Friday, April 11, 2008



Tarehe ya uhuru wa Zanzibar

yazua mtafaruku Bungeni



Na Ramadhan Semtawa, Dodoma

MKANDA unaotumika katika kompyuta, ambao umeandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, umeibua mkanganyiko katika Bunge la Muungano jana, baada ya kuonyesha kwamba Zanzibar ilipata uhuru wake mwaka 1963.

Akitafuta mwongozo wa Spika baada ya kipindi cha maswali na majibu jana asubuhi, Mbunge wa Dimani Hafidh Ali Tahir (CCM), alisema mkanda huo unaeleza muungano ulifanyika baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961 na Zanzibar mwaka 1963.

Tahir alifafanua kwamba, kutokana mkanda huo kupotosha historia, baadhi ya wabunge wa CUF bungeni wamekuwa wakiutafuta kwa udi na uvumba ili waonyeshe dunia kwamba kumbe historia ya visiwa hivyo inapotoshwa.

“Mheshimiwa Spika naomba mwongozo wako, hapa kuna Disk ambayo imesambazwa kwa wabunge na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini disk hii imepotosha historia ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,” alisema na kuongeza;

“ Sasa hivi mkanda huu unasakwa na wenzetu wa CUF, wanataka kuutumia kuonyesha dunia kwamba, historia ya Zanzibar inapotoshwa. Ninavyojua mimi, Zanzibar ilipata uhuru baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, mwaka 1964. "

Tahir, alisema Bunge ni chombo nyeti, hivyo kitendo cha wizara kuandaa mkanda kama huo bila kuuhakiki kwa makini kisha kuupeleka bungeni, ni makosa hivyo akaomba mwongozo wa Spika katika hilo .

Alisema ndani ya mkanda huo pamoja na mambo mazuri ya kueleza vivutio vya utalii, lakini kuna mwanamke mmoja anajitokeza na kuzungumzia historia hiyo ambayo inapotosha historia halisi.

Baada ya kuomba mwongozo, Tahir pia alitaka kanda hizo zikusanywe na zirudishwe wizarani zikafanyiwe marekebisho kuliko kuendelea kuzisambaza.

Kutokana na ombi la mbunge huyo, Spika alisimama na kukiri ofisi yake kusaidia mawasiliano na wizara ili kanda hizo zisambazwe kwa wabunge.

Sitta alifafanua kwamba, atamuita Waziri wa Maliasili na Utalii kwa ajili ya kupata maelezo ya kina.

Alisema suala hilo halitapaswa kufika wiki ijayo, hivyo litazungumzwa wiki hii.

“ Sisi tulisaidia mawasiliano na Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini nitakutana na waziri,” alisisitiza Spika.

Historia ya Visiwa vya Zanzibar ambayo kwa sehemu kubwa imetawaliwa na Sultan, imejaa utata kuhusu lini hasa uhuru wa kweli ulipatikana.

Wachambuzi wanaamini historia hiyo ndiyo inayotesa visiwa hivyo hasa Pemba na Unguja, huku sehemu kubwa ya Wapemba wakiamini uhuru kamili ulipatikana mwaka 1963 chini ya Waziri Mkuu, Mohamed Shamte kutoka Zanzibar National Party (ZNP).

Hata hivyo, Waunguja wengi ambao wana asili ya Afrika, wanaamini mapinduzi ya Januari 12, 1964 ndiyo halali kwani yaliondoa utawala wa Shamte, ambaye wanadai alikuwa kibaraka wa Waarabu ambao walikuwa na ngome zaidi Pemba .

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya Wapemba wanaamini uhuru kamili ulipatikana mwaka 1963 hivyo kilichofanyika mwaka 1964 ni mapinduzi haramu dhidi ya utawala halali.

3 comments:

Anonymous said...

TAREHE YA UHURU WA ZANZIBAR

Historia ya uhuru wa Zanzibar isiwe ndio tatizo la kukaa watu bungeni kupoteza muda wa kulitatua, halita solve matatizo ambayo wananchi wa hususan Pemba kupatiwa maendeleo ambayo hayajaonekana tokea kupatika uhuru au kufanyika mapinduzi ya 1964. More than 40 years now. Ikiwa uhuru ulipatikana 1964, kwanini sioni sherehe zinafanzika kila mwaka kuadhimisha uhuru huo. Mapinduzi sio uhuru, angalieni kamusi za kiswahili. Someni historia ya Zanzibar vizuri, mukumbuke Lancaster House Summit and who attended it. Mzanzibari.

Anonymous said...

Kilichofanyika ni "Funika kombe mwanaharamu apite". Lakini ukweli unabakia pale pale UHURU 1963 na MAPINDUZI 1964.

Anonymous said...

Wazee huko bungeni msituchanganye! Lugha kwenu ishakuwa na kigugumizi? Hata mimi niliyozaliwa juzi najua kutofautisha baina ya Uhuru na Mapinduzi! Mshalikoroga mtakunywa na wa kwenu tu!