Wednesday, April 23, 2008

Mkapa, Yona washtakiwe




2008-04-23 09:05:17
Na Joseph Mwendapole, Dodoma

Hoja ya Rais mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Daniel Yona, kumiliki mgodi wa Kiwira, imetinga bungeni, kukiwa na shinikizo la kutaka wachukuliwe hatua za kisheria.

Mbunge wa (Vunjo CCM), Bw. Aloyce Kimaro ndiye aliyeibua sakata hilo bungeni, akisema Bw. Mkapa na Bw. Yona, walijimilikisha kwa bei `chee` mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ulioko mkoani Mbeya.

Alitaka viongozi hao wachukuliwe hatua za kisheria kwa kuwa wamekosa uadilifu na kukiuka taratibu za maadili ya uongozi wa umma.

Bw. Kimaro aliibua sakata hilo wakati akichangia Muswada wa Umeme wa Mwaka 2007 juzi jioni.

Alisema licha ya kuununua kwa bei chee ya Sh. milioni 70, wameanza kufua umeme ambao wanauuza kwa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na kulipwa Sh. milioni 146 kila siku kama malipo yanayotokana na uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme.

``Yona kaanzisha kampuni na Mkapa, inaitwa Tanpower Resource Tanzania Ltd, na ndiyo iliyonunua Kiwira kwa Sh. milioni 70 tu badala ya bei halisi ya Sh. milioni 700,`` alisema.

Alisema kutokana na viongozi hao wa zamani kumiliki mgodi huo na kuanza kuzalisha umeme na kuuzia Tanesco, wanalipwa Sh. milioni 146 kila siku kama malipo yanayotokana na uwezo wa mitambo kuzalisha umeme. Tozo hilo (capacity charge) hutolewa hata kama mitambo haizalishi umeme.

Alisema viongozi hao hawaonyeshi mfano mzuri kwa mawaziri wa sasa, wizara hiyo na viongozi wengine waliopo madarakani na akahoji kwa nini hawachukuliwi hatua za kisheria.

``Hawa vijana wataiga mfano gani,`` alihoji Bw. Kimaro.
Wizara ya Nishati na Madini inaongozwa na Waziri William Ngeleja na Naibu wake Bw. Adam Malima ambao ni vijana.

``Malima kule kwake ana gesi, sasa naye aunde kampuni? ``aliendelea kuhoji na kuongeza, ``ifike mahala tuseme sasa inatosha``.

Alisema Rais Jakaya Kikwete lazima aseme mwisho na hawa wanaolihujumu taifa lazima Watanzania waseme mwisho na wahusika wafikishwe mahakamani.

``Ifike mahala sasa tuseme inatosha, Rais Kikwete sasa lazima aseme mwisho, hawa wanaotuhujumu lazima sasa tuseme mwisho, ni lazima wafikishwe mahakamani,`` alisema.

Akifafanua kuhusu Kiwira, Bw. Kimaro alisema thamani ya mgodi huo uliojengwa na Wachina mwaka 2004, ilikuwa ni Shilingi bilioni nne.

Alisema wakiwa madarakani viongozi hao, walijiuzia mgodi huo bila utaratibu wowote kwa Sh. milioni 700 lakini walilipa Sh. milioni 70.

Alisema mwaka 2006, bila utaratibu unaoeleweka walianza kufua umeme huko Kiwira na kuuza kwa Shirika la TANESCO.

Alisema anatofautiana na sera ya kuweka umeme kufanywa kuwa huria kwa sababu tayari wapo watu ambao wamejiwekea mazingira mazuri tangu mapema.

Aidha Bw. Kimaro aliitaka serikali kufuta tozo za ?capacity charge? kwa kuwa halina maana yo yote na linamuumiza Mtanzania.

Alisema haungi mkono muswada huo wa sheria na badala yake aliahidi kupambana na wizara hiyo wakati itakapowasilisha bajeti yake katika Bunge la bajeti.

Meneja Uhusiano wa TANESCO Bw. Daniel Mshana, alipoulizwa aligeuka mbogo na kutaka maswali yanayohusu shirika hilo kulipa mamilioni haya yaelekezwe kwa Bw. Yona.

``Mambo yanayozungumzwa kwenye Bunge mimi siwezi kuyazungumzia hata siku moja. Anayezungumza ni Waziri au Katibu Mkuu, usiniulize umesikia,`` alifoka.

Jitihada za kumtafuta Bw. Yona hazikuzaa matunda licha ya kumtafuta kwa simu ya mkononi na ile ya ofisini kwake Mtaa wa Sokoine kwani zote hazikuwa na majibu.

  • SOURCE: Nipashe



No comments: