Monday, September 29, 2008

Ubaguzi wa rangi

Norway bado upo,

kibaya zaidi…

kwenye makanisa!

Mchungaji toka

Sierra Leone akataliwa

Kusalisha kwenye

Mazishi…..


Mchungaji wa Parokia ya Oppdal, jimbo la Nidaros, Joseph Moiba (Pichani, mwenye asili ya Sierra Leone), amekataliwa mara tatu na Wakristo wa Parokia hiyo kusalisha kwenye mazishi ya Wanorwejiani. Baadhi ya Wakristo wa Parokia hiyo wamemwambia kuwa "Mtu kama yeye, yaani Mwafrika" hawezi kusalisha Wanorwejiani na arudi kwao alikotoka. Kibaya zaidi ni kuwa Mkuu wa Makasisi wa Parokia hiyo, mchungaji Kirsten Almås, alitafuta mchungaji Mnorweji kusalisha kwenye mazishi mara zote hizo tatu, Moiba alipokataliwa kusalisha, bila hata kuingilia kati. Askofu wa jimbo la Nidaros, amekataa kuingilia mgogoro huo, na kujaribu kulifukia ardhini, hilo la mchungaji Moiba kubaguliwa kwa sababu ya rangi na asili yake!

Kama mwezi mmoja uliopita, saa kama 7 mchana, akiwa petroli stesheni moja, baadhi ya watu walianza kumdhihaki kwa maneno ya kibaguzi rangi na mmoja wao alitaka hata kumpiga. 

Mchungaji Moiba amekuja Norway toka Sierra Leone mwaka 2000 na mwaka 2006 aliajiriwa na kanisa la Kilutheri la Norway. Kasisi Joseph Moiba ni mchungaji wa kwanza Mwafrika kuwa Mchungaji wa Parokia hapa Norway.

Magazeti ya Oppdal,  Opp na Opdalingen ndiyo yaliyoandika kashfa hiyo kwa mara ya kwanza, kabla ya magazeti makubwa ya Oslo kuanza kuandika. Gazeti la Verdens Gang (VG)  na Dagbladet (mtandaoni) yaliandika tukio hilo, Jumamosi 27. Septemba, na gazeti la Aftenposten liliandika makala kubwa ya kurasa mbili, Jumapili, Septemba 28


1 comment:

Anonymous said...

Ubaguzi wa rangi uko kila nyanja hapa Norway. Ukitaka kupanga nyumba, ukipiga simu, mwenye nyumba akisikia sauti na lafudhi yako tu, utaambiwa nyumba imeshapangishwa!!! Ukimpa simu rafiki yako Mnorweji apige naye kuulizia, atajibiwa nyumba haijapangishwa, aende akaiangalie!!!!

Tulie tu...