Taifa Stars yafanya
Kufuru kwa kuifunga
Mauritius 4 - 1
Timu ya taifa, Taifa Stars jana Jumamosi, iliwafunga wenyeji Mauritius kwa magoli 4-1 katika mechi ya kukamilisha ratiba ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia kanda ya Afrika, uliofanyika kwenye uwanja wa Mfalme George wa Tano.
Kwa ushindi huo dhidi ya timu ambayo Stars ingeweza kuifunga zaidi ya mabao hayo zilipokutana nyumbani Mei, Stars imefikisha pointi tano na kujihakikishia nafasi ya tatu isiyo na maana yoyote kwenye msimamo wa kundi A.
Lakini kwa ushindi huo pia Stars imefunga jumla ya mabao yote iliyofunga katika mechi sita za kampeni iliyopita ya kwenda Ghana, na mara mbili ya idadi iliyopata katika michezo minne ya kwanza ya mbio za kwenda Afrika Kusini mwaka 2010.
Stars ilishambulia tangu mwanzo wa mchezo na ilipata bao la kwanza katika dakika ya 11 lililofungwa na Kigi Makassy aliyewahi mpira wa adhabu uliopigwa na Shabaan Nditi baada ya Mrisho Ngassa kufanyiwa madhambi na mmoja wa walinzi wa Mauritius.
Hatahivyo, wakiwa wanashangilia bao hilo, dakika mbili baadaye Mauritius walisawazisha kwa mfungaji kupiga mpira tik tak uliomzidi kimo kipa namba moja wa kocha Marcio Maximo Ivo Mapunda.
Lakini Nizar Khalfan alisawazisha makosa hayo kwa kuongeza bao la pili katika dakika ya 19, alipowahi mpira wa pasi ya juu kukatisha safu ya ulinzi uliopigwa na chipukizi Jerson Tegete.
Tegete alipachika bao la tatu katika dakika ya 28 akiwahi pasi ya Nditi, na dakika tano baadaye alishindilia bao la nne baada ya kuwahi krosi iliyopigwa na Ngassa.
Stars ingeweza kupata mabo zaidi kama washambuliaji Tegete na Mussa Hassan wangekuwa makini zaidi katika kipindi cha pili.
Akizungumza mara baada ya mchezo, Meneja wa Stars Tasso Mukebezi alisema walistahili ushindi zaidi ya huo, na kwamba hayo ni maandalizi ya hatua ya mwisho ya michuano ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani dhidi ya Sudan itakayofanyika Novemba na Desemba.
Stars imefikisha pointi tano baada ya mchezo wa awali kutoka sare na Mauritius na Cameroon.
Timu ilikuwa:
Stars: Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Salum Sued, Nadir Haroub `Canavaro`, Geofrey Bonny, Shabaan Nditi (Jabir Aziz), Nizar Khalfan, Jerson Tegete (Adam Kingwande), Mrisho Ngassa na Kigi Makassy (Mussa Hassan `Mgosi`).
Awali, katika mechi zilizochezwa juzi Ijumaa mabao matatu katika dakika 13, za kipindi cha pili yalizaa ushindi muhimu wa 3-2 wa Kombe la Dunia kwa Algeria dhidi ya Senegal.
Matokeo hayo yaliwapa wenyeji uongozi wa pointi moja juu ya Senegal kileleni mwa Kundi la Sita.
Nalo goli la dakika za mwishoni la Ahmed Osman liliipa Libya ushindi wa 1-0 dhidi ya Ghana katika mwechi ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia jijini Tripoli Ijumaa, na kuiweka kileleni mwa msimamo wa kundi.
Osman alifunga katika dakika ya 84 ya mechi hiyo ya Kundi la Tano la kanda ya Afrika na kuiwezesha Libya kuwa na pointi tatu zaidi ya timu nyingine na kukaribia kuihakikishia kucheza hatua ya tatu.
Djibouti ilifungwa nyumbani 3-0 na Malawi.
Msimamo wa Kundi la Kwanza la michuano ya awali ya Kombe la Dunia kanda ya Afrika baada ya mchezo wa Stars na kabla ya Cameroon kucheza na Cape Verde jana usiku:
- SOURCE: LETE RAHA
No comments:
Post a Comment