Friday, April 11, 2008


Hatima ya `mchwa`

katika serikali leo


* Ripoti ya Mkaguzi Mkuu kuwasilishwa bungeni
* Kikwete aliahidi kuwasafisha watakaoboronga
* Mkaguzi, wenyeviti wa kamati kufafanua ripoti

na godfrey dilunga

HATIMA ya mafisadi au mchwa kama alivyowahi kuwaita Rais Jakaya Kikwete, waliomo Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Halmashauri, itajulikana leo bungeni, mjini Dodoma.

Hatima yao itajulikana wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, atakapowasilisha Ripoti ya Hesabu za Serikali kwa mwaka ulioishia Juni 30, mwaka jana.

Ripoti hiyo inahusisha ukaguzi wa fedha Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Halmashauri zote nchini.

Hatua hiyo itakuwa ni ya pili katika historia ya Bunge kwa ripoti ya CAG kujadiliwa. Mabadiliko hayo yalifanywa kwa ridhaa ya Rais Kikwete mwaka jana.

Rais alifikia uamuzi huo baada ya kubaini namna ripoti ya CAG iliyowasilishwa kwake mwaka jana, inavyobainisha ufisadi unaofanyika katika ofisi za umma. Katika ripoti hiyo, mabilioni ya fedha yalibainika kupotea kwa njia mbalimbali.

Wakati akiamua ripoti hiyo ijadiliwe na Bunge, Mawaziri na watendaji wakuu wa mashirika ya umma na halmashauri, Rais Kikwete aliahidi kwamba, yeyote atakayerejea makosa hayo ya ufisadi kama ripoti ya CAG ilivyobainisha, atakuwa amejifukuzisha kazi.

Hivyo basi, kwa kuzingatia msimamo huo wa Rais Kikwete mwaka jana, ni dhahiri kuwa ripoti ya sasa ya CAG itawang’oa ‘mchwa’ watakaobainika kufanya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisi ya CAG, inaeleza; “Ripoti ya Hesabu za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na zile za mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2006/2007, zitawasilishwa bungeni Aprili 11 (leo) mjini Dodoma.”

“Uwasilishaji huo utafuatwa na mkutano na waandishi wa habari baina ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Wenyeviti wa Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma,” inaeleza taarifa hiyo kutoka ofisi ya CAG.

Kutokana na utashi wa Rais Kikwete katika kupambana na ufisadi, hasa baada ya kuruhusu ripoti ya CAG kujadiliwa bungeni, Bunge liliwahi kupitisha Azimio la kumpongeza Rais.

Baada ya kukabidhiwa ripoti ya kwanza ya CAG akiwa madarakani, Aprili 15, mwaka jana, Rais Kikwete aliitisha kikao maalumu cha viongozi wakuu wa Serikali, kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa ili kujadili ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa Azimio lililopitishwa na Bunge kupongeza hatua hiyo ya Rais, ni mara ya kwanza katika historia ya nchi kwa Rais kuitisha kikao maalumu cha viongozi wote wa Serikali kujadili na kutoa maelekezo ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Azimio hilo la Bunge lilisomwa bungeni na Mbunge wa Ukerewe, Gertrude Mongela, Aprili 20, mwaka jana.




No comments: