* CUF, CCM waanza kususiana tena
* Wajiandaa kurejesha ya mwaka 2001
* Lipumba, Hamad waenda kwa IGP
* Maandamano yaitishwa Pemba J’mosi
na Deodatus Balile.
* Wajiandaa kurejesha ya mwaka 2001
* Lipumba, Hamad waenda kwa IGP
* Maandamano yaitishwa Pemba J’mosi
na Deodatus Balile.
KUNA kila dalili kuwa damu inakaribia kumwagika tena Zanzibar. Matukio yanayozidi kujiumba moja baada ya jingine, yanaielekeza Zanzibar kule ilikotokea miaka ya 2001.
Kauli ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) juu ya Tamko la Butiama la Chama Cha Mapinduzi (CCM), linaonekana limetonesha vidonda, hivyo chuki, uhasama, kununiana na kutoaminiana miongoni mwa Wazanzibari kumerejea tena.
“Pemba hali si nzuri. Tangu Tamko la CCM la Butiama, hadi leo mambo yanakwenda yakirejea kule tulikotoka… Leo watu wanasusia kupanda meli zinazomilikiwa na wafuasi wa CCM kutoka Pemba kuja Unguja, na mitaani mambo si shwari tena,” alisema Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid, ambaye pia ni Mbunge wa Wawi, Pemba.
Tamko la Butiama la CCM lilisema chama hicho kimsingi kinakubaliana na mapendekezo yaliyofikiwa na Kamati ya Makatibu Wakuu wa CCM na CUF. CUF kamati yao ilikuwa ikiongozwa na Maalim Seif Shariff Hamad, huku ya CCM ikiongozwa na Luteni Yusuf Makamba.
Kati ya mapendekezo yaliyotolewa, kubwa lilikuwa ni la kuunda Serikali ya Mseto, ambayo ingetoa fursa ya CCM kama chama kilichoshinda uchaguzi wa mwaka 2005 kutoa Rais wa Zanzibar na CUF kama chama kilichopata ushindi wa pili kutoa Naibu Rais wa Kwanza.
Katika muundo huo, pia angekuwa Naibu Rais wa Pili, ambaye angetokana na chama kilichoshinda uchaguzi, hapana shaka CCM, ambaye angekuwa anaendesha shughuli za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Baraza la Wawakilishi, kazi inayofanywa na Waziri Kiongozi kwa sasa.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa Zanzibar kuna kundi la viongozi wahafidhina wenye kuona iwapo mabadiliko hayo yangetokea, basi wangepoteza nyadhifa walizonazo, hivyo wakamzunguka Rais Amani Abeid Karume na kumpenyezea hoja ya kutaka ziitishwe kura za maoni katika kukubali mapendekezo ya Kamati ya Makatibu wa Kamati ya Mwafaka, wazo ambalo naye aliliunga mkono bila kujua madhara yake.
Chini ya utaratibu mpya, Cheo cha Waziri Kiongozi, kilikuwa kinakufa, hivyo ni wazi hata Natibu Waziri Kiongozi, cheo anachokishikilia kiongozi anayedhaniwa kuwa kinara wa kundi la wahafidhina, Juma Ali Shamuhuna nacho kilikuwa kinakufa kifo cha asili, hivyo angekwenda na maji.
Shamuhuna ambaye wana-CCM wamekwisha kumuonjesha joto ya jiwe kwa kumnyima kura za Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, kama ni shati basi anaona vishikizo vyote vimekwishakatika kimebaki kimoja hiki cha Unaibu Waziri Kiongozi, hivyo yeyote anayetishia uwepo wa cheo hicho, kwake ni adui mkubwa.
Katika misingi hiyo, wiki hii amesikika akitamka hadharani huku akiapiza mizimu na mbingu kuwa hata kukitokea nini, basi ifahamike kuwa kwa Zanzibar haitakaa ikatokea Serikali ya Mseto. Haya ni maneno yale yale yaliyovunja miafaka iliyopita.
“Matamko ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kama hili la Juma Shamuhuna, yanaondoa kabisa matumaini ya mshikamano kwa Wazanzibari… Wapemba wanaona wametengwa kabisaaaa, maana hata hiyo asilimia 15 ya kura alizopata Pemba Karume, hakuzitumia kuchagua waziri yeyote… huyu mmoja aliyemteua Bi Zainab Omar, hana wizara maalumu na kapewa ofisi Pemba peke yake.
“Wananchi wamekata tamaa. Matumaini yaliyokuwa yamerejeshwa na mwafaka, kwamba sasa ajira zingeanza kupatikana kwa usawa, pato la taifa lingeongezeka na uchumi wa nchi kutengamaa yote yamepotea sasa… Karume sasa amesafiri kwenda Marekani, si ajabu atatumia dola 300,000 (karibu Sh milioni 360), kwenda kushukuru msaada wa vitabu wa dola 100,000 (karibu Sh milioni 120).
“Haya sisi CUF tungeingia serikalini tungeyazuia. Matumizi ya ovyo yangebadilika. Hali ingekuwa kama ilivyo sasa kwenye Serikali ya Muungano. Baada ya Bunge kukunjua makucha, kila mtu anakuwa makini anafahamu kuwa system (mfumo) zinafanya kazi,” alisema Hamad Rashid huku akionyesha uchungu usoni.
Kutokana na hali ya hewa kuchafuka huko Pemba na Unguja, viongozi wa CUF wameanzisha kampeni maalumu ya kuwasilisha ujumbe wao kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa kuwajulisha nini kilichotokea Zanzibar na wao wanalishughulikiaje suala hilo.
Kwa sasa wamekwisha kuwasiliana na Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa na Askofu Mkuu wa Anglikana, Dk. Valentino Mokiwa. Hawa wote wanawaeleza hali inavyozidi kuchafuka Zanzibar. Pia Wamemuona Katibu wa Kamati ya Kutetea haki za Waislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Wiki hii pia ujumbe mzito kutoka CUF, ukiongozwa na Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, umekwenda ofisini kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Said Mwema, naye ukamweleza hali ilivyo Zanzibar.
Hamad Rashid alipoulizwa IGP aliwapokeaje, akasema kwa ufupi tu: “Ametwambia ametusikia na atayafanyia kazi tuliyomweleza… sisi kwa upande wetu tumetimiza wajibu wetu. Tuna kazi ya kuziba viashiria vya uvunjifu wa amani, utulivu, mshikamano na upendo. CCM wanapaswa kuliona hili kwa uharaka mkubwa.
“Uongozi wa CCM wafahamu kwamba wao ndiyo wanaoendesha nchi. Rais (Jakaya) Kikwete asimamie suala hili CCM watie saini mwafaka huu vinginevyo hali itakuwa mbaya,” alisema Hamad Rashid.
Alipohojiwa na Rai juu ya chapisho la Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, kuwa hakuwezi kuwapo Serikali ya Mseto hadi mwaka 2010, alisema ana wasiwasi huenda Msekwa hajui anachokisema na wala hajui anenalo.
“Tutakuwa tunafanya nini katika kipindi cha mpito? Mwafaka huu ni kwa ajili ya uchaguzi uliovurugika wa 2005, na lengo ilikuwa ni kwamba tuunde Mseto ili tupate free and fair elections (uchaguzi huru na wa haki). Sasa hiyo 2010 tufanyeje? Tutafanya uchaguzi under what circumstances (katika mazingira yapi)… hajui (Msekwa) anenalo,” alisema Hamad Rashid.
Mazungumzo yalipotajwa kuvunjika, CUF walitangaza kuwa sasa wataanza kufanya maandamano makubwa katika nchi nzima. Tayari wamefanya maandamano Zanzibar yaliyopata maelfu ya wafuasi.
Jumamosi ya wiki hii, sasa wametangaza rasmi kuwa watafanya maandamano ya mwaka huko Pemba. “Nashindwa hata kukwambia hali itakuwaje. Tutafanya maandamano makubwa ajabu huko Pemba. Jumamosi tunataka kuionyesha dunia kuwa haki imeporwa,” Mkurugenzi wa Vijana, Salim Biman, aliliambia Rai kwa njia ya simu juzi.
Hofu inayojengeka hapa ni iwapo Polisi wataamua kupambana na wafuasi wa CUF katika maandamano hayo huko kisiwani Pemba, basi hali inaweza kuwa mbaya.
Mmoja wa viongozi wakuu wa CCM, aliyeomba asitajwe, yeye alisema haelewi kwa nini watu hawaoni hali iliyopo Zanzibar. “Pale tayari kumemwagiwa petroli. Kinachohitajika ni kichaa kuwasha kiberiti, nchi nzima inawaka moto. Sijui kwa nini tunapoteza kumbukumbu haraka hivi. Yaliyotokea 2001, hayako mbali… lazima tukubali kubadilika, tuingie mwafaka na CUF,” alisema kada huyo.
Mazingira anayokumbushia ya mwaka 2001, yalitokana na kuvunjika kwa mwafaka wa Juni 9, mwaka 1999. Katika mwafaka huu uliosimamiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chifu Emeka Anyaoku, CCM na CUF ilikuwa wamekubaliana kumaliza matatizo ya kisiasa Zanzibar, lakini chokochoko za viongozi wa ndani ya CCM zikavunja mwafaka huo.
Wakati huo kundi la mahafidhina lilikuwa linaongozwa na rais aliyestaafu mwaka 2000, Komandoo Dk. Salmin Amour, kupinga madai ya CUF waliokuwa wakisema uchaguzi wa mwaka 2005 haukuwa huru na wa haki. Katika uchaguzi huo, Dk. Salmin alitangazwa mshindi kwa kupata kura asilimia 50.2 dhidi ya asilimia 49.8 za Seif Shariff Hamad.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CUF walisusia vikao vya Baraza hilo, na mgomo uliendelea hadi mwaka 1999, ulipotiwa saini mwafaka wa kwanza. Wakati wajumbe wakisusia vikao, wananchi mitaani walikuwa wakisusiana sherehe, harusi na misiba.
Vurugu hizo zilipoa kidogo, lakini baada ya mwaka mmoja ziliamshwa na uchaguzi wa mwaka 2000 ambao CUF walisema Seif aliibiwa tena kura na Karume. Zamu hii hali ilikuwa mbaya. Katika kipindi kifupi, watu walianza kuwekeana kinyesi kwenye visima vya maji kulingana na nani ni mfuasi wa chama kipi, huku masikani zikichomwa moto.
Kilele cha vurugu hizo kilikuwa mwaka 2001, wakati CUF walipofanya maandamano makubwa wakapambana na polisi, ambapo takwimu zisizo rasmi zinasema watu 50 waliuawa, ila Ripoti ya Brigedia Jenerali Hashim Mbita, ilibainisha kuwa waliokufa katika mapambano hayo walikuwa watu 32.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, mapambano hayo yalizalisha wakimbizi waliokimbilia Shimoni-Mombasa, nchini Kenya, ambako walikaa kwa muda mrefu.
Kitendo cha mwafaka kuvunjika kinaashiria kuwa Watanzania wanaoishi Unguja na Pemba, tayari wameanza kurejesha chuki hizo, kwani habari zilizothibitishwa na Hamad Rashid pamoja na kususiana huduma za jamii, sasa wameamua kutopeleka hata bidhaa zinazozalishwa Pemba kwenda kuuza Unguja.
“Unguja hawalimi sana, ni mjini kule. Sasa wenyewe Pemba wameamua kuwa wasipeleke ndizi na maembe yao kuuza kule Unguja… na mazao mengine ya kilimo. Hii ni hatari kweli,” alisema.
CCM wao wanaamini kuwa mazungumzo hayo hayajavunjika na wanaendelea kufanya kila kinachowezekana yaweze kukamilishwa. Hata hivyo, wanasisitiza kuwa yanayotaka kutokea ni mabadiliko makubwa katika Katiba ya Zanzibar na ile ya Muungano, hivyo inabidi wananchi washirikishwe kwa njia ya kura ya maoni.
No comments:
Post a Comment