Tuesday, May 13, 2008


Hatukubali Mkapa

adhalilishwe -Pinda



*Asema wataalamu wetu ni butu kujadili mikataba
*Azungumzia mapokezi ya vigogo waliowajibishwa


Na Mwandishi Wetu


SERIKALI imesema haipo tayari kuona Rais mstaafu Bw. Benjamini Mkapa anadhalilishwa kwa kuzomewa hadharani na haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atayebainika kufanya hivyo kwani kufanya hivyo ni ukiukaji wa utawala wa sheria.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda alipokutana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika mkutano wa kufahamiana na kubadilishana mawazo ambapo pia walipata fursa ya kumuuliza maswali.

Akijibu swali kuhusu taarifa za madai ya kukamatwa kwa baadhi ya watu wanaotuhumiwa kumwita Rais huyo fisadi hivi karibuni, Bw. Pinda hakuthibitisha wala kukanusha jambo hilo lakini alisema kamwe hafurahii kuona Rais Mkapa anazomewa anapopita mitaani.

Bw. Pinda alisema yapo mambo yanaweza kufanywa lakini si sahihi hata kidogo kumzomea kiongozi huyo na kwamba vitendo vya kumdhalilisha kamwe havitaruhusiwa katika nchi inayofuata misingi ya utawala wa sheria.

" Hatuwezi kuwa watu wasiojiheshimu, kwa lengo hilo hapana ! waliomwita mhujumu uchumi huenda tabia yao haikuwa ya Kitanzania. Siwezi kufurahia kuona Mkapa anapita anazomewa hata kidogo ! Yapo mambo yanaweza kufanywa, kumshtaki mtu si tatizo lakini sio sahihi kumhukumu mtu bila taratibu kufikiwa," alisema na kusisitiza;

Vitendo vya kumdhalilisha kama Taifa tuseme hapana ! katika nchi inayoongozwa chini ya utawala wa sheria tusichukue sheria mikononi. Siafiki Rais Mkapa kuzomewa, ana heshima yake ni binadamu anastahili heshima, zipo taratibu zinazotakiwa," alionya

Akijibu swali lililohoji usafi wa mawaziri waliobaki madarakani baada ya Rais Jakaya Kikwete kupangua baraza hilo, Bw. Pinda alisema hawezi kuwathibitisha kwa hilo kwani waliomo serikalini ni binadamu kama watu wengine na kufafanua kuwa jukumu lake kama Waziri Mkuu ni kuhakikisha timu hiyo inafanya kazi kwa maadili yanayokubalika na umma.

Alisema Rais Kikwete anajitahidi kutambua na kuteua viongozi wazuri bali matatizo yanayojitokeza ni wahusika wenyewe wanapoingia kwenye dhamana hizo na kusisitiza kwamba suala la uadilifu vita dhidi ya rushwa ni vita endelevu.

"Rais amejitahidi kutambua watu wazuri lakini wanapoingia wanaanza kuhangaika kuangalia huku na huko. Yapo yaliyotokea siku za nyuma lakini hawa tuliona tutazidi kusisitiza suala la uadilifu. Hii ni vita endelevu. Hakuna rushwa inayotoka mbinguni zote zinatoka humu humu," alisema.

Richomond
Kuhusu swali la nani anaendelea kupokea pesa zinazodaiwa kulipwa kampuni hiyo kila siku na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),Bw. Pinda, alisema kampuni hiyo sasa haipo na majukumu yake yalichukuliwa na Dowans ndiyo inapaswa kuhusishwa kwa hilo.
Hata hivyo, alisema uchunguzi kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na Tume teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa zabuni ya Richmond bungeni yanaendelea kufanyiwa kazi na tayari kwenye maeneo mengine utekelezaji unaendelea.

Sambamba na hilo alizungumzia mkataba Kampuni ya Kupakua na Kupakia Mizigo Bandarini ya (TICTS) na kueleza kuwa pamoja na uhalali wake umeonekana kuwa na dosari nyingi.

Bw. Pinda alisema kinacholiumiza Taifa sasa na uwezo hafifu wa wataalam kupitia na kukubaliana juu ya mikataba mbalimbali. Alisema kutokana tatizo hilo serikali itaangalia uwezekano wa kushirikisha kamati huru za wataalam wa masuala ya sheria kupitia na kutoa mapendekezo ya mikataba mbalimbali kabla haijasainiwa, ili kupunguza dosari hizo.


Kugawa Mikoa

Alisema hivi sasa katika ofisi yake kuna maombi mengi ya kugawa mikoa, wilaya majimbo na vijiji. Hata hivyo alisema jambo hilo linahitaji gharama kubwa kwani kuanzisha mkoa mmoja zinahitajika si chini ya sh. bilioni 10 na wilaya ni kati ya sh. bilioni tano hadi sita.

Kuhusu majimbo alisema suala hilo linategemea zaidi ushauri wa Tume ya Uchaguzi kama ina pesa kuweza kuhudumia majimbo hayo mapya.

Aliko Balali
"Ukiniuliza yuko wapi sijui" alisema Bw. Pinda alipoombwa kutoa taarifa za uhakika kuhusu aliko gavana huyo wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania
( BoT) . Alisema Bw. Balali anahitajika kutokana na masuala ya BoT na kurudia kauli ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bw. Salva Rweyemamu kwamba gavana huyo akihitajika si jambo kubwa, atapatikana.

Bei ya Mafuta

Kuhusu ongezeko la bei za mafuta linalochangia kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali, Bw. Pinda alisema Mamlaka ya Udhibiti wa Bei ya Umeme na Maji ( EWURA) inajitajihidi katika suala hili lakini bei inazidi kupanda siku hadi siku.

Alisema serikali inaangalia uwezekano wa kuagiza bidhaa hiyo kiasi kikubwa kwa wakati mmoja hali itakayosadia kushusha bei kwenye vituo vya mafuta.

Mapokezi vigogo

Akijibu swali lililohoji kuwa anajisikia viongozi waliowajibishwa kwa tuhuma za ufisadi kupokelewa kwa makeke majimboni mwao, alisema huo ni mtazamo wa wananchi wao majimboni na kwamba tuhuma hizo haziwaondolei upendo wao. Alisema serikali haina uwezo kuwahukumu kabla ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Bw. Pinda aliwataka watendaji wote wakiwemo mawaziri kuwa wazi kwa vyombo vya habari na kushirikiana kutoa taarifa, binafsi alisema amejipangia utaratibu wa kukutana na wahariri kila baada ya miezi mitatu kujadili na kujibu hoja mbalimbali kwa manufaa ya jamii.


Alivipongeza vyombo hivyo na kueleza kuwa sasa vimeifikisha serikali pagumu kutoka na umakini wa kufuatilia masuala mbalimbali jambo ambalo alisema kuna mambo mengi yanayofanyika sasa ambayo kama vyombo hivyo vingelala yasingefanyika.

" Vyombo vya habari vimetufikisha pagumu tuliomo serikalini, tunafanya kazi mmesukuma mambo, kama 'press' ingelala yasingefanyika " alisema na kuahidi kuwa serikali itajitahidi kuhakikisha uhuru zaidi kwa vyombo vya habari unakuwepo.

1 comment:

Anonymous said...

HEHE PINDA USIYAPINDE MAMBO,VIONGOZI WA BONGO MMEZIDI, KWA MASILAHI YENU KILA CHA ULAYA NA MAREKANI MNAIGA, KWA MANUFAA YA WALIOWATEUWA SERIKALI HAINA PESA,MNAPOINGIA KWENYE SIASA MKUBALI YOTE KAMA MNAVYOIGA MASILAHI YENU KAMA WALIVYO VIONGOZI WA ULAYA,KUZOMEWA KWA MWANASIASA NI KITU CHA KAWAIDA, ANAZOMEWA BUSH; MALIKIA SEMBUSE HUYU AMBAYE TUNAJUA TOSHA NI FISADI NA HATAKI KUJIBU AU KUSEMA KWA SABABU YAKIBURI CHAKE WACHA WAMZOMEE,WATANZANIA TUAMKE TUACHANE NA VIONGOZI WALIOZEA SHIKAMOO ZA UNAFIKI JAPO TUMEWAZIDI UMRI:LAZIMA TUJUWE SIASA SI NYUMBA ZETU TULIKOZOWEA SHIKAMOO,