Saturday, May 17, 2008

AYA ZA AYAH

Kiburi kaburi


Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.


Mpenzi Frank,

VIPI mpenzi wangu? Waendeleaje na maisha? Mimi hapa mzima nikipata nafasi ya kipekee ya kushuhudia vibweka vya wakubwa tu. Wanavyobweka, sina haja ya kuangalia viigizo vya luninga, napata igizo tofauti hapa nyumbani kila siku.

Tena, nimegundua kwamba pamoja na kujidai kote huko, hawana tofauti yoyote na walimu wetu wa shule huko kijijini. Wao nao kiburi mtu lakini kiburi cha bure. Si unamkumbuka yule mwalimu wetu mkuu pale kijijini wakati sisi tuko darasa la sita. Ndiyo yule Fyatu wa Mafyatu.

Alivyokuwa anatunyanyasa kila siku huku akidai kwamba anatupenda sana na mateso yote ni kwa faida yetu.

Alivyokuwa anatuchapa bila sababu na tukithubutu kumwambia kwamba si haki, alivyotuchapa zaidi hadi ile sehemu chini ya mwembe nyuma ya madarasa ikabatizwa ‘uwanja wa damu’.

Alivyokuwa anatulimisha kila siku kwa faida yake mwenyewe. Sisi tulale na njaa, yeye ajenge nyumba huko kwao!

Alivyokuwa anafisadi pesa zetu za shule lakini kamati ya shule ikimwuliza maswali alivyokuwa anawaziba mdomo kwa ukali eti wanajua nini, yeye ndiye anayejua.

Alivyokuwa anagawana pesa za shule na marafiki zake eti hata padre anakula kanisani kwa hiyo ana haki ya kupanga posho ya kitako apendavyo.

Alivyokuwa anatamba kwamba hatumwezi lolote maana yeye ni mkubwa, anajuana na wakubwa na wao watamlinda hata wazazi wafanye nini.

Yaani yule mwalimu alikuwa mwanaharamu. Nakumbuka nilivyokuwa nakunja karatasi ndani ya sketi ili kupunguza makali ya mipigo lakini haikusaidia kitu maana yule hakujali utu wala ustaarabu. Alikuwa anapiga apendavyo.

Na unakumbuka wale watoto wenzetu walioamua kuhama shule baada ya kuchoka kupigwa kila siku, na kulimishwa, na kutukanwa, na baada ya ahadi isiyo na hesabu kwamba anajali elimu yao wakati wanatolewa darasani kila siku?

Unakumbuka walivyofanyiwa? Kuchapwa tena, na kufungiwa ndani ya shule hadi waombe radhi na wakome kuomba uhamisho. Yaani badala ya kuangalia sababu zilizowafanya kuomba uhamisho, mwalimu aliwaita mahaini, waasi, wasaliti, wajeuri, wazururaji, wabwia unga ili mradi awatafutie kila tusi alilolibeba ndani ya mfuko wake. Halafu karudia kututambia tena eti yeye ni yeye, yeye na Mwenyekiti wa Kijiji ni chanda na pete, yeye ni mwandani wa mabosi wote, na yeyote mwenye kutaka kupigana naye, ni sawa na yai kupigana na jiwe. Tutapasuka tu na kumwagika mdomo.

Lakini kilichonishangaza ni jinsi wanafunzi wetu, hata wale ambao wamechangia sana damu ya uwanja walivyomshangilia mwalimu mkuu … ‘Babu … babe … babu … babe’ bila hata aibu. Ama kweli tunajiua sisi wenyewe.

Kisha mwalimu mkuu alizidi kutamba.

‘Ndiyo, acheni hawa wazazi wachache wa wakorofi wakilalamika. Kwanza wala si wa hapa. Wazazi wa hapa wanaojua mambo vizuri wananisifu kwa jinsi ninavyowaadabisha. Wanashangilia. Kama hamwamini nendeni kuwauliza.’

Mimi nilimwuliza baba lakini alitingisha kichwa tu.

‘Mwanangu tutafanya nini. Nataka usome tu. Sasa nikianza kupiga kelele na wewe utaadhibiwa vikali sana. Wataka kutafuta karatasi zaidi tena ndani ya sketi?’

Baba alitabasamu lakini mimi sikukubali kulainika.

‘Lakini si mngelalamika wote kwa pamoja.’

‘Kuna waoga wengi mno. Watatusaliti. Hebu vumilia kidogo mwanangu.’

Yaani hapo nilitaka kumchukia hata baba yangu. Kwa nini hatujali kiasi hicho? Kwa nini ananiacha kuteseka vile? Yaani mtu mmoja au hata watu wachache wenye nia mbaya waachwe tu kutuharibia maisha yetu na mustakabali wetu. Kisha wewe uliacha shule kabisa, eti ‘bora nipigwe na dunia kuliko yule mwanaharamu.’ Niliona shule chungu kwelikweli na baba niligoma kuongea naye zaidi ya kumsalimia asubuhi.

Ndiyo maana nilishangaa ile siku ya siku wakati yule mwalimu anajiandaa kupeleka watoto wengine uwanja wa damu. Ghafla likajitokeza kundi kubwa la wazazi, tena baba yangu akiwa mstari wa mbele, na kuzunguka ofisi ya shule. Lo, sote tulitoka darasani mara moja maana nani angekosa senema ya bure.

Wazazi walianza kusema kwa pamoja:

‘Ondoka hapa. Ondoka hapa. Acha kunyanyasa watoto wetu.’

Kumbe majitu ya kutamba ni maoga pia. Alipoona maji yamemfika shingoni yule mwalimu alitetemeka, alibembeleza, alijaribu kujieleza eti anakuwa mkali kwa faida yetu sisi wenyewe, anatulimisha ili tujifunze kilimo lakini wazazi walizidi kumzomea. Kwa hiyo, mwalimu mkuu alipoona kwamba hawataki kumsikia, ghafla alichomoka na kujaribu kuruka dirishani.

Yaani nilicheka, hasa suruali yake iliposhika kwenye msumari kidogo abaki ananing’inia bila suruali kuchanika. Wazazi wangetaka wangemshika papo hapo. Lakini wazazi hawakuwa na nia ya kumdhuru. Walitaka aondoke tu hivyo wakabaki wanamzomea huku mwalimu akikimbia kama mwehu.

‘Hilooooo ….fisadi ….. fisi …...’

Basi siku ile ilikuwa sherehe. Tulicheza ngoma siku ile hadi miguu ikauma. Lakini tuliweza kuona kweli walimu gani wanamjali mwalimu mkuu na walimu gani wanajali haki na elimu. Wale vibaraka wa mwalimu mkuu walijitoa kimyakimya lakini wengine walijiunga nasi katika kushangilia kuondoka kwa huyu. Na wazazi hivyohivyo.

Kumbe kushangilia kwetu kulikuwa bure. Kesho yake tuko darasani tunasoma kama kawaida, tukaona wingu la vumbi likipanuka, likipanuka, likipanuka hadi likatanda juu yetu kama kundi la tai walamizoga na katikati la wingu yakajitokeza magari matatu yaliyojaa mafyekafyeka ukome.

Ingawa tulikuwa tumekaa darasani tunasoma, wao wakaruka kama watu wanaoingia vitani na Wamarekani, na kuingia darasani na kupigapigapiga ovyo hadi sote tulikimbia. Kisha walitufuata hadi nyumbani huku wakipiga hadi hata kuku. Sijui kuku katika kuwalinda vitetea wake naye alikosea nini.

Na mwisho alijitokeza mwalimu mkuu akisindikizwa na mwenyekiti wa kijiji na mabosi wa elimu. Tukaitwa kwenye kikao huko tumezingirwa na fyekafyeka ukome. Tukasomewa risala jinsi tusivyo na adabu, tusivyo na shukrani, kwamba yule mwalimu mkuu amedondoshwa kutoka mbinguni kwa faida yetu na sisi ni waasi tu. Kadiri tulivyokaa kimya wale mabosi wakazidi kufoka hadi mzazi mmoja aliiuna mkono. Mafyekafyeka walishika marungu yao wakijiandaa kumshambulia lakini mwalimu mkuu aliashiria huyu aweze kusema maana alijua ni mwenzake.

Ndipo hapo siwezi kusahau mpenzi. Maana yule mzee alimgeuzia mwalimu mkuu mbao, hoja hadi hoja huku tukimshangilia, kwanza kwa wasiwasi kisha kwa nguvu kabisa maana hata fyekafyeka walipigwa butwaa na yule mwalimu mkuu na kiburi chake chote alionekana amevuliwa nguo zote. Ndipo hapo nikagundua kwamba hata katika kundi linaloonekana kuwa upande wa wanyanyasaji kwa sababu ya cheo chao, au dini yao, au kabila au nini sijui, wapo ambao cheo chao, na dini yao, na kabila lao ni haki tu. Wanaweza kunyamaza, wanaweza hata kushangilia kinafiki au ki-woga lakini hatimaye dhamira zao haziwezi kuwaruhusu kunyamazia ukatili.

Najua nimeshakusimulia hayo yote siku nyingine. Lakini usiniulize mpenzi kwa nini nakumbuka yote hayo leo. Utajaza mwenyewe na kama huwezi kujaza basi….

Akupendaye
Mwenye akili timamu
Hata hapa Jehanamu
Hidaya


mabala@gmail.com


Toka gazeti la Raia Mwema wiki hii

No comments: