Vitambulisho vya uraia
visitolewe kwa
wahamiaji
Na Kakoloboji Mwandanji
TUNAWEZA kusema nini kuhusu uraia wa Tanzania? Ukizungumzia mambo kwa mfano yanayowahusu wakimbizi, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi za Afrika, watakushangaa.
Ukizungumza na kutaja madikteta wa dunia hii, huwezi kufaulu kwa kuwa kila mmoja wetu, akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa hiki au kile, anaota mapembe. Mara nyingi anakuwa sugu. Anakuwa haambiliki!
Mfalme fulani wa nchi fulani, alipoulizwa na kuelezwa kuhusu Taifa, yeye alikejeli kwa kusema: “Taifa, Taifa lipi? Mimi ndiyo Taifa.” Labda kwa siku hizi, dikteta wa namna hiyo, atasema unasema nini wewe.
Kazi hiyo uliyonayo, mimi ndiye niliyekuajiri, ukiendelea nitakuondoa.
Tuachane na hayo, naomba sasa mniruhusu nizungumzie mambo fulani fulani yanayohusu uraia wa Taifa letu, Tanzania.
Kila ninapowaza na kutafakari kuhusu uraia wa Tanzania, huwa sipati majibu.
Huwa ninajiuliza; hivi ni kwanini Taifa la Tanzania lina ukarimu wa kiajabu?
Sijathibitisha. Lakini maneno yaliyozagaa mitaani, ni kwamba uharamia na ukorofikorofi ulioenea katika kila kona ya nchi yetu hii, unatokana au unasababishwa na wahamiaji, raia kutoka nje ya nchi yetu. Wahamiaji hao, wengi wao wameingia nchini mwetu wakiwa na ‘vijisenti’ vyao, na matokeo yake, kwa sababu sisi Watanzania ni watu wema, kiasi cha kukaribia utakatifu, watu hao hupata sehemu za kujibanza, na hatimaye huotesha mizizi. Shauri yako! Yeyote akijifanya mdadisi, mimi binafsi sijadadisi.
Kwa hiyo basi, Taifa letu hili hadi sasa, limeanza kukorogwa na watu hao maharamia. Kuna maeneo ambayo wahamiaji hao wamejikita, na wana nguvu kiasi kwamba wameweza kumiliki hata nyumba zao za ibada.
Binafsi, nimewahi kwenda kwenye nyumba za ibada za watu hao, hata Kiswahili chao ni pinduapindua. Nilipouliza kulikoni Kiswahili hiki, nikaambiwa katika Tanzania, watu wote ndimi zao haziko sawa.
Baada ya kupata jibu hilo, sijarudi tena katika Kanisa hilo. Nyumba za ibada nini bwana! Jaribu kwenda maeneo mengine. Siyataji hapa. Lakini ukifika huko, unatambuliwa kwamba wewe ni mtu wa Tanzania. Sisemi tuanze kubaguana, la hasha!
Ninachosema ni kwamba hao wanaosema watatengeneza vitambulisho vya uraia wa Taifa hili, mbona hadi sasa hawajatueleza namna na mbunu watakazotumia katika kuhakikisha kwamba vitambulisho hivyo vya uraia haviangukii mikononi mwa wahamiaji hao. Kwa mtazamo wangu, siku ya siku itakapofika, wahamiaji hao nao watapanga mstari na kujiandikisha, tupende tusipende. Pengine, anaweza akatokea mtu akanitaka nieleze namna watakavyojiandikisha.
Lakini, mbona ni wahamiaji wengi tu hapa nchini wanazo pasi zetu za kusafiria? Mbona wanavyo hata vyeti vya kuzaliwa?
Kwanini hao wenye kupata ukandarasi wa kuorodhesha watu hao, hawatuelezi itakavyokuwa? Ni nini hiki? Mkandarasi huyo tumeambiwa atapata utajiri mkubwa sana. Usiniulize itakuwa kiasi gani!
Ninachosema ni kwamba huu si mwisho wa dunia, wala si Alfa. Cha muhimu hapa, na ambacho ndicho cha msingi, ni kuhakikisha kwamba walaghai wote hao, hata kama hawafukuzwi nchini, basi wanadhibitiwa wasipate vitambulisho hivyo vya uraia.
Wadhibitiwe vipi, waimarishaji wa sheria wanajua!
Rafiki yangu mmoja, aliwahi kunishekesha kidogo, pale aliponiambia wazi wazi kwamba mambo ya wahamiaji yamehusishwa pia hata katika ukandarasi. Basi, mpaka hapo tumekwisha!
Uzalendo ni lazima uwepo. Uzalendo lazima uzingatiwe katika hili la vitambulisho vya uraia. Kandarasi zinatawala sana siku hizi, yeyote ajaribu tu, atashindwa.
Chanzo: Maoni ya wasomaji kwenye gazeti la Mtanzania
No comments:
Post a Comment