Friday, April 04, 2008

Ugomvi wa maiti
Mahakama yatoa

hukumu



na Asha Bani

HATIMAYE Mahakama ya Wilaya Kinondoni Dar es Salaam, jana iliamuru mwili wa marehemu Paulo Goliama (40) uzikwe kwa imani ya dini ya Kikristo.

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Emilius Mchauru, baada ya kusikiliza kwa siku mbili mfululizo hoja za pande mbili, ambazo zilikuwa zikiomba mahakama hiyo iwaruhusu kumzika marehemu kwa imani ya dini zao.

Pande hizo ni mama wa marehemu, Anna Goliama ambaye ni Mkristo na waumini wa dini ya Kiislamu wanaowakilishwa na Katibu wa Masjidi ya Swafaa-Sinza, Muumini Bilali.

“Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili nimebaini hoja zilizowasilishwa na upande wa wadaiwa ni dhaifu na zimeshindwa kuishawishi mahakama ikubaliane na hoja hizo,” alisema Mchauru.

Mchauru, ambaye alianza kusoma hukumu hiyo saa 7:30 hadi saa 10:30, alichambua vifungu vya sheria kabla ya kutangaza uamuzi wa kesi hiyo, ambayo imevuta hisia za watu wengi.

Alisema kuwa hoja ya upande wa utetezi iliyokuwa ikidai kwamba walikuwa wakimfahamu marehemu tangu mwaka 1979, na kwamba alikuwa muumini mzuri wa Msikiti wa Swafaa, haijamshawishi kuamini kama ni kweli, kwa sababu kuna ushahidi unaoonyesha marehemu alibadili dini na kuwa Mwislamu mwaka 1996.

Alisema hoja nyingine iliyokuwa ikidai kwamba marehemu aliacha ujumbe wa maandishi kwamba yeye na mtoto wake wakifariki wazikwe kwa imani ya dini ya Kiislamu, pia imeshindwa kabisa kumshawishi kutokana na yeye kuamini maandishi yale yalikuwa kama wosia uliokosa ushahidi.

“Huo ujumbe wa maandishi mliokuwa mmeuleta mbele ya mahakama hii kama kielelezo, mahakama hii inauita ni wosia usiokuwa na ushahidi, hivyo kwa sababu hiyo, mahakama imekataa kupokea kielelezo hicho,” alisema Mchauru.

Alisema kwa mujibu wa hoja na vielelezo vilivyotolewa na mama wa marehemu na mke wa marehemu, Agnes Goliama, mahakama inakubali kuwa marehemu hadi anakufa alikuwa ni Mkristo.

Hilo linathibitishwa pia na uamuzi wa marehemu, wakati huo akiwa hai, kubadili jina la mtoto wake wa kwanza kuwa Anna, licha ya kuzaa na mwanamke ambaye ni Mwislamu, Atala Nasiri.

“Yawezekana kabisa marehemu alibadili dini na kuwa Mwislamu kwa ajili ya kutaka kumpata Atala na ndiyo maana ndoa ilipovunjika aliamua kurudi kundini na kutubu katika Kanisa lake la KKKT,” alisema Mchauru.

Mchauru alisema anapingana na vielelezo na ushaidi uliotolewa na upande wa utetezi kwamba mara kwa mara alikuwa akimtembelea marehemu nyumbani kwao na kusema kwamba kama alikuwa akimtembelea na kuwasiliana na marehemu mara kwa mara, alishindwaje kujua kama marehemu aliugua kichaa na kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Juzi upande wa wadaiwa ulidai kuwa mtoto wa marehemu aliyezaa na mtalaka wake alikuwa akiitwa Aina, jambo ambalo hakimu alisema mahakama imekata kuamini kwa sababu ushaidi unaonyesha jina la Anna ndilo lililosababisha ndoa kusambaratika.

Mchauru pia alitupilia mbali hoja ya wakili wa utetezi, Abubakar Salim, iliyokuwa ikidai kwamba mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

Hakimu Mchauru alisema kuwa hoja hiyo haina msingi wowote na kama wataona mahakama haikuwatendea haki, basi waende Mahakama Kuu.

Dakika chache baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, wakili wa utetezi aliwaeleza waandishi wa habari kwamba hakubaliani na uamuzi huo na kwamba leo atakata rufani Mahakama Kuu.

Wakati wakili akiyasema hayo, waumini wa dini ya Kiislamu waliofurika mahakamani hapo tangu saa sita mchana, walikosa simile na kuanza kupayuka ndani ya chumba cha mahakama na nje ya viunga vya mahakama, wakidai hukumu hiyo ni batili.

“Hii hukumu ni batili, hakimu ni ‘kanjanja’ … kama rais wa nchi hivi karibuni alivyowaita waandishi wa habari makanjanja, basi na baadhi ya mahakimu pia ni makanjanja kama huyu,” alisikika muumini mmoja akisema.

“Hata wakizika jioni ya leo tutaufukua na kuuzika tena kwa imani ya dini ya Kiislamu kwani sisi tunaamini huyu ni Mwislamu mwenzetu,” alisikika muumini mwingine akisema kwa jazba.

Waumini wa Kikristo walijikuta wakipiga vigelegele kwa furaha, huku wakiimba nyimbo za kumtukuza Mungu, baada ya mahakama kuwaruhusu wamzike marehemu kwa imani ya dini yao.

“Mungu ni mkubwa, amesikia kilio chetu… hapa ni Biblia tu, mtoto ni wa kwetu tumemlea na kumuuguza wenyewe hatukuona miongoni mwa hawa waumini wa dini ya Kiislamu ambao bila huruma wameamua kuzua vurugu kwenye msiba wa mwanangu, kuja kunisaidia kuuguza mwanangu…..nimesamehe, kwani yote ninayofanyiwa nimemwachia Mungu’ alisema Anna Goliama, mama mzazi wa marehemu.

Kwa mujibu wa mama wa marehemu, mazishi yalipangwa kufanyika jana jioni kwenye makaburi ya Sinza, Dar es Salaam.

Hata hivyo wakati mwili wa marehemu unaelekea kuzikwa, waumini wa dini ya Kiislamu waliokuwa mahakamani hapo waliwaambia waandishi wa habari kwamba jioni ya jana wangekwenda katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni kwa ajili ya kujadili hatima ya uamuzi huo wa mahakama na kuamua kusonga mbele.

Hata hivyo tangu mchana makachero wa polisi waliimarisha ulinzi katika eneo hilo la mahakama kwa hofu ya kutokea kwa vurugu.

Marehemu Paulo Goliama alifariki dunia machi 25 mwaka huu na baada ya taratibu zote za mazishi kukamilika, waumini wa dini ya Kiislamu waliingilia kati na kupinga marehemu asizikwe kwa imani ya dini hiyo.

Hata hivyo pande zote mbili zilipelekana mahakamani, wakati waumini wa dini ya Kiislamu walikimbilia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisumu, na Wakristo kukimbilia katika Mahakama ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Hata hivyo Mahakama ya Kisutu ilijitoa katika kuamua kesi hiyo na kuamuru ihamishiwe katika Mahakama ya Kinondoni.


juu

Maoni ya Wasomaji


Maoni yanayotolewa na wasomaji wa safu hii ni ya kwao na sio maoni ya kampuni ya Freemedia Ltd. Aidha sio maoni ya mtunzi au mwandishi wa habari au makala husika hapo juu. Maoni haya hayajahakikiwa wala kuafikiwa na kampuni ya Freemedia Ltd.
Maoni 2 yameshatolewa. (Nawe toa maoni yako!)


Dini ya kiislam haisemi hivyo hawa waumini wanavyofanya jamani, mbona watu wanapenda kupotosha mafundisho ya dini. Hivyo inavyokuwa ndio hatima ya marehemu. Kama ndugu waislam wanataka maiti za kuzika si waende Mererani wakawasaidie waislam waliofiwa na ndugu zao mazishi. Na kama anachosema huyo mama ni kweli basi wana makosa kwa kushindwa kumuuguza mwislam mwenzao na kusubiri mpaka afe ndio wakagombee maiti. Watupe ushahidi wa aya unaowaelekeza kufanya waliyofanya.

na Kipepe, Tanzania, - 4.04.08 @ 01:19 | #4891

Ama kweli ujinga ni ugonjwa mbaya kuliko UKIMWI! Ni aibu kwa dhehebu la kiislamu pamoja na kiongozi wenu kukosa busara na kuuthibitishia uma wa Watanzania jinsi Uislamu ulivyo hatari kwa amani Tanzania, na dunia nzima.

Kitendo cha kuvamia Kanisa wakati Ibada ya wafu ikiendelea, tena ikiambatana na machungua ya Ndugu wa marehemu kumpoteza mwenzao, ni kukosa heshima kwa watanzania wenzenu.

Ikiwa kweli mlimpenda marehemu Paulo Goliama, kwanini hamkumhudumia alipokua mgonjwa? Au ndiyo hizo sera zenu za "ndoa" za mkeka?

Isitoshe mmetoa ushahidi wa uongo mahakamani kuwa eti marehemu aliandika barua azikwe kiislamu. Hakika mlipaswa kuadhibiwa kwa kuidanganya mahakama. Mshukuruni hakimu kwa huruma yake na mkatubu na kuwaomba radhi wafiwa.

Ona jinsi mlivyojivunjia heshima hata baada ya uamuzi wa mahakama kwa kupayuka na kumtukana hakimu Mchauru kwa kumuita kanjanja. HAYA NDIYO MNAYOFUNDISHWA KATIKA UISLAMU? NA KITABU CHENU MNACHOKIITA "KITUKUFU" KINAHALALISHA KITENDO MLICHOKIFANYA?

FIKIRINI TENA JUU YA IMANI YENU KAMA MNAITAKIA DUNIA AMANI, nayi mkiwa wanadunia.

na Mpigne, Dar, - 4.04.08 @ 02:03 | #4898


Kutoka Tanzania Daima.



No comments: