Thursday, April 24, 2008



Wanafunzi 39 waliofanya

Vurugu Chuo Kikuu

Dar watimuliwa



* Wafutiwa udahili na serikali, pia marufuku kujiunga na
chuo chochote

* Majina yao kuangazwa Alhamisi, pia watashtakiwa mahakamani

Na Waandishi Wetu, Dodoma na Dar es Salaam.


SERIKALI imetangaza kuwafutia udahili na kuwafukuza masomo wanafunzi waliofanya vurugu katika huo Kikuu cha Dar es Salaam.

Taarifa ya serikali iliyosomwa bungeni jana jioni mjini hapa na Waziri wa Elimu na na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, ilieleza kwa kifupi kuwa wanafunzi hao wapatao 39 wa chuo hicho wamefutiwa udahili na hawataruhusiwa kujiunga na chuo chochote nchini.

“Waliofanya vujo leo (jana) wamefutiwa udahili na kufukuzwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hawataruhusiwa kujiunga na chuo chochote,” alisema Profesa Maghembe katika taarifa hiyo bungeni saa 11.30.

Profesa Maghembe alisisitiza msimamo wa serikali kuwa haitawavumilia watu wanaofanya uhalifu na vurugu badala ya kusoma.

Adhabu hiyo imewakumba wanafunzi 39 waliodaiwa kuwa vinara mgomo ulianza Jamatatu wiki hii ili kuushinikiza uongozi wa chuo hicho kuwarudisha chuoni wenzao 15 waliofukuzwa awali kwa tuhuma kama hizo.

Mgomo huo ulifuatwa na vurugu zilizozuka juzi chuoni na kusababisha uongozi wa chuo kutoa taarifa polisi ambao waliwadhibiti wanafunzi hao na kuwakamata baadhi yao huku wengine wakiumizwa vibaya kwenye mapambano hayo.

Katika hatua nyingine, wanafunzi 38 wa chuo hicho ambao waliongoza vurugu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na shitaka ya kula njama na kusababisha fujo.

Akisoma hati ya mashitaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Said Msuya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Kenyela aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Mohamed Rashid (24), Blessas Lyimo (21), Mtaha Frank (24), Natanael Innocent (22), Kisendi Rashid (24), Rahel Chasaba (22), Ester Sanga (21), Lutandilo Hosea (22) na Mgaya Risper (24).

Wengine ni Rose Casmir (21), Lugome Claus (25), Mbaraka Charles (23), Abdallah Seleman (23), Charles Peter (25), Kizito Prim (23), Deodatus Ngoti (28), Juma Athuman (25), Juma Athuman (25), Gabriel Gibson (23), Chogelo Gregory (22), Mwankunga Edgar (25), Munish Hilary (22), Patrick Yesaya (22) Alex Manonga (22) na Maliwa Nyasilu (22).

Pamoja na Abrahamani Ephraimu (23), Bugumia Matiko (22), Mtandika Miraji (27), Maige Emanuel (24), Masudi Salehe (20), Mdeme Ramadhan (23), Jalud Said (23), Lutaiwa Frenk (22), Mwasyeba Anosisye (24), Shahamila Royald (23), Ahamad Masasi (22), Fimbo Yoseph (25), Halima Mfaume (23) Stella Kambanga (24), wote ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya mlimani.

Kenyela alidai kuwa Aprili 22, mwaka huu katika muda usiofahamika huko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mlmani kilichopo wilayani Kinondoni washitakiwa hao kwa pamoja walikula njama na kusababisha fujo kwa wanafunzi na Wahadhiri na kusababisha kuvunjika kwa amani.

Alidai kuwa siku hiyo ya tukio saa 4:50 usiku katika chuo hicho waliwafanya fujo ya kuwazuia wanafunzi na Wahadhiri kuingia madarasani na kuwapiga kitendo ambaho kilielekea kusababisha uvunjifu wa amani.

Katika kesi nyingine wanafunzi 13 kati ya hao 38 walifikishwa katika mahakama hiyo wakabiliwa na shitaka lingine la kushambulia na kusabisha maumivu ya mwili.

Ilidaiwa mbele ya Hakimu Mkazi, Hassan Makube, kuwa siku hiyo ya tukio wanafunzi hao walikula njama ya kuwashambulia wanafunzi ambao walikataa kushiriki katika unjifu wa amani.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, saa 2:30 usiku katika chuo hicho Kikuu cha Dar es Salaam wanafunzi hao walimshambulia kinyume cha sheria Rashid Ally kwa kutumia fimbo na mawe na kumsababishia maumivu makali mwilini.

Wakati huo huo wanafunzi wengine kumi kati ya hao 38 walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Euphimia Mingi wakikabiliwa na kula njama ya kuwashambulia maofisa wa Polisi wakati wakiwa kazini.

Inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio wanafunzi hao waliwashambulia ofisa wa polisi namba E. 8464 PC Petro wakati akiwa katika majukumu yake ya kazi kwa kumkata na chupa katika mguu wake wa kulia.

Washitakiwa hao walikana mashitaka na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Baadhi ya washitakiwa hao waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wanaominika.

Jana askari polisi wa Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia (FFU) wametembeza mkong'oto kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliodaiwa kuchochea fujo na kuwahimiza wenzao kugomea masomo chuoni hapo.

Wanafunzi hao walipata kipigo hicho jana mchana na kusababisha baadhi yao kuumia na wengine kukamatwa kwa kusababisha fujo chuoni.

Kuitwa kwa askari hao kulitokana na wanafunzi hao kuendesha mgomo siku mbili kwa madai ya kutaka wenzao waliosimamishwa masomo warejee chuoni bila masharti.

Juhudi za uongozi wa chuo kuwataka wanafunzi hao warejee madarasani zalishindikana hiyo kuulazimu utawala kutoa taarifa Jeshi la Polisi kuomba msaada ndipo FFU walifika na kutembeza mkong'oto wa nguvu.

Kabla ya kipigo hicho kuanza, wanafunzi hao waliogoma walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali kushinikiza wenzao waachiwe ikiwa ni pamoja na wimbo wa taifa na kutoa hotuba za kuhamasisha

“Hatuwezi kuendelea na mosomo wakati wenzetu wako nje, huu utakuwa usaliti. Tukubaliane pamoja na tuungane kuwarudisha wenzetu vinginevyo hakieleweki hapa,” walisikika baadhi ya wanafunzi wakisema.

Wamnafunz hao walianza mgomo Jumatatu ili kuushinikiza uongozi wa chuo kuwarejesha chuoni wanafunzi wenzao 15 waliofukuzwa kutokana na vurugu zilizotokea mwezi uliopita na kusababisha kifo cha msichana mmoja na baadhi ya mali za chuo



No comments: