Kura ya maoni kwa
Muafaka? Dalili za
kufilisika kiuongozi
![]() |
KWA takribani mwezi mmoja nimekuwa na shughuli nyingi kiasi kwamba sifuatlii vya kutosha habari na matukio ya kitaifa. Hiyo ni kutokana na hatua tuliyofikia sasa ya kuandika taarifa ya Kamati ya Kupitia Sekta ya Madini ambayo mimi ni mjumbe. Hivyo, muda mwingi napata taarifa kutoka kwa marafiki, ndugu na wabunge wenzangu.
Nilipopata simu kutoka kwa rafiki yangu aliyekuwa Butiama akinijulisha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeamua suala la Muafaka liende kwa wananchi na kuliamulia kwa Kura ya Maoni nilishtuka sana.
Nikamwambia bila kufinyangafinyanga maneno kuwa uamuzi wa CCM ni dalili za kufilisika kiuongozi. Haikuniingia akilini hata kidogo kwa Halmashauri Kuu ya CCM kuchukua uamuzi wa aina hii. Kwamba CCM kama chama kikuu cha siasa nchini kinapaswa kuonyesha uongozi kwa vyama vingine vya siasa. Kwamba chama hiki kikubwa na kikongwe kwa kupitia uzoefu wake wa siasa wa miaka dahari kinapaswa kutoa mwongozo kwa vyama vingine na wananchi kwa ujumla kuhusiana na masuala makubwa ya nchi.
Uamuzi wa Butiama kuhusiana na Muafaka umeshindwa kuonyesha kuwa CCM inaweza kuongoza. Badala yake uamuzi umedhihirisha hisia kuwa chama hiki kinajifia, hakina uwezo wa kufikiri kimkakati, kinacheza na utulivu wa nchi na kimefilisika kiuongozi. Nitaeleza.
Kwanza, ninapenda kuweka fikra zangu wazi kwamba sikubaliani na wazo la Zanzibar kuwa na naibu marais wawili kama lilivyokubaliwa na timu za mazungumzo za vyama vya CCM na CUF. Sioni sababu yoyote ya kuwa na nafasi hizi. Nadhani haina mantiki kwa Visiwa vya Zanzibar kuwa na naibu marais wawili, ni kuongeza vyeo bila sababu za msingi.
Ningependelea Zanzibar iondokane kabisa na cheo cha Rais wa Zanzibar na badala yake kuwe na Waziri Mkuu mtendaji na Naibu wake na kwamba chama cha siasa kitakachopata wajumbe wengi wa Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi kitoe Waziri Mkuu na kile cha pili kitoe Naibu wake mwenye mamlaka katika masuala kama Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ.
Hata hivyo, makala hii inahusiana na uamuzi wa Butiama kuhusu Muafaka na wala si Muafaka una nini ndani yake. Muafaka una lenga kuleta utengamano wa kisiasa Zanzibar, kupunguza migogoro ya kisiasa na kuimarisha amani na utulivu. Unalenga kuwafanya wanasiasa wa Zanzibar kufanya kazi pamoja kwa faida ya wananchi wa Zanzibar. Muafaka ni zaidi ya makubaliano ya kisiasa ambamo wanasiasa wanagawana vyeo, ni makubaliano ya kijamii ambamo watu wa Zanzibar wanarejesha mahusiano yao mema na kuondoa ubaguzi miongoni mwao.
Muafaka ungewafanya Wazanzibari kuhukumiana si kwa kigezo cha uanachama wa mtu katika chama cha siasa au kisiwa anakotoka mtu, bali kwa kigezo cha tabia ya mtu. Mwafaka ilikuwa ni hatua moja ya kuelekea Zanzibar yenye utulivu na iliyoshamiri kiuchumi.
Uamuzi juu ya Muafaka ni uamuzi wa viongozi wa kisiasa kutoka vyama vya CCM na CUF. Ni wajibu wa viongozi hawa kuamua. Wajibu huu ulitolewa kwa viongozi wa vyama hivi na wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Wananchi waliwachagua wanasiasa ili waweze kuchukua maamuzi kwa niaba yao. Kitendo chochote cha kurejesha kwa wananchi uamuzi kuhusu Muafaka ni kukwepa majukumu na kushindwa kiuongozi kwani jaribio kuu la uongozi wowote ni kufanya maamuzi, tena maamuzi magumu.
Kitendo cha wananchi wa Zanzibar kupiga kura zilizoonyesha dhahiri tofauti za visiwa vya Pemba na Unguja na vile vile Mji Mkongwe na sehemu nyingine za Unguja, katika uchaguzi wa 1995, 2000 na 2005 ni ushahidi wa wazi kwamba wananchi wa Zanzibar wapo tayari kuongozwa na vyama hivi viwili vikubwa. Hapakuwa hata na ulazima wa mazungumzo ya Muafaka kuchukua zaidi ya miaka miwili kwani tayari wananchi walikwisha kuamua kupitia kura zao. Ilikuwa ni kiasi cha viongozi wa kisiasa kuona hisia hizi za wananchi na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Pius Msekwa ni msomi anayeheshimika na mwandishi wa vitabu kadhaa, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Taifa wa CCM ameamua kuandika makala kuelezea uhalali wa maamuzi waliyofanya Butiama kana kwamba kura za maoni ni jambo zuri kwa Muafaka. Makala hiyo nimeisoma katika gazeti la Serikali la Daily News la Jumatatu Aprili 7, 2008.
Katika makala hiyo, Msekwa, Spika wa zamani wa Bunge, anajenga hoja yake kwa kutumia kanuni ya ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi. Anauita Muafaka kuwa ni mabadiliko mazito ya Katiba ambayo yanahitaji kuamualiwa na watu. Amewanukuu wasomi wanaoheshimika kama Profesa Mgongo Fimbo katika kuelezea ni kwa nini kura ya maoni kuhusu Muafaka ni kitu kizuri kwa Zanzibar.
Kuna kitu mzee Msekwa amekosea sana. Yeye na jamii ifahamu ya kwamba kama kura ya maoni inahitajika haipaswi kuwa ni kwa Muafaka bali ni kwa mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar. Na ili mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yaamuliwe kwa kura ya maoni ni lazima Katiba yote ipitishwe kwanza kwa kura ya maoni na ndani ya Katiba hiyo kuwe na vifungu ambavyo mabadiliko yake yanahitaji kura ya maoni ama kwa Kiingereza:Sanctity Provisions.
Nchi nyingi za kidemokrasia zenye matumizi ya kura ya maoni, hutumia kura hiyo kwa maamuzi mazito sana ya Taifa ambayo huhitaji wananchi wote waamue. Sioni hata kidogo kama Muafaka una sifa ya kuamuliwa kwa kura ya maoni.
Hispania, kwa mfano, ilitunga katiba yake ya mwaka 1978 kwa kupitia kura ya maoni na kuweka vifungu ambavyo ili kuvibadili katika katiba ni lazima kuita tena kura ya maoni. Vifungu hivi ni kama vile vinavyohusu Tamko la Haki za Binadamu.
Uganda ni mfano mwingine ambako uamuzi kuhusu kuondoa au kutoondoa vikomo vya mtu kugombea urais hupelekwa kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni. Rasimu ya Katiba ya Bomas, nchini Kenya, Katiba ya Jamhuri ya Afrika Kusini na Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ziliamuliwa kwa kura ya maoni na zina vipengele ndani yake vinavyosema ni vifungu gani vya katiba kubadilishwa kwake kwahitaji kura ya maoni.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 haikupitishwa na Wazanzibar kwa kura ya maoni na wala haina vipengele vinavyotaka kura ya maoni ili kuvirekebisha.
Ni busara ya kawaida kabisa kwamba kabla ya kuupeleka Muafaka kati ya CCM na CUF kwa kura za maoni, Katiba ya Zanzibar inabidi kuandikwa upya, iwekewe vifungu vya kura ya maoni na kisha kuwapelekea Wazanzibari kuamua NDIYO au HAPANA kuhusiana na Katiba hiyo. Sasa kama vipengere vya makubaliano katika Muafaka vinagusia vifungu vya Katiba vinavyohitaji kura ya maoni, Muafaka waweza kupelekwa kwa wananchi. Kama sivyo, vyama vyaweza kusaini makubaliano yao na kisha kuyatekeleza kwa mujibu wa Katiba.
Hivyo, CCM imekosea kimantiki kupendekeza kura ya maoni kwa ajili ya Muafaka wake na CUF. CCM walipaswa kwanza kuukubali Muafaka wakaweka sahihi makubaliano hayo na baadaye kufanya mabadiliko yanayostahili katika Katiba ya Zanzibar. Hapa ingeweza kupitisha sheria inayotaka baadhi ya sehemu za katiba mabadiliko yake yapitishwe kwa wananchi kupitia kura ya maoni na hivyo kuipeleka katiba hiyo kupigiwa kura. Kimsingi Si Muafaka unaopaswa kupigiwa kura kama wanavyosema CCM bila kujua, bali ni ama Katiba ya Zanzibar au Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar.
Kama CCM ilishindwa kuona suala hili la wazi kabisa na la msingi basi haina haki ya kuwa chama tawala, na kwa kweli watakuwa hawana hata hadhi ya kuwa chama cha siasa maana haya ni masuala ya msingi ambayo kiongozi yeyote wa siasa anapaswa kuyajua..
Nchi nyingi za kidemokrasia duniani zinasita kuruhusu maamuzi kuchukuliwa kwa kura za maoni isipokuwa kwa maamuzi ya msingi kama masuala ya Haki za Binadamu, ukomo wa uongozi na suala kama kuwa na muungano kwa sababu wanaogopa kuwa wananchi hawana muda kutafakari kwa kina masuala mazito na magumu kulinganisha na mabunge. Na kwa kweli wananchi wanaajiri wanasiasa kila miaka mitano ili wawafanyie maamuzi.
Hivi toka lini CCM wameanza kupenda wazo hili la kura ya maoni? Si ni CCM hii hii ambayo miaka yote inapinga kura ya maoni kuhusu Muungano kuwapo au usiwepo? Si ni CCM hii hii ambayo imekuwa ikikataa katakata Mkutano wa Katiba nchini ili kuwapa nafasi Watanzania kuandika Katiba yao? Wamepata wapi sasa haya maono ya kuwa na kura ya maoni kuhusu Muafaka Zanzibar?
Kitu kimoja ambacho CCM na uongozi wake wote unashindwa kuelewa ni kwamba mwito wa kura ya maoni Zanzibar kuhusu Muafaka inaweka mfano mbaya sana unaweza kuchochea machafuko.
Kwa maono haya ya kura ya maoni kutoka Butiama, CCM wataweza kweli kumkatalia Mchungaji Christopher Mtikila atakapotaka Watanganyika waamue kwa kura ya maoni kama wanataka Muungano au hapana?
Hivi akitokea kichaa mmoja, mtu mwenye chuki na hasira kuwa utajiri wa madini ya nchi haunufaishi mikoa yenye utajiri huo na akiamua kutaka wananchi wa Kanda ya Ziwa wapige kura kuamua kama wawe nchi au wabaki ndani ya Tanzania, CCM itakubali? Itawezaje kukataa wakati wenyewe ndio wamekuwa makuadi wa kura ya maoni kuhusu Muafaka wa Zanzibar? Profesa Chachage angekuwa hai angewaita CCM makuadi wa demokrasia shirikishi!
Kura za maoni hupigwa kwa taratibu maalumu zilizowekwa na si kwa maamuzi yaliyojaa tamaa ya madaraka na yanayopanda mbegu za kugawa nchi kama yaliyochukuliwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Butiama. Maamuzi haya yana lengo moja tu la kuchelewesha Muafaka Zanzibar kwa gharama yoyote. Uamuzi wa CCM kuhusu Muafaka ni hatari kwa usalama, utulivu na umoja wa kitaifa na ni uamuzi ambao haupaswi kusherehekewa na Mtanzania yeyote mwenye kuipenda nchi.
Hivi CCM walifikiri kwa kina kweli madhara ya uamuzi wake kwa mustakabali wa Taifa hili? Mimi sitakuwa tayari kuona chama hiki kikubwa na kikongwe (The Grand Old Party – CCM) kikitishia uhai wa Taifa. Kwa kupitia makala hii nimesema yangu na nimeonya. Ninawaomba CCM waache uchochezi huu. Wasaini makubaliano na CUF na mara moja Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itayarishe miswada ya mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ili kukidhi haja ya Muafaka.
Mungu ibariki Tanzania,
Iepushe Tanzania na mabalaa!
Toka Raia Mwema wiki hii
No comments:
Post a Comment