Sunday, April 13, 2008

Mahojiano: Prof. Haroub Othman:

Sioni dhamira ya mwafaka wa kweli


*Asema hayati Karume angekuwepo, angesikitika
*Asauri wasomi, wanajamii waishinikize Serikali


PROFESA Haroub Othamn wa Idara ya Taaluma za Mandeleo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni mmoja wa wasomi wanaozifahamu kwa undani siasa na historia ya Zanzibar. Katika mahojiano haya aliyoyafanya wiki hii, Dar es Salaam na mwandishi HASSAN ABBAS, msomi huyo anaeleza mtazamo wake kuhusu kuvunjika kwa mazungumzo ya muafaka baina ya vyama vya CUF na CCM na mtazamo wake juu ya nini kifanyike.

Swali: Mwafaka wa kisiasa kati ya CCM na CUF umechukua hatua nyingine
baada ya tamko la CCM kutaka kura ya maoni. Nini maoni yako kwanza kwa kuanzia na msimamo huo mpya wa CCM?

Prof. Haroub: Rais Jakaya Kikwete alipoliarifu Bunge kwamba ana azma ya kilipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la mpasuko wa kisiasa Zanzibar, wananchi wengi wa Bara na Visiwani walifurahi. Ilipoundwa kamati ya pamoja ya CCM na CUF matumaini ya wengi yalikuwa kwamba sasa mambo yatanyooka.

Kwa wengi tuliokuwa tukifuatilia mazungumzo hayo kulikuwa na wasi wasi baadhi ya wakati kwamba labda yalikuwa hayapewi kipaumbele inachostahiki; lakini bado tulikuwa na imani kwamba Rais atatimiza ahadi yake. Sasa kusema kweli sidhani kwamba ipo dhamira na utashi wa kisiasa wa kulimaliza tatizo hili.

Tunaambiwa kwamba pande zote mbili katika mazungumzo yale zilikuwa
zinawaarifu wakubwa wao kila wakati juu ya nini kimetokea, nini
kimekubaliwa na wapi kuna matatizo. Kuna nyakati tumeona kwamba
Mheshimiwa Yusuf Makamba na Mheshimiwa Seif Shariff wakiitwa kwenye kamati kusaidia ipigwe hatua ya kusonga mbele.

Ikiwa hivyo ndivyo, sidhani kwamba viongozi wakuu wa CCM na wa CUF walikuwa hawajui nini kimekubaliwa. Nataka kuamini kwamba walikubaliana nayo. CUF waliyakubali hadharani. Ikiwa katika CCM viongozi wa juu walikuwa na mashaka nayo, haikuwa na haja kuyaharakisha kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa. Kwa maoni ya mtu wa kawaida, kusema kwamba viko vipengere vizungumzwe upya au kuleta dondoo jipya ni njia ya kistaarabu ya kusema huyakubali.

Swali: Unafikiri nini chanzo cha kuja wazo hilo linaloelezwa kuibuliwa
sana na wajumbe wa CCM-Unguja huku wale wa Pemba wakionekana kuwa watulivu? Je, kuna uhafidhina CCM Unguja kama inavyodaiwa?

Prof. Haroub: Sijui nini kilitokea kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa, lakini nijuavyo mimi CCM ni chama kimoja. Nini ilikuwa 'consensus' (makubaliano) ya wajumbe? Je, kulipigwa kura? Itakumbukwa mwaka 1995 wajumbe wa kamati maalumu ya Zanzibar walipopiga kura kwa wingi kumtaka Dkt. Mohamed Bilal agombee kiti cha Urais, wingu wao haukufua dafu juu ya wingi wa wajumbe wa NEC nzima.

Swali: Katika suala hilo hilo la kura ya maoni. Kwa mtazamo wako
unadhani ni wazo muafaka sasa kurejea kwa wananchi na kuwauliza katika suala hili, ukilinganisha na masuala mengine ya kitaifa yaliyowahi kuamuliwa huko nyuma bila maoni ya wananchi?

Prof. Haroub: Wananchi kuulizwa juu ya mambo mbali yanayowahusu na yanayohusu taifa ni wajibu. Lakini katika hili wananchi waulizwe nini?

Ilipobadilishwa katiba ya Tanzania na kumuondosha Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais na badala yake kuwepo na mgombea mwenza, wananchi waliulizwa? Kwa hakika badiliko lile liligusa msingi wa Makubaliano ya Muungano (Articles of Union), lakini hatua ilichukuliwa na Bunge!

Hakuna anayesema kwamba serikali ya mseto ni kitu cha kudumu lakini ni njia ambayo wengi wanaiona kuwa itapunguza chuki, uhasama na malumbano ambayo yanaizuia Zanzibar kupiga hatuwa za haraka za maendeleo.

Swali: Kwa upande wao CUF nao wametoa tamko kuwa hawako tayari kurejea katika mazungumzo, wakisisitiza kuwa CCM imefanya kile wanachokiita usanii wa kisiasa na wamekwenda mbali kiasi cha kuhoji umakini wa Rais Kikwete. Unauzungumziaje msimamo huu wa CUF nao?

Prof Haroub: Huo ni msimamo wa CUF na labda wanasababu kufikia uamuzi huo. Uongozi, kama alivyokuwa mara kwa mara anatukumbusha Mwalimu Nyerere, ni kuonyesha njia. Wakati mwengine kiongozi inabidi kuchukuwa maamuzi machungu; na hata kwenda kinyume na matakwa ya chama chake madhali jambo lenyewe lina faida kwa taifa zima.

Swali: Profesa umekuwa mstari wa mbele sana kutaka hali ya kisiasa
Zanzibar itengemae. Kwa namna suala hili lilipofika sasa ushauri wako ni upi hasa katika kuyaokoa mazungumzo ya muafaka wa kisiasa na kwa maslahi ya Zanzibar? Nini kifanyike kwa wanasiasa hasa wakuu Rais Kikwete na Karume?

Prof. Haroub: Wasiwasi wangu ni kwamba ikiwa suala la mpasuko wa kisiasa halikutafutiwa ufumbuzi wa kuduma sasa, hali ya kisiasa, kijamii na
kiuchumi itazidi kuzorota.

Swali: Kwa maoni yako kama Karume angekuwa hai leo, akiwa mwasisi wa
umoja kuanzia ule wa ASP, Muungano na hata kuzaliwa kwa CCM, angeweza kuwa na maoni gani kuhusu Zanzibar iliyopo sasa?

Prof. Haroub: Nadiriki kusema mengi yangemsikitisha. Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikusudia kuondosha dhulma, uonevu, uhasama, na yalilenga kuleta usawa na kuboresha maisha ya mwananchi wa kawaida. Mzee Karume alielezea dhamira hizo katika tamko alilolitowa pale uwanja wa Maisara siku ya tarehe 8 Machi 1964.

Swali: Katika hotuba yake ya April, Rais Kikwete anasema maamuzi ya Butiama yako sahihi na kwa NEC kuagiza kura ya maoni yalikuwa sahihi.
Hili unaweza kulizungumzia vipi?

Prof. Haroub: Tatizo hili si la CUF au CCM bali ni la Zanzibar nzima na
Tanzania kwa ujumla. Kwa sasa tunaliona ni baina ya CUF na CCM ni kwa sababu wao ndio wapo kwenye mstari wa mbele katika mgogoro huu.

(Kikwete) Kama mwenyekiti wa CCM ana haki ya kusema hivyo; lakini Mheshimiwa Jakaya Kikwete pia ni Rais wa Jamhuri.

Swali: Ushauri wako wa Wazanzibar wakati huu wa kutibuka kwa mazungumzo ya muafaka ni upi?

Prof. Haroub: Ni wakati jumuiya zisizo za kiserikali Tanzania nzima, wapenda demokrasia na amani kupaza sauti zao na kudai kwamba suluhisho la kudumu lipatikane.

Sisi wasomi katika maandishi na mihadhara yetu tumekuwa tukielezea athari Zanzibar, na Tanzania, imekuwa ikizipata kwa mpasuko huu kuendelea. Na hilo hatutowacha kulisemea.

Swali: Ungepata nafasi ya kukutana na Rais Amani Karume, Rais Kikwete na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad ungekuwa na lipi zito la kumwambia kila mmoja kwa manufaa ya Tanzania na Afrika kwa ujumla?

Prof. Haroub: Sidhani ningewaambia kitu chechote tofauti na kile nalichokuwa nikisema tangu mwaka 1995, hata kabla ya uchaguzi wa mwaka ule.

Marehemu Dkt Omar Ali Juma ni shahidi wangu, na leo angekuwa hai, angenambia: 'Huchoki!'


No comments: