Thursday, May 01, 2008



Mawaziri wengine

kwenda na maji



Kikwete ashtuka, aagiza wote wachunguzwe


ILI kukwepa makosa ya kiuteuzi, Rais Jakaya Kikwete sasa ameamua kuwachunguza mawaziri wake wote na wanasiasa ambao wanatarajiwa kuwamo katika timu yake ijayo, Raia Mwema imeambiwa.

Habari za wiki hii zinasema hatua hiyo ya Rais Kikwete inalenga kukwepa makosa kama yaliyofanyika katika uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ambaye tangu mwanzo uteuzi wake ulikuwa ukitiliwa shaka na umma.

Chenge tayari amejiuzulu na sasa yuko katikati ya tuhuma za hodhi ya fedha nyingi zilizoko nje ya nchi zinazodaiwa kuwa zimepatikana katika mchakato wa ununuzi wa rada ya kiasi cha Sh bilioni 70/-.

Yeye ni waziri wa nne kujiuzulu katika kipindi cha chini ya miezi minne, akitanguliwa na mawaziri wengine watatu, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha, aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Afrika Mashariki, wao wakituhumiwa kuhusika na mradi tata wa umeme wa dharura uliokabidhiwa kampuni ya Richmond Development LLC ya Marekani.

Kutokana na kujiuzulu huko kwa wasaidizi wake muhimu mfululizo, imeelezwa sasa kwamba Rais Kikwete ameunda timu ya siri ya kuwachunguza kwa kina mawaziri wa sasa na wanasiasa ambao wanaweza kuingizwa katika serikali yake, huku akitafakari kwa kina muundo wa serikali yake.

Kwa mujibu wa habari hizo, Kikwete amejikuta akitafakari kwa makini mbinu na mkakati wa kujiepusha na aibu ambayo imeikumba serikali yake hasa baada ya kujiuzulu kwa Chenge ambaye alimrudisha katika serikali yake baada ya kuvunja Baraza la Mawaziri kutokana na kujiuzulu kwa Waziri Lowassa.

“Rais hivi sasa anatafakari jinsi ya kujiepusha kupata aibu kama aliyoipata kutokana na kujiuzulu mfululizo kwa mawaziri wake wanne kwa kuhusishwa na kashfa mbalimbali. Anaona hilo si jambo jema kwake na ndiyo maana anaangalia sasa asije kuteua watu ambao watakumbwa na kashfa nyingine na kulazimika kuvuruga tena serikali yake,” anaeleza ofisa mmoja ndani ya Serikali.

Imeelezwa kwamba uchunguzi huo unaoendelea kwa siri kubwa sana unawahusisha baadhi ya watu ambao hawamo serikalini kwa sasa wakishirikiana na watendaji wachache wa sasa ambao uadilifu wao hautiliwi shaka na unatarajiwa kumkabidhi Rais Kikwete taarifa wakati wowote kuanzia sasa.

Pamoja na kuwapo uchunguzi huo, habari za uhakika zinaeleza kwamba hivi sasa mawaziri na watendaji wengi serikalini wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu mno ya woga, kila mmoja akihofia kuhusishwa na kashfa.

“Hivi sasa wanasiasa na watendaji serikalini wanafanya kazi kwa woga mkubwa na baadhi wanafanya kazi bila kuamini yeyote. Hata baadhi ya mawaziri wanapoteza imani na wenzao na sasa wakipewa maagizo ama ushauri wanataka kila kitu kiwekwe kwa maandishi na wanaondoka na kopi za nyaraka kwenda nazo nyumbani ama mahali wanakopaamini,” anaeleza mtendaji mmoja.

Mtendaji huyo mwandamizi serikalini akizungumza kwa sharti la kutotaka kutajwa kwa sababu zilizo wazi, anasema wapo baadhi ya mawaziri ambao wanadiriki hata kuogopa maagizo ya Rais na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na sasa wakipewa maagizo wanaomba kupewa kwa maandishi hali ambayo imeelezwa kutishia tija katika utendaji kazi wa kila siku serikalini.

“Kupotea kwa imani miongoni mwa wanasiasa na watendaji hakuashirii hali nzuri hata kidogo kwa utendaji wa kila siku wa Serikali na hii inaathiri kwa kiasi kikubwa ufanisi,” anaendelea kueleza ofisa huyo ambaye yuko karibu na utendaji wa kila siku wa Serikali ya sasa.

Ikiwa imesalia miaka miwili tu kumaliza kipindi chake cha kwanza cha urais, Kikwete amejikuta akikabiliana na misukosuko mingi mfululizo inayoitikisa Serikali yake pamoja na asasi nyingine nyeti, hali ambayo imeelezwa kuwa si nzuri sana kwake.

Kwa muda mrefu sasa Serikali ya Kikwete imejikuta ikikabiliana na mambo yanayoibuka badala ya Serikali yenyewe kuibua mambo, hali ambayo imeelezwa kufanana sana na kazi ya “zimamoto”.

Mbali ya Serikali yake, Bunge nalo limekuwa katika misukosuko ambayo inatishia uimara wake, pamoja na kuwa sasa wabunge wameonekana “kuchangamka” zaidi kuisimamia Serikali lakini na wao kwa upande wao wamejikuta wakisuguana wao kwa wao na hata na Spika wao, Samuel Sitta.

Matukio yanayoelezwa kuanza kuitikisa Serikali ni pamoja na tuhuma zilizoielemea Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mradi wa umeme wa dharura uliokabidhiwa kwa kampuni ya Richmond Development LLC, sakata la rada na kuyumba kwa mazungumzo kati ya CCM na CUF, yanazidi kumyumbisha Kikwete.

Hata vikao vya CCM kijijini Butiama alikozaliwa na kuzikwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, vimeshindwa kutoa matunda yaliyokusudiwa na wengi ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wale wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi na kumaliza tofauti za kisiasa visiwani Zanzibar.

Awali iliripotiwa kwamba kumekuwapo mkakati maalumu wa kuwasafisha kwa zamu mawaziri wanaoandamwa na tuhuma za mbalimbali zilizofahamika na zile ambazo hazijaanikwa kwa sasa hali ambayo imewatia kiwewe mawaziri wengi wa sasa.

Hali hiyo ndiyo hasa iliyomsukuma Rais Kikwete kuamua kutafuta watu wa kumsaidia kuwachunguza mawaziri wa sasa na wale ambao anaamini kwamba wanaweza kuingia katika baraza lake jipya, kama ataamua kufanya mabadiliko makubwa.

Pamoja na kuwapo kwa tuhuma za kweli kwa baadhi ya mawaziri na wanasiasa, zipo taarifa kwamba baadhi ya watu wametumia nafasi huyo kuwatisha, kuwafitini ama kuwahujumu baadhi ya mawaziri kwa maslahi binafsi huku baadhi wakihaha kutafuta njia ya kujihami na kujisafisha.

Kwa sasa shutuma na hofu kubwa imeelekezwa kwa vyombo vya habari na kwa baadhi ya wanasiasa ambao kwa pamoja wanadaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine na kuiyumbisha Serikali, lakini imeelezwa kwamba Kikwete mwenyewe, “amekuwa akifurahishwa na hali hiyo” ambayo anasema inamsaidia kuisafisha Serikali yake bila ya yeye kupata lawama.

“Pamoja na watu kuona kwamba Kikwete anayumbishwa na hali ya sasa, yeye binafsi anafurahishwa sana kuona kwamba nchi imekomaa kidemokrasia na kwamba yeye binafsi hawezi kulaumiwa kwa vyovyote vile na yanayowakumba mawaziri wake. Binafsi aliwapa nafasi ya kujisafisha na kufanya naye kazi lakini kwa bahati mbaya wimbi la tuhuma za ufisadi limewakumba,” anasema ofisa mmoja mwandamizi wa serikali.

Ofisa huyo anakumbusha jinsi Kikwete alivyozungumza na watendaji wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) ambayo sasa imeboreshwa na kuongezewa kazi ya “kupambana” Februari, 2006 aliwaambia wazi wazi wasaidizi wake kwamba anawafahamu wala rushwa na kwamba amewapa muda wa kujirekebisha.

“Alipotoa kauli Mbeya miezi michache baada ya kuingia madarakani watu waliona kama anafanya mzaha lakini sasa yanayotokea ni matokeo ya kauli zake. Alisema anawafahamu wala rushwa na kuwapa muda wa kujirekebisha, sasa miaka miwili imepita yanayowakumba wasimlaumu tena,” anasema ofisa huyo.

Hata hivyo, kuchelewa kwake kuchukua hatua ama kuacha vyombo vingine kuchukua hatua kunaelezwa na wanasiasa mbalimbali kuwa si dalili njema kwa kiongozi ambaye ameingia madarakani kwa ridhaa ya zaidi ya asilimia 80 ya wapiga kura.

Pamoja na kuwa tuhuma nyingi ni zile zilizotokana na mambo yaliyofanyika wakati wa serikali ya awamu ya tatu, baadhi ya wahusika ni wale wale ambao wamo ndani ya serikali ya sasa baadhi wakiwa Rais Kikwete anawaamini ama kushirikiana nao, hali ambayo bado haimuepushi sana na baadhi ya tuhuma.

Mwanasiasa mmoja mkongwe na ambaye amekwisha kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri, aliliambia Raia Mwema wiki hii kwamba, hali ya sasa isipodhibitiwa nchi itaingia katika hali ya machafuko ambayo hatujajiandaa kukabiliana nayo.

“Sasa ukipita na gari zuri unaitwa fisadi na pole pole ‘mafisadi’ watapigwa mawe, magari yao yatachomwa moto nyumba zitavamiwa na kuchomwa moto. Watakaofanya hayo watakuwa ni wananchi ambao hawana vigezo vya kujua nani ni fisadi na nani anatumia mali halali. Serikali, asasi zisizo za kiraia, viongozi wa dini, wazee na vyombo vya habari ni lazima tushirikiane kuhakikisha hayo hayatokei,” alisema mwanasiasa huyo mstaafu.

Mwanasiasa huyo anayeheshimika, amesema hata kuibuliwa upya kwa mjadala wa uwezekano wa kumshindanisha Kikwete na mwana CCM mwingine katika uchaguzi wa mwaka 2010 ni dalili ya kuyumba kwa chama hicho tawala na serikali yake.

Umekua ni utamaduni wa CCM kumuachia Rais aliye madarakani amalizie vipindi viwili, lakini kwa sasa tayari kuna makundi ndani ya CCM wakiwamo wale waliokumbwa na wimbi la tuhuma za ufisadi, yameanza kupanga mikakati ya kumpinga Kikwete 2010.

Mikakati hiyo imeelezwa kufikia hatua mbaya zaidi ya kuwapo kwa vyombo mbadala vya ‘kiserikali’ vinavyofanya kazi mahsusi ya kufuatilia nyendo za wale wanaoonekana kuwa tishio kwa mikakati hiyo na hivyo kuendelea kupanua wigo wa mtikisiko ndani ya Serikali ya Kikwete na ndani ya CCM.



No comments: