Thursday, May 08, 2008


Muafaka Zanzibar:

Chama tawala CCM

chamkana Shamhuna


Na Muhibu Said.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kauli ya Naibu Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Ali Juma Shamhuna kwamba kwa sasa hakuna uwezekano wa kuundwa kwa Serikali ya Mseto visiwani humo, ni maoni yake na si msimamo wa chama hicho.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Kapteni John Chiligati alisema jana kuwa msimamo wa CCM, umeshatolewa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu (NEC-CCM), kilichofanyika Butiama, mkoani Mara, Machi mwaka huu na si kama alivyosema Shamhuna.

"Yeye (Shamhuna) kama Mtanzania na mwana CCM ana haki kutoa maoni, lakini msimamo wa CCM tulishautoa Butiama," alisema Chiligati ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Alisema katika msimamo wa Butiama, mapendekezo ya mwafaka wa kisiasa Zanzibar, NEC-CCM iliyakubali kimsingi, lakini baada ya kubaini kuwapo na mapungufu, iliiagiza kamati ya CCM ya mazungumzo ya mwafaka ikutane na kamati ya mazungumzo hayo ya CUF ili wayafanyie marekebisho.

"Hivyo tunasubiri wenzetu wa CUF wamalize maandamano yao kisha tukutane tuendelee na mazungumzo," alisema Chiligati.

Hata hivyo, alipokumbushwa kuhusu msimamo uliokwishatolewa na CUF wa kutokubali kuendelea na mazungumzo na CCM na kumtaka Rais Jakaya Kikwete awakutanishe Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad na Rais Aman Abeid Karume, Chiligati alisema wanachoheshimu wao ni maamuzi ya NEC-CCM.

"Mwamuzi wa mwisho ni NEC, sasa wanapotuchagulia mtu wa kukutana naye na kwamba, hawataki kuzungumza na huyu kwasababu saini yake haitambuliwi, hatuwaelewi," alisema Chiligati.

Akijibu hoja mbalimbali kutoka kwa wazee wa CCM wa Jimbo lake la Donge, Mkoa wa Kaskazini Unguja waliokuwa wakitaka maelezo ya kina juu ya chanzo cha kuzuka mjadala wa Serikali ya Mseto Zanzibar Aprili 5, mwaka huu, Shamhuna alisema hivi sasa hakuna uwezekano wa kuundwa kwa Serikali ya Mseto kati ya CCM na CUF visiwani humo.

Alisema kwa kuwa wananchi wa jimbo lake walimwita na kumweleza msimamo wao wa kupinga serikali ya mseto, atayawasilisha maoni hayo kwenye Baraza la Wawakilishi na kama kuna watu watakaosema anachafua hali ya hewa na kisha kufukuzwa, atarudi kwa wananchi waliomchagua kufanya nao kazi.

Seif Shariff Hamad sio Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, kama ni suala la kutafuta vyeo, ili eti Seif Shariff awe Waziri Kiongozi katika Serikali ya Mseto haiwezekani. Apate cheo kwa Katiba ipi, maana katiba yenu haizungumzii Serikali ya aina hiyo na hata Katiba ya Tanzania nayo haisemi hivyo, alisema Shamhuna akiwahutubia wazee wa jimboni kwake.

Alisema dunia ya leo si ya kulazimishana na pia dunia haikulazimisha Serikali ya Mseto kwani hata mataifa makubwa hayana mfumo wa utawala wa aina hiyo.

Siku iliyofuata, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alikuja juu na kumtaka Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kueleza msimamo wake kuhusiana na kauli hiyo.

Alisema kauli hiyo ya Shamhuna inachochea chuki na kuvuruga mchakato ulioanza wa kuupatia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, hivyo wanamuomba Rais Kikwete aeleze kama huo ndio msimamo wa CCM au la.

Alisema kauli ya Shamhuna inatoa taswira mbaya kwa CCM katika jamii, kwani inadhihirisha kuwa chama hicho kikongwe hakina nidhamu wala utaratibu katika maamuzi yake.

Alisema ni aibu kwa kiongozi mwandamizi wa serikali kama alivyo Shamhuna kutoa kauli inayopingana na maamuzi ya watendaji wakuu wa chama chake, hasa mwenyekiti wake Kikwete ambaye ameonyesha nia thabiti ya kumaliza tatizo la mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar kwa amani.

Naye Msaidizi Maalum wa Katibu Mkuu katika Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa CUF, Ismail Jussa alisema chama chao hakitishwi wala hakibabaishwi na kauli za kutapatapa za wanasiasa, kama Shamhuna waliofilisika kisiasa ambao wamekataliwa hata ndani ya CCM yenyewe.

Jussa alidai kuwa ana uhakika kwamba hakuna mwananchi aliyemwita Shamhuna huko Donge, lakini ni mwenyewe ndiye aliyewaandaa wananchi hao na hata kuwaelekeza cha kumwambia ili apate nafasi ya kuendeleza ajenda yake.

No comments: