Sunday, August 24, 2008

Walimu wataka utafiti

wa lugha ya kufundishia



na Deogratius Temba

WALIMU nchini wameshauri kufanyika kwa utafiti wa lugha sahihi ya kufundishia mashuleni wanafunzi waweze kuelewa masomo vizuri.

Ushauri huo waliutoa mapema Jumatano, wiki hii wakati wakichangia katika majadiliano maalumu yaliyoandaliwa na Shirika la Oxfam Tanzania ya kuwezesha walimu kutumia mbinu shirikishi katika kufundisha.

Wengi wa waliochangia walieleza kuwa lugha inayotumika katika shule za sekondari ambayo ni Kiingereza ni kikwazo kwa wanafunzi kuelewa kwa ufasaha masomo yao.

Walishauri kuwa ni muhimu kwa serikali kabla ya kuandaa mitaala ya kufundishia, kukaa pamoja na wadau wengine wa elimu nchini na kufikiri njia sahihi zinazopaswa kutumika.

Kety Allen, Mkurugenzi wa Mradi wa Elimu Vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro, alisema kwa zaidi ya miaka 14 akiwa katika sekta ya elimu amekutana na wanafunzi wengi ambao hawaelewi masomo vizuri kwa sababu lugha ya kufundishia ni tofauti na wanayotumia kuwasiliana kila siku.

Pia walimu hao walikosoa tabia ya serikali kupitia Taasisi ya Elimu na wizara, kubadilisha mitaala kila mara serikali mpya inapoingia madarakani. Kwamba ni makosa kwa kila waziri kuingi na mambo yake mapya katika wizara hiyo.

“Mabadiliko ya mitaala ya kila mara uchaguzi ukifanyika, akiingia waziri mpya anasema ingiza hicho, ondoa hicho hayafai. Kuna mabadiliko mengine yanakuwa ya kisiasa, kulingana na matakwa ya mtu, hili ni hatari kwa maendeleo ya elimu,” alisema.

Katika taarifa yake kwenye majadiliano hayo, Shirika la Oxfam Tanzania lililoandaa mjadala huo lilieleza kuwa limejipanga kuhakikisha linawapa walimu muda wa kukaa pamoja na kujadili mambo yao hasa changamoto zinazowakabili katika kufundisha.

Naye Mratibu wa Programu ya Elimu wa Oxford Tanzania, Ellen Binagi, alisema maoni yaliyotolewa na washiriki wa semina hiyo yatakuwa changamoto kwa serikali na wadau wa elimu nchini.


Kutoka: Tanzania Daima

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

afadhali kwa kweli kwani fikiria miaka yote shuleni halafu unatoka sifuri si afadhali hata kuchunga mbuzi tu.

Anonymous said...

Lakini tusilaum bure mawaziri, kwani kazi hiyo hushariwa na watendaji wa wizara, kama wakurugenzi,Katibu mkuu,waziri huwa msemaji tu, Siku hizi kama waziri akikurupuka na kuandaa mitaala mipya, Katibu mkuu na wakurugenzi wana haki ya kuukataa,
Bongo