Friday, May 02, 2008

AYA ZA AYAH

Luninga zetu na ushambenga

uliovuka mipaka



Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.


Mpenzi Frank,

NAKUMIC Bwana, lini utakuja kunifariji? Siku zote hizi hujapata hata safari moja ya biashara uje usuuze roho yangu mpenzi wa moyo? Au kuna wengine wanakusuuza na wewe? Mara nyingine hapa, nakaa nasononeka peke yangu na sina wa kumtulia mzigo mzito wa moyo.

Kama wiki hii mpenzi. Si uliona picha ya mtoto aliyekatwa kichwa? Yaani kuona vile nilitaka kutapika. Kwanza, kweli utu wetu umekuwa butu kama alivyosema yule fyatu Makengeza. Hata kama ni uchawi, ni unyama gani unaowafanya watu kujiunga na wachawi namna hii.

Lakini pia nalaumu sana vyombo vya habari. Wakihaha kuwabana wakubwa wanaotufanyia unyama kila siku nafurahi sana. Lakini kuna mambo mengine wanakosea sana. Itakuwaje wanaonyeshe mambo ya kutisha namna hii bila kujali nani anaangalia? Inawaathiri vipi?

Kwa mfano, watoto wadogo wa dada yake mama bosi (MB) walikuwapo. Walikuwa wanachezacheza pembeni mwa luninga. Ghafla zikatolewa zile picha za yule binti aliyechinjwa. Basi yule binti mdogo pale akaangalia akaanza kupiga yowe papo hapo na ingawa nilijitahidi kuzima luninga, haikusaidia kitu. Alikimbia na kwenda kujificha nyuma ya kabati akifikiri kwamba watakuja kukata kichwa chake na yeye.

Ilibidi MB afanye kazi ya ziada kumbembeleza atoke kula. Tena bahati mbaya alianza kutoka bosi akaingia kwa mbwembwe zake, mtoto akafikiri ni mchinjaji akakimbia tena kujificha. Hapo Bosi alilazimika kujiunga na wabembelezaji hadi akakubali kutoka. Na hata hivyo alikataa kula nyama kabisa akisema: ‘Naona damu … naona damu.’ Kumbe na bosi alikuwa amekwishaona zile picha pia. Wacha afoke.

‘Unaona sasa? Hawa washenzi wa vyombo vya habari wanaimba haki za binadamu haki za binadamu. Kumbe na wao ni wa kwanza kuvunja hizi haki.’

Akamwangalia mtoto wake akitegemea ataanza kubisha lakini BB alibaki kimya. Bosi aliendelea.

‘Tena safari hii hawawezi kujidai ni magazeti ya udaku tu. Kila kituo cha luninga kimeonyesha picha hizi tena na tena na tena. Hivi wana akili gani? Halafu wanawazonga wafiwa na kuanza kuwauliza wanajisikiaje kutokana na kisa hiki. Kwani walitegemea wafiwa waseme wanashangilia? Wanajua jibu lakini bado wanawasumbua. Hawawezi kuheshimu faragha za mtu? Yaani mimi naomboleza wewe ni nani kuniuliza maswali hapo? Haki ya Mungu ingekuwa mimi ningevunja kipaza sauti chao papo hapo.’

BB akaamka.

‘Lakini huoni baba tatizo ni sisi pia? Kwa nini watu walikusanyika pale kuangalia kichwa cha yule binti? Wanapigania kuangalia, na si ajabu walikuwa wanapigania kutoa maelezo yao kwenye luninga.’

‘Sawa kabisa. Lakini kama watu ni washambenga, haina maana kwamba vyombo vya habari videkeze ushambenga huo. Sheria zipo, maadili yapo. Hata huyu mtoto mwingine anayedaiwa kufanya maovu hayo si haki aonyeshwe mbele ya hadhara namna hii. Lakini kila kituo kinataka umaarufu, au tuseme kinaogopa kupoteza umaarufu kwa kutoonyesha.’

‘Si biashara baba!’

‘Biashara ya ufisadi. Lazima tuwadhibiti. Vyombo vingine viko pale tu kutangaza umaarufu wa mwenye chombo au kumtetea akiumbuliwa. Huo ndio uhuru tunaoutaka? Wao walichaguliwa na nani ili wajidai kutudhibiti hivyo?’

Hatimaye BB alichokozeka.

‘Ahaa! Kumbe una madonge wenzako wanaumbuka? Ndiyo maana unataka kuwadhibiti.’

‘Ohoo, Bi Vijisiasa ameamka. Vidhibitiwe kwa vyote.’

‘Lakini baba huwezi kulinganisha wanaosababisha umasikini kwa mamilioni ya watu kwa ulafi wao binafsi na hivi vyombo vya habari.’

‘Wingi wa waathirika si kipimo cha ufisadi maana inategemea una nafasi gani kuwafisadi watu.’

‘Sawa lakini bado wenye uwezo zaidi lazima wawajibike zaidi. Kama hawataki, wasiingie kwenye mambo hayo kabisa.’

‘Mwanangu usianze hubiri zako hapa. Tunaongelea kitendo cha wazi cha kwenda kinyume cha maadili ya uandishi na haki za watu.’

‘Nakubali baba.’

Bosi aliendelea.

‘Mara nyingine nawaona waandishi wa habari kama fisi wanaozungukazunguka mizoga wakingoja nafasi yao. Ndiyo maana lazima wadhibitiwe na maadili ya kazi zao.’

‘Lakini nani anafuata maadili ya kazi hapa? Unashangaa nini baba?’

Safari hii MB aliingilia kati.

‘Lakini mwanangu baba yako si amesema. Huwezi kutetea maovu yako kwa kuonyesha maovu ya watu wengine. Maovu ni maovu tu!’

‘Sibishi mama. Na naamini wahusika katika vyombo vya habari wanatakiwa kuwajibisha wanaovunja maadili yao. Kwanza siamini kwamba yule anayedaiwa kufanya unyama huo ana miaka 18 kweli. Au ni njia ya kumweka hadharani kwa sababu si mtoto tena. Kisha wanaenda kushawishi au kuhonga siri za mahojiano ya polisi zitoke nje. Wanataka kuharibu kesi? Au wanajuaje kwamba yule mtoto ana akili timamu na habwati tu?’

Baba alitabasamu.

‘Kweli mwanangu.’

‘Na watu wa dini nao wananishangaza. Leo watangaza misukule, kesho mashetani. Wanajuaje? Na yule wa Ulaya ambaye amemfunga binti yake miaka 24 na kumbaka na kuzaa naye, yeye pia ni msukule au ni mashetani?’

Baba alitabasamu tena.

‘Umefanya vema kutaja kesi ya yule mwanaharamu wa Austria. Jana vyombo vyote vya habari vimemwongelea huyuhuyu tu. Lakini umeona mke wake akihojiwa? Au umewaona wale watoto waliototolewa huko chini ya nyumba? Na ile kesi ya Uingereza ambapo mtoto alikutwa chini ya kitanda. Umemwona laivu kwenye luninga? Ndiyo maana nasema lazima vyombo vya habari vidhibitiwe kama havitaki kujidhibiti vyenyewe. Nakuambia tumevidekeza hadi vinajiona miungu midogo.’

Basi mpenzi waliendelea kuzungumzia hiyohiyo muda mrefu. Lakini mimi nilipewa kazi ya kumpeleka yule mtoto wa dada yake MB alale. Ilikuwa kazi kabisa. Kwanza alikataa kuingia kwenye chumba chake bila mimi kuingia kwanza huku akiangalia. Nilifungua pazia ili nihakikishe kwamba hakuna mtu aliyekaa nyuma. Kisha niliangalia chini ya kitanda na ndani ya kabati. Mpaka alikubali kuingia na kulala kitandani. Lakini nilipotaka kutoka akaanza kulia tena kwa nguvu.

‘Wanakuja … wanakuja … nawaona.’

Nilijaribu kumtuliza kwa kufungua kabati zote tena na kutingishatingisha mapazia lakini haikusaidia kitu. Mwisho MB alimwambia BB alale naye kwa hiyo waliondoka pamoja.

Lakini ukiangalia mpenzi naona leo bosi kasema kweli kwa kiasi fulani. Kukalia kooni vyombo vya habari ni vibaya sana. Lakini vyombo navyo visikalie koo za watu pia, na wakijisahau, navyo viwajibishwe. Sikatai sote tunao ushambenga wetu. Kwenye matukio ya ajabu hakuna anayekubali kupitwa.

Lakini hii ina maana kwamba ni lazima tudekezwe na ushambenga wetu. Kwanza angalia huyu mtoto wetu alivyoathirika. Watoto wangapi wadogo wameona picha ile? Hata kama hawajapiga kelele kama huyu, wameathiriwa vipi kwa kuona kichwa cha mtoto wa umri kama wao? Haiwavurugi kweli? Hawapati jinamizi kweli?

Kisha kwa nini waandishi wanifuatefuate wakati niko katika majonzi makubwa sana? Eti wananiuliza najisikiaje? Hawajui? Wanahitaji kweli kunisikia nikisema nina majonzi hayo? Kwa nini dunia nzima ione machozi yangu? Sikutaka kuanikwa hadharani. Sikujipeleka kupigiwa kura. Balaa imetokea kwangu, kwa nini wengine waniongezee balaa? Wanaowazonga wakubwa wetu wawe na utu na maadili mema lazima na wao waonyeshe maadili mema pia vinginevyo hata uhalali wao wa kuzonga wageuka mizengwe.

Akupendaye mno japo hutaki kuonekana,

Hidaya


Kutoka Raia Mwema wiki hii.





No comments: