Vitambulisho vya
taifa utata mtupu
Muda wa kuthibitisha maombi ya wazabuni waongezwa
Baadhi walalamika kutumiwa barua muda ukiwa umeshakwisha
MRADI wa Vitambulisho vya Taifa umekumbwa na utata mwingine baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuongeza muda wa kuweka wazi matokeo ya zabuni hiyo, jambo lililoyachanganya makampuni yaliyoomba.
Kwa mujibu wa barua iliyotumwa kwa makampuni yaliyoomba zabuni ya kutengeneza vitambulisho hivyo, makabrasha ya maombi yalifunguliwa Juni 25, mwaka huu, uthibitisho wa zabuni ungefanyika ndani ya siku 84, “lakini kutokana na wingi wa maombi tuliyopokea tumeongeza muda wa uthibitisho wa uhalali wa maombi yako.”
Barua hiyo, yenye kumbukumbu CAB/48/468/01/109 ya Oktoba 16, 2008, inasema kuwa kutokana na wingi wa maombi ya zabuni hiyo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inawaomba waombaji kuiandikia tena ndani ya siku 30 tangu muda wa kuandika barua hiyo ya Wizara, Oktoba 16, 2008.
Kwa mujibu wa barua hiyo, zabuni hiyo inatambuliwa kama “MoHA/NIDA/PQ/2007.08/01 for the Implementation of the National Identification System Based on Smart Card Technology.”
“Kwa hiyo tunakuandikia ili kukuomba uweze kutuandikia ili kuongeza muda wa kuthibitisha maombi yako kwa kipindi kingine cha siku 30 kuanzia tarehe ya barua hii, ili kutuwezesha sisi tumalizie mchakato wa maombi.
“Barua ya majibu ni lazima iletwe na tarishi kwa Katibu, Bodi ya Zabuni ya Wizara, Wizara ya Mambo ya Ndani, Mtaa wa Ohio/Ghana, Dar es Salaam, Tanzania, na ipokewe ndani ya siku 14 tangu tarehe ya barua hiyo.
“Maombi ambayo hayatazingatia uhalali wa muda huo yatabatilishwa bila kupewa taarifa yoyote ya ziada,” ilisema barua hiyo, ambayo imesainiwa na A.M. Wambura, Katibu wa Bodi ya Zabuni ya Wizara na nakala zake kupelekwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Mratibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ndani ya Wizara hiyo.
Baadhi ya waombaji wa zabuni hiyo waliozungumza na gazeti hili walieleza wasiwasi wao kuhusu mwelekeo wa mradi huo, hasa kwa kuwa barua hiyo imechelewa kuwafikia kwa sababu ‘ilitumwa kwa njia zisizo za kawaida’ na kuwafikia wakati siku zilizotajwa na barua ya Wizara zikiwa zimepita.
Baadhi yao wanaamini kwamba hilo lilifanywa kwa makusudi ili kuwaengua katika patashika ya kumpata mshindi na kumfagilia njia yule ambaye Wizara inamtaka.
![]() Waziri Lawrence Masha |
Lakini Raia Mwema ilipomtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, juzi Jumatatu, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa njia ya simu, na badala yake akasema yatumwe maombi maalumu ya kumwona.
“Mimi siwezi kuzungumzia suala hilo kwenye simu. Ni lazima uombe appointment, uje ofisini ndipo uniulize maswali hayo, kwa sababu na mimi ninahitaji kuwa na wasaidizi wangu,” alisema.
Raia Mwema ilipomwomba ipangiwe muda wa kumwona, Masha alisema apigiwe tena simu saa moja baadaye, wakati huo ikiwa ni saa 4.10 asubuhi ya juzi Jumatatu.
Hata hivyo, Masha alipopigiwa simu majira ya saa 5.10, yaani saa moja baadaye, mtu mwingine alijibu kuwa alikuwa katika kikao na hivyo apigiwe tena saa moja nyingine ambayo ingefuata. Juhudi zaidi za kumpata hazikufanikiwa.
Mradi huo uumekuwa ukigubikwa na utata mara kwa mara huku kukiwa na sura dhahiri ya ukosefu wa uwazi, na hata kujenga hisia kwa baadhi ya watu kuwa ni kinyang’anyiro cha ulaji.
Wiki ya Mei 14 na Mei 20, mwaka huu. Masha alitangaza kuwa zabuni ya mradi huo ingetangazwa kabla ya mwisho wa Mei mwaka huu, lakini tayari ofisi ya mradi huo ilikuwa ipo na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) alikuwa ameteuliwa.
Mradi wa Vitambulisho vya Taifa umekuwa ukipita katika hatua za kuiva na kufifia, kwa kuwa zabuni ziliwahi kushindaniwa, washindi wakapatikana, lakini hazikutangazwa hadharani, ikiwamo kampuni mmoja kutoka Malaysia.
Miaka takribani 10 iliyopita kampuni kutoka Malaysia ilishinda zabuni ya utengenezaji wa Vitambulisho vya Taifa, lakini zoezi zima halikutangazwa kwa umma.
Chanzo: Gazeti la Raia Mwema la mtandaoni.
No comments:
Post a Comment