Wednesday, July 30, 2008

Kalamu ya Mwigamba





Samson Mwigamba

MHESHIMIWA Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, salaam aleykum. Juma lililopita niliwasiliana na Watanzania wote kwa njia hii ya makala. Nilijaribu kuwachokonoa ili kupata mawazo yao juu yako.

Na kwa bahati nzuri nilikuwa nimeongea moja kwa moja na Watanzania wote wakiwamo wasaidizi wako muhimu. Na ili kuwahakikishia kwamba niliwalenga na wao pia niliamua kuwataja kabisa pale niliposema, “Yote kwa yote ni kwamba kila mtu anajua sasa Rais Kikwete uwezo wake wa kuliongoza taifa na chama chake umepungua.

"Ninaamini ndani ya dhamiri yangu kwamba hata wasaidizi wake, wakiwamo usalama wa taifa, mawaziri na manaibu mawaziri, wanamtandao na wapambe wake, wabunge, viongozi wenzake ndani ya chama, watendaji wake serikalini na wasaidizi wake wengineo wote wanajua hili”.

Nilifanya hivyo kwa makusudi ili kupata maoni yao juu ya hili. Nawatambua sana wasaidizi wako. Ni watu mahiri sana kwa kulinda maslahi yao na ya wakubwa wao. Nilijua watanijibu haraka haraka kwa kukanusha ukweli huo mdomoni huku mioyoni mwao wakiutambua. Lakini hawakufanya hivyo. Hii inathibitisha kwamba hata wao ukweli uliwagusa na wamefikia mahali ambapo hawawezi kupingana nao.


No comments: