Kikwete aenda Libya
Na Gladness Mboma
MWENYEKITI wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete ameondoka nchini jana kuelekea katika nchi za Libya na Ethiopia kwa ziara fupi ya kikazi.
Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Bw. Salva Rweyemamu ilisema kuwa Rais atakutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa nchi hiyo, Kanali Mummar Gaddafi juu ya jitihada za kupatanisha mgogoro kati ya nchi za Chad na Sudan.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo nchi za Libya na Kongo ziliombwa na AU kuzipatanisha nchi jirani za Chad na Sudan ambazo uhusiano wao umekuwa siyo mzuri kwa muda sasa.
Bw. Rweyemamu alisema nchi hizo mbili zimekuwa na mzozo wa kisiasa unaosababishwa na upande mmoja na vita ya Darfur, lakini pia kutokana na kila moja ya nchi hizo kumtuhumu mwenzake kwa madai ya kusaidia waasi wa nchi nyingine.
Alisema Rais Kikwete ataondoka nchini Libya kwenda Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria mkutano wa pili wa Kamisheni ya Afrika kuhusu Ajira kwa Vijana iliyoanzishwa na Waziri Mkuu wa Denmark, Bw. Forg Ramussen.
Bw. Rweyemamu alisema Bw. Ramussen alimwomba Rais Kikwete kuwa mjumbe wa Kamisheni hiyo inayoshughulikia masuala hayo ya ajira kwa vijana Barani Afrika.
Alisema kuwa Rais Kikwete alikubali kuwa mjumbe wa Kamisheni hiyo ambayo pia Mwenyekiti wake ni Bw. Rasmussen.¨
No comments:
Post a Comment