katika wosia

Mandari anasema mtu anayeandika wosia anatakiwa awarithishe warithi halali wa mali zake na mtu mwingine yeyote anayetaka mwenyewe kumrithisha mali zake, lakini anatakiwa asirithishe rafiki sehemu kubwa kuliko ile ya warithi halali kisheria.

Aidha, anasema kuna baadhi ya sababu ambazo mrithi huweza kumnyima mrithi halali urithi. Katika hali ya kawaida mwosia anatakiwa amrithishe kila mrithi halali wa mali zake isipokuwa tu kama mrithi amezini na mke wa mwosia, mrithi amejaribu kumuua, kumshambulia au kumdhuru vibaya mwosia au kumtendea mama wa mwosia mambo mabaya yaliyotajwa hapo juu. Pi sababu nyingine ni bila sababu ya kuridhisha, mrithi kutomtunza mwosia wakati wa shida ya maradhi au njaa.

Endapo mwosia ataandika wosia bila ya kuwemo wakili au hakimu na mashahidi waliotajwa hapo awali, basi wosia huo utakuwa batili.

Wosia uwekwe wapi?

Wosia ni siri, ikiwa na maana kuwa kilichoandikwa hakitakiwi kujulikana na kila mtu, hivyo lazima uhifadhiwe sehemu ambayo hauwezi kusomwa na mtu yeyote kabla ya kifo cha mtoa wosia. Sehemu ambazo wosia unaweza kuhifadhiwa ni benki au mahakamani na sehemu nyingine yoyote ambapo mwosia anaamini panaweza kuwa na usiri unaotakiwa.

Inashauriwa hivyo, kwani waliorithishwa mali na mwosia wanaweza kutafuta mbinu za kumuua ili wapate kurithi au ikaleta ugomvi kati ya warithi na mtoa wosia.


Kutoka gazeti la Tanzania Daima.

No comments: