Tuesday, October 21, 2008

Seretse Khama Ian Khama,

Rais wa Botswana

Ziarani Tanzania




na Ramadhani Siwayombe, Arusha

RAIS wa Botswana, Luteni Jenerali Seretse Khama Ian Khama, akiwa na msafara wake wa maofisa 18, ametua jana nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kupokewa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete.

Rais Khama aliwasili akiwa ameambatana katika msafara huo na Mkuu wa Majeshi wa Botswana, Luteni Jenerali T.H.C Masire, Waziri wa Ulinzi, Dk. Seretse na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, P.TC. Skelemani.

Ziara hiyo ya Rais Khama ni mwaliko maalumu kwa ajili ya kuja kushuhudia na kuwavisha nishani maofisa wa jeshi, waliomaliuza mafunzo ya muda mrefu ya mwaka mmoja katika Chuo cha Kijeshi cha Monduli (TMA).

Wanaohitimu mafunzo hayo ni maofisa 155, ambapo kati yao 22 ni maofisa wa jeshi wanawake kutoka nchini Botswana, maofisa 12 kutoka Uganda, watano kutoka Kenya, wawili kutoka Shelisheli na waliobaki 101 ni maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Kijeshi cha Monduli, Kanali Jairosi Mwaseba, alisema maofisa hao walianza mafunzo Oktoba mwaka jana na leo ndiyo wanahitimu mafunzo hayo ambapo watatunukiwa nishani zao, mbele ya marais hao katika chuo hicho.

Aidha, katika Uwanja wa KIA, Rais Kikwete aliambatana na baadhi ya mawaziri wa Jamhuri ya Muungano, akiwemo John Magufuli (Mifugo na Uvuvi), Wiliam Ngeleja (Nishati na Madini), Dk. Huseni Mwinyi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), na Batilda Buriani (Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).

Pia alikuwepo Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidore Shirima na maofisa wengine mbalimbali wa serikali mkoani hapa.

Baada ya kumalizika kwa uvishaji wa nishani kwa maofisa wa jeshi leo, marais hao wataondoka kwenda nchini Uganda kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika (AU), unaoanza kesho nchini humo.


No comments: