Friday, May 30, 2008

Kutokana na kile kinachoaminika kukiuka maadili, Serikali imetishia kuzifuta Bendi za Akudo Impact, FM Academia na TOT-Respect kwa kuruhusu wanenguaji wake kucheza nusu uchi....

Onyo hilo la Serikali limetolewa kupitia Baraza la Sanaa la Taifa, ambalo limeziandikia barua bendi hizo na kutaka kuanzia sasa wahakikishe wanenguaji wao wanavaa nguo za heshima.

“Baraza hili halitasita kuchukua hatua ikiwemo ya kufungia bendi zenu ikithibitika kuwa mnaendelea na ukiukaji huo,” ilisema barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, F. Magoti.

Magoti katika barua yake hiyo yenye kumbukumbu na. BST/MB/FMA/VOL. l/28 ya Juni 27, mwaka huu alisema bendi hizo kwa makusudi kabisa zinaonekana kukiuka maadili ya Watanzania kwa kuruhusu vichupi kutawala katika maonyesho yao.

“Tendo hili ni ukiukwaji wa maadili ya Watanzania na ni kuwadhalilisha wanenguaji na watazamaji wa maonyesho yenu.
“Kumbukeni kwamba maonyesho yenu hayaishii katika maholi ya dansi pekee, bali yamekuwa yakiharibu kwa kuwaonyesha watoto wadogo kupitia vyombo vya habari...,” ilisema barua hiyo.

Wakati Akudo, FM Academia na TOT Respect zikiwa zimekalia kuti kavu, Bendi za African Stars ‘Twanga Pepeta’ International na Diamond Musica zenyewe zimesalimika katika onyo hilo la Serikali.

Baadhi ya mashabiki wa muziki wa dansi walionekana kufurahia hatua hiyo ya Serikali na kusema hiyo inaonyesha jinsi watendaji walio chini ya Rais Jakaya Kikwete walivyopania kutekeleza majukumu yao.

1 comment:

Anonymous said...

Kwangu mimi ni jambo la kufurahisha kwamba serikali inaingilia kati ili kuhifadhi hadhi ya wananchi. Mara nyingi nashindwa kuwaonyesha wenyeji wangu video za TZ kwa ajili wakiona yale maviuno yao huwa wanagutuka sana. Je, hakuna dansi namna nyingine?