Sunday, April 20, 2008

Anti Dina, gazeti la Maisha

Mume wa mtu

'ananitesa'



Anti,

POLE na kazi, mimi ni msichana wa miaka 24 tatizo langu ni kwamba nimetokea kumpenda sana mume wa mtu, anti nisaidie mdogo wako kwani nimependa zaidi ya kupenda, ila yeye hana habari na mimi. Kibaya zaidi nafanya naye kazi sehemu moja kila ninapomwona anazidi kunichanganya. Nilishamweleza hali halisi anasema yeye anamwogopa Mungu.

Anti, sifurahii kabisa maisha yangu kwani muda wote nimekuwa mnyonge mawazo yameniteka nimepata maradhi ya vidonda vya tumbo sababu ya mawazo, kama ujuavyo maumivu ya moyo hayasemeki hata chakula hakipandi, kama kungekuwa na dawa ya kuzuia kupenda ningeitumia, kwani mapenzi yananitesa.

Anti nisaidie mdogo wako, nakonda kila kukicha, hata nikijitahidi kula chakula vizuri lakini hakifanyi kazi nataka kwenda shule lakini nikifikiria kumwacha roho inaniuma sana kuwa mbali na uso wake.

Anti nisaidie kwani mapenzi yananiweka pabaya sikio la kufa halisikii dawa, nahitaji msaada wako wa hali na mali kwani siyatamani tena maisha haya ya mateso nimekata tamaa.

Q. J

Pole sana mdogo wangu, najua mapenzi yanavyouma, lakini elewa utamau au raha ya mapenzi ni kumpenda mtu anayekupenda. Kuna usemi unaosema ' mpende akupendaye, asiyekupenda achana naye'.

Pamoja na wewe kumpenda huyo mume wa mtu kupindukia lakini kwa maelezo yako ni kwamba yeye hana mapenzi nawe, lakini si hivyo tu kikubwa anamwogopa Mungu kwa kutembe nje ya ndoa yake kama kweli hilo liko katika moyo wake.

Unachotakiwa kujua ni kwamba pamoja na yeye kutoonyesha mapenzi kwako, lakini kuna kiuizi kingine, yeye ni mume wa mtu hata kama ataamua kukubali ufanye naye mapenzi atakutumia tu, lakini mapenzi yake yako kwa mke wake nawe utakuwa unajipotezea muda wako.

Umri wako bado ni mdogo sana na tena kama una mipango ya kusoma ni bora uende shule, wanaume wapo wengi tena wazuri, utampata wako wa maisha, huyo unayempenda si wako sana sana utajiingiza kwenye matatizo kwani hawakukosea waliosema 'mume au mke wa mtu ni sumu'. Jaribu kumsahau huyo mume wa mtu, tulia utampata wako wa maana.

No comments: