Sunday, April 13, 2008


Mwenge wa Olimpiki kuzinduliwa leo


Na Sophia Ashery




MWENGE wa Olyimpiki unatarajia kuzinduliwa leo mchana na kukimbizwa katika Jiji la Dar es Salaam.

Mwenge huo utazinduliwa na kukimbizwa kuanzia Tazara hadi uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo kutafanyika sherehe mbalimbali.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja Masoko wa Kampuni ya Coca Cola kwa kanda ya Afrika Mashariki na Kati ambao ni mdhamini mkuu wa mwenge huo, Caroline Mbaga, alisema kila kitu kimekamilika kwa ajili ya kukimbiza mwenge huo.

Alisema tayari wakimbizaji wa ndani na nje ya nchi waliopata mafunzo ya jinsi ya kukimbiza mwenge huo, wapo tayari kwa shughuli hiyo.

"Tulifanya semina kwa wakimbizaji 80 wa mwenge huo, na leo wapo tayari kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo ya kihistoria," alisema Caroline.

Alisema ni fursa kwa watanzania na wakazi wa Dar es Salaam kushuhudia tukio hilo la kihistoria ambapo Dar es Salaam ni Jiji pekee barani Afrika kuwa mwenyeji wa mbio hizo.

"Tunajivunia kuwa wenyeji wa mbio hizo kwa kuwa ni fahari kwa nchi yetu kwani katika nchi zote za Afrika, Tanzania pekee ndiyo iliyobahatika kuwa mwenyeji wa mbio hizo," alisema Kimbisa.

Mbali ya hilo, Caroline alisema ulinzi mkali unatarajia kuwepo katika shughuli nzima ya ukimbizaji mwenge huo kutokana na kuwepo baadhi ya watu wa kupinga mwenge huo.

Alisema licha ya hivyo, wanatarajia kutokuwepo kwa vitendo vyovyote vya kupinga mwenge huo na kuendeleza sifa ya nchi ya kuwa na amani na utulivu.

No comments: