Kutamba ni kutambikia?
Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
Mpenzi Frank,
MAMBO vipi? Waendeleaje na biashara zako? Bila shaka mvua zakuvuruga kweli. Laiti ningeweza kuja kukusaidia maana najua wewe mwanamume mvivu kweli kwa kuinama na kupiga deki. Lakini upande mwingine, bora ujifunze maana tukioana napiga deki risepsheni si duka lako.
Hapa mikiki kama kazi. Bosi akarudi kutoka Butiama akiwa kama amepagawa. Anaweza kukaa kwa muda huku akiwaza, ghafla anashtuka na kusema kwa sauti
Jamani Muafaka
Muafaka maafa
Muafaka na mafisadi
Tuwapigie kura mafisadi nani tuwe na Muafaka nao.
Kisha anainama na kutingishika kana kwamba anapigwa fimbo na baba wa taifa. Kwa kweli, kama mtu ni mshirikina ni vigumu kuamini kwamba hawatakuwa wameathiriwa na mizimu ya baba yetu Butiama. Yeye alitupenda sisi walalahoi, wao wametuponda na kutufanya walalahoi zaidi, kisha wanajipeleka kaburini kwake kana kwamba wanaweza kujenga muafaka na yeye wakati malengo ni tofauti kabisa. Huu si kama ushirikina wa namna fulani, tena wa kuomba laana kabisa?
Hata hivyo, sishangai kwamba hawa waheshimiwa na watukufuru wanafanana na wanakijiji wenzetu maana hata waheshimiwa wabunge na manabii maarufu wanaamini misukule hadi wanadanganywa hivihivi laivu. Nashangaa jinsi anavyothubutu kuendelea kuhubiri baada ya kuumbuka kiasi hicho. Na ni kuumbuka mpenzi. Wewe wajidai waongea na Mungu kwa simu ya mkononi kabisa kisha vitoto viwili vyakuchota akili na fedha namna hii.
Nilimsikia Bosi akimfananisha na yule mwingine ambaye aliapa mbele ya hadhara kwamba hatahubiri tena hadi mpinzani fulani aingie ikulu kama Rais. Haya, uchaguzi ukapita, mpinzani kaanguka, mhubiri afanye nini. Kala pini, kala pini hadi uzalendo ukamshinda akaendelea kama kawaida. Kwa kweli mimi nawashangaa sana wanaojidai kuongea na Mungu namna hii. Watajuaje ni yeye kweli? Si kwamba wanajisikilizia wenyewe tu lakini kwa sababu ya viburi vyao, wanafikiri nafsi yao ndiye Mwenyezi mwenyewe?
Na ushirikina na hawa wabwataji wetu wakuu sisemi. Kila siku inaonekana wanatafuta wachawi tu, wachawi tu, daima ni wachawi wengine, badala ya kujiangalia na kutambua makosa yao wao wenyewe.
Lakini niache hayo maana mimi najua nini kuhusu mambo hayo? Namkumbuka tu mwalimu wetu wa dini alivyokuwa anasisitiza kwamba dhambi kuu kiburi. Kiburi kinazalisha madhambi yote mengine.
Tena alikuwa anaimba ‘kiburi ni kaburi’, ‘kiburi ni kaburi’. Kisha akawa anasema kwamba kukumbatia utajiri, na matajiri ni dhambi kubwa sana. Lakini hebu angalia siku hizi. Matajiri ndio wenyewe kwa kila dini, na hata chama chenyewe. Ndiyo maana nimechoka kwenda kusali. Inanihusu mimi nini tena? Mambo yote ya kupata magari makubwa kwa kusali kama vile ni mashindano ya kampuni ya simu yananihusu mimi ambaye sina mbele wala nyuma? Waache wakae huko na kujidanganya wanaongea na Mungu na Mungu anawapenda wanavyotamba na utajiri wao uliojengwa juu ya misingi ya ufisadi. Ptuuu!!!
Vinginevyo mimi mzima na utashangaa kusikia mpenzi nimepanda ndege juzi. Yaani ilikuwa kichekesho. Nafurahi kwamba mama Bosi anaona nafanya kazi vizuri kiasi kwamba anaona hawezi kushiriki shughuli bila mimi kuwapo ndiyo maana kanipeleka Mwanza kupika kwenye shughuli ya mdogo wake. Ningefurahi zaidi kama angeona kwamba nastahili kulipwa kwa kazi zote za ziada. Yeye anaona amenipa fahari kubwa sana kupanda ndege, na hiyo fahari inatosha lakini nimeenda huko na kukesha siku mbili kuandaa mambo zake, kwa nini nisilipwe. Yaani kupanda ndege imekuwa nongwa.
Lakini nilifurahi kupanda ndege. Kwanza niliogopa. Mimi nilidhani wakati ndege inaruka inajiviringisha kabisa ndiyo maana lazima tufunge mikanda. Basi nilikuwa nashika kiti utadhani tajiri na pesa zake. Kumbe inapaa tu, inapaa tu, na hakuna chochote cha ziada. Watu tu ndiyo hatari. Upande wa pili wa mama Bosi kakaa msichana. Licha ya kuambiwa na rubani kwamba watu wote wazime simu zao, yeye akawasha ya kwake muda mrefu kabla hatujatua. Mama Bosi kakasirika.
‘Wewe unafanya nini hapo? Husikilizi matangazo kwamba ni hatari kuwasha simu?’
Msichana katabasamu tabasamu ya kifedhuli.
‘Oh, samahani mama nilidhani tumeshatua tayari.’
Mama bosi si unajua mpenzi, hamkopeshi mtu.
‘Pumbavu kabisa. Huwezi kuangalia nje. Na hata sasa hujazima hiki kimeo chako.’
Akaanza kuwaita wahudumu wa ndege hivyo msichana kafunga simu harakaharaka. Mama bosi kaendelea.
‘Yaani mawasiliano ya ndege yanaweza kuharibika kwa dakika mbili kutokana na ukaidi wako lakini sioni kama mahusiano yako na huyu unayempigia yataharibika kwa hizo dakika mbili. Huwezi kuvumilia?’
Msichana kanyamaza nyamaaa. Lakini ndege ilipogonga chini kidogo tu, si yeye tu bali karibu ndege nzima, na hata mama Bosi mwenyewe wote wakawasha simu zao kana kwamba hawana akili nzuri. Hivyo watu waliishije kabla ya hizi simu?
Tena utawasikia wanaongelea mambo ya ajabu sana bila kujali nani anasikiliza.
‘Sasa Bwana we utanipa hela za matumizi au hunipi? Kwani unataka niishije?. Mpenzi feki origino.’
Yaani, kwa kuwa ana simu anataka watu wote wajue kwamba ametupwa. Haoni haya?’
‘Zile pesa zile kazipeleke kwa Tall. Yeye atajua azifanyie nini. Si unajua mkutano na waheshimiwa ni kesho. Takrima bwana.’ (huku anacheka)
Huyu ni fisadi nini? Tena fisadi origino maana yeye naye hajali nani anasikia.
Halafu wengine wanavyoweka sauti za milio yao, si afadhali disko vumbi za kwetu. Mimi na ujinga wangu nilijua kwamba simu ni kwa faida ya mwenye simu. Kwa nini sisi sote tushtushwe na mlio mkali wa simu wa kila dizaini kila dakika? Naona hiki ni kiburi cha aina nyingine tena.
Haya, basi tunatelemka kwenye ndege kila mtu ameshika simu utadhani hirizi. Tunaenda sasa kupata mizigo yetu. Yaani, hapo nilishangaa kabisa mpenzi. Mimi nilidhani mambo ya ndege ni mambo ya ustaarabu. Si ni chombo cha wenye nacho? Lakini pale Mwanza hakuna!!! Kwanza wasubiri mzigo wako. Kisha mizigo unatupwa chini kasehemu kadogo. Kwa sababu hakuna nafasi inabidi watu wakanyagane, wapigane kumbo ili wapate mizigo yao. Yaani kweli Mwanza, mji mkubwa kama ule hawawezi kutengeneza mpango mzuri zaidi? Sasa, mara mama mmoja kapoteza wigi, mara mwingine shati lilichanika kisha mheshimiwa mmoja Super Glue yake ya kushikiza simu sikioni ikakatika na simu kudondoka chini. Mwache ahangaike kuitafuta katikati ya makanyagano. Mbona Dar es Salaam mambo ya mizigo ilikuwa rahisi lakini huko Mwanza, sina hamu.
Suala la simu nilimwuliza mama Bosi maana naona wenye simu wanachafua hewa kabisa. Nilikosea maana nilisahau mama Bosi naye kaweka mlio wa kuonyesha kwamba yeye ni mke wa Waziri hivyo kaniangalia kama vile mimi ni kiroboto. Wala hakunijibu. Tena naona kama aliongeza sauti ya mlio zaidi.
Na nikimalizia mambo yangu ya uchawi, hata timu zetu za mpira zinachekesha sana. Jamaa achapwa mabao kibao huko kisha atangaza miujiza kama vile wapinzani watageuka misukule kutokana na matangazo ya gazetini. Anadhani kutamba ni kutambika. Ama kweli twadanganywa kirahisi sana.
Akupendaye mchawi wa moyo wangu bila kutumia hata dawa.
Hidaya
Kutoka Raia Mwema wiki hii
No comments:
Post a Comment