Monday, April 28, 2008

Mtoto mchawi

amla mtoto



na Alfred Lucas na Lucy Ngowi

JIJI la Dar es Salaam, jana lilizizima kwa hofu baada ya mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 12, kukamatwa akila kichwa cha mtoto wa kike mwenye umri kati ya miaka mitatu na minne.

Tukio hilo la kushitusha lilitokea jana asubuhi, majira ya saa 2.45 baada ya askari mgambo anayelinda lango kubwa la Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) kumsimamisha na kumuhoji mtoto huyo aliyetambuliwa kwa jina la Ramandani Mussa alipokatisha katika lango hilo.

Mtoto huyo, ni yule aliyeripotiwa kuanguka kwenye Kanisa la Mikocheni Assemblies of God, Dar es Salaam linaloendeshwa na Mchungaji, Dk. Gertrude Rwakatare kabla ya kuelezwa kwamba ni tukio lenye sura ya uongo.

Alipofika getini, alisimamishwa na askari mgambo, Fulgence Michael Simfukwe, baada ya kumtilia shaka wakati akipita katika lango hilo.

“Sababu za kuanza kumuhoji ni kwamba, nilidhani ni mtoto mtukutu ambaye pengine amempora mtu na kuamua kukatisha njia pale getini, lakini akanijibu kwamba amebeba zawadi na kwamba anampelekea shangazi yake anayefanya kazi IPPM.

“Nikamuuliza kwanini asimsubiri nyumbani, yeye akang’ang’ania kutaka kupita, nikawa na wasiwasi. Baadaye nikamwambia afungue mfuko tuone hiyo zawadi.

“Alikataa, na alipokubali nikaona ametoa kichwa na kuanza kula sehemu ya shingo huku akinifuata, nilishtuka nikarudi nyuma na kumfuata mfyeka majani, nikampora fyekeo na kumpiga, akaanguka na kukiachia kichwa,” alisimulia Simfukwe kabla ya watu kuanza kujaa na kumshangaa mtoto huyo.

Alisema taarifa za mtoto huyo kula kichwa cha mtoto mwenzake zilisambaa haraka na kumfikia daktari aliyekuwa akimtibu alipolazwa katika hospitali hiyo kwa uchunguzi wa akili yake baada ya kuanguka katika paa la kanisa linaloongozwa na Mchungaji Rwakatare.

“Daktari aliyekuwa akimtibu alifika kumuona. Alikuwa anamtibu kisaikolojia kabla ya kumwachia juzi, alishangaa kuona kijana aliyeachiwa siku mbili tu, amerudi tena kufanya ushirikina,” alisema.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, daktari huyo baada ya kumuona mtoto huyo alisema: “Wewe si ulikuwa wodini, ni miongoni mwa watoto walioletwa kutoka kwa Mama Rwakatare? Sisi tulidhani ni uongo, ile habari ilipotolewa, lakini mimi kwa namna hii, nimeamini na kuogopa. Kwa kweli yule mama hakuwa mwongo, hawa vijana kweli ni wachawi.”

Mvulana huyo alichukuliwa pamoja na kichwa cha mtoto na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Selander Bridge ambako alihojiwa na makachero wa kituo hicho na baadaye mkuu wa kituo hicho aliwathibitishia waandishi wa habari kuwa Mussa anakiri kuwa ni mchawi.

Alisema Mussa aliwaambia makachero hao kuwa alidondoka katika harakati za kishirikina usiku wa kuamkia jana.

Baadaye alitolewa mbele ya waandishi wa habarí na walipomuhoji alieleza kuwa, alianguka akiwa njiani kupeleka zawadi kwa shangazi yake.

“Sasa nikawa napeleka zawadi kwa shangazi, lakini watu wamenipora, wamenipiga, nataka nyama yangu, nataka nyama yangu,” alisema kwa taabu huku akionyesha kwamba hana nguvu.

Kauli ya kijana hiyo ilimfanya askari mmoja wa kike wa kituo hicho mwenye cheo cha koplo kuanza kulia machozi, huku akisema tangu alipojiunga na Jeshi la Polisi, hajawahi kukutana na unyama kiasi hicho.

Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Polisi Ilala, Charles Mkombo aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Aprili 25 mwaka huu, mama wa mtoto aliyeliwa kichwa, Upendo Dunstan, mkazi wa Kimara Baruti na mtoto wake, Salome Yohana, walikwenda kumtembelea shangazi wa mtoto huyo anayeishi Tabata.

Alisema, mama na mtoto huyo walikuwa wageni wa kulala kwa shangazi wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina moja la Furaha, lakini majira ya saa tatu usiku juzi, binti huyo aliyekuwa akicheza kwa kuingia ndani na kutoka, alitoweka ghafla, ndipo juhudi za kumtafuta zilipoanza.

Mkombo alisema kuwa, juhudi hizo ziligonga mwamba hadi jana majira hayo ya asubuhi, wakati jirani yake shangazi wa mtoto huyo, Lucas Lugaya, alipokuwa anakwenda kujisaidia katika choo cha shimo kilicho nje ya nyumba, alipoona kanga na jiwe juu yake, na alipoliondoa alikuta kiwiliwili cha mtoto huyo aliyefariki.

Polisi kwa kushirikiana na familia ya marehemu walikitambua kiwiliwili na kichwa alichokamatwa nacho Mussa, kuwa ni vya mtoto aliyepotea usiku juzi.

Baada ya kiwiliwili kupelekwa Muhimbili na kichwa kuoanishwa, familia na umati wa watu waliokusanyika uliangua kilio baada ya kubaini kuwa alikuwa ni mtoto Salome.

Mchungaji Rwakatare alifika katika Kituo cha Polisi, Selander Bridge, baada ya kupata taarifa za mvulana huyo ambazo zilikuwa zikisambaa kwa kasi na kumtambua Mussa kwamba ndiye aliyeanguka kanisani kwake wakati wakiwa kwenye maombi.

“Mtoto ni yule yule, mimi nimemuona aliyeanguka hapa wakati ule. Na aliponiona aliruka na kusema mama ana moto, sitaki anisogelee. Ninamshukuru Mungu amethibitisha mwenyewe. Wale watoto walianguka kwa ushirikina,” alisema Mchungaji Rwakatare.

Rwakatare alisema Mussa ni mtoto, lakini amekuwa akitumiwa katika matukio ya kishirikina. Alisema kama watumishi wa Mungu, wameamua kupambana na roho za kishirikina kwani ni nguvu za giza zinatumika.

“Muwape ‘support’ watumishi wa Mungu. Hii kazi inahitaji maombi, tusaidiane ili watu wafunguliwe,” alisema mchungaji huyo anayeendesha huduma za kiroho Mikocheni.

Mussa ametambuliwa kuwa anaishi maeneo ya JET na wazazi wake wanaishi Tabata. Hata hivyo, mwenyewe wakati akihojiwa na polisi pamoja na waandishi wa habari alieleza kuwa anaishi makaburini na chakula chake ni nyama za watu.

Kutoka gazeti la Tanzania Daima.



No comments: