Wednesday, April 23, 2008




Kizaazaa chuo kikuu

Dar es Salaam



Gloria Tesha
Daily News; Wednesday, April 23, 2008 @00:02


MGOMO unaoambatana na fujo uliendelea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani jana, kwa kundi linaloongoza mgomo huo kuwafungia katika chumba cha maktaba wanafunzi wenzao waliokuwa wakijisomea na kuwachapa viboko baadhi ya waliokuwa madarasani, wakiwalazimisha waungane nao.

Wanafunzi wanaolazimisha mgomo wamesema wataendelea nao leo, wakidai kuwa ni njia pekee ya kuubana uongozi wa chuo hicho kuwarudisha chuoni wanafunzi wenzao 19, akiwamo Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi (Daruso), Julius Mtatiro, waliosimamishwa masomo kwa makosa mbalimbali.

Ghasia hizo zilianza asubuhi wakati kundi lililogoma lilipokuwa likipita katika madarasa na sehemu za kujisomea nje likiwafukuza na kuwatishia wenzao waliokuwa wakisoma kwa fimbo na waliogoma kuacha kusoma walitandikwa.

Baadhi ya wanafunzi walisema kwa nyakati tofauti chuoni hapo jana kuwa hali hiyo inatishia amani na usalama wao na kwamba wana wasiwasi kuhusu hatima ya mgomo huo, kwani upo uwezekano wa chuo kufungwa na hivyo kuathirika katika masomo.

“Hatukatai kuandamana kudai haki zetu hasa wenzetu, kwani tunachoona ni kwamba waliosimamishwa masomo hawakutendewa haki maana kama ni uchunguzi unapaswa kufanyika wakiwa chuoni, lakini vile vile fujo inayosababisha kuharibu vitu si sawa, ndiyo maana unaona wengine tumekaa pembeni,” alisema mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Fatma.

Hata hivyo, uongozi wa chuo ulitoa taarifa polisi kutokana na vurugu hizo na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow alionekana na kundi la askari zaidi ya watano pamoja na wale wa kutuliza ghasia wakiwa na gari lao wakiwa wametanda katika maeneo mbalimbali ya chuo hicho.

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda Rwambow alisema ameamua kwenda mwenyewe na vijana wake kuhakikisha usalama na amani katika chuo hicho na kuongeza kuwa kuanzia jana wameanza operesheni ya kuwakamata wanafunzi watakaofanya fujo.

“Chuo kipo katika eneo langu na ni kazi yetu sisi polisi kulinda amani na usalama wa raia, ndiyo maana niko hapa na leo tunaanza rasmi kuwakamata wote watakaozua fujo ndiyo maana kwa mchana huu unaona hakuna tena maandamano,” alisema Rwambow.

Kwa upande wake Rais wa Daruso ambaye jana hakupatikana kwa urahisi kutokana na vikao, alikaririwa akisema mgomo unaoendelea chuoni hapo umeitishwa na wanafunzi wenyewe na vikao kati yao na Utawala vinaendelea katika kukabiliana na tatizo hilo.

Taarifa za kikao cha uongozi wa chuo pamoja na Daruso zilizotolewa juzi jioni zilieleza kuwa mgomo unaoendelea unafanyika kinyume cha sheria za chuo na kwamba hawatakuwa tayari kumvumilia ye yote atakayebainika kusababisha uvunjifu wa amani, masomo na vifaa katika mazingira ya chuo hicho.

Wanafunzi 14 walisimamishwa masomo Februari mwaka huu baada ya kujihusisha na fujo katika eneo la hosteli ya Mabibo na sehemu ya Mlimani na watano wengine walidaiwa kukutwa na bangi Aprili mwaka huu. Idadi hiyo inamshirikisha Waziri Mkuu wa Daruso, Mtatiro.




No comments: