Kumbadilisha
mwanamme
inawezekana!?
Mwaka tunaumaliza jamani. Ukiulizwa umefanya nini mwaka huu wote unaweza ukose majibu ya haraka haraka lakini yote maisha. Unayo nafasi nyingine ya kujipanga na kuhakikisha kuwa mwaka ujao unakamilisha uliyoyadhamiria.
Leo nimeshawishika kuweka makala hii kufuatia kesi nyingi ambazo nimekuwa nikikumbana nazo huko mtaani.
Wapo wasichana ambao huamua kuolewa wakidhani baada ya kuolewa huenda waume zao wakaja kubadilisha zao tabia ambazo hawapendezwi nazo. Wapo pia wanawake ambao huamini wanaweza kuwabadili waume zao kwakuwa wanapendwa.!
Mathalani iwe mumeo ni mvutaji sigara kupindukia, mlevi chakari au labda iwe ni mgonjwa wa wanawake yaani kicheche ama tu ana katabia ambako kana kukera.
Ukweli ni kwamba Mwanamme huwa habadilishiki tena si kwa usiku mmoja usijidanganye kwa hilo, mwanamme anaamua kubalika mwenyewe Full stop. Unachoweze kufanya wewe nikumuonyesha sababu yakinifu na kumpa muda aamue mwenyewe.
Unaweza kumbadili kwa kumfanya aamini akibadilika itamsaidia. Wanawake wanataka kuwabadili tabia wapenzi wao, wapenzi hao wakidhani wanawake hao wanataka kuchukua nafasi za mama zao hapo sasa ndipo shughuli ilipo.
Huenda unadhani kwa kutumia kupendwa kwako kunaweza kuwa silaha na ngao ya kumgeuza mwanamme utakavyo, kumbe unajidanganya. Kwakuwa kitakachokuja kukumaliza hapo nikuja kugundua kuwa yule uliyekazana kumbadili kwa miaka kadhaa hajabadilika na matokeo yake unaweza kuja kuugua kichaa bure.
Unashindwa kupata majibu ya haraka haraka kuwa huyu mtu asiyebadilishika ni mtu wa aina gani. Kwanza ni vyema ukafahamu kuwa kuna sababu nyingi tu zilizopelekea kwa nini mumeo akawa na tabia hiyo inayokuudhi.
Kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho asilimia mia moja ni kwamba kumbadilisha mtu wa namna hiyo haiwezekani. Lakini!
Kumfanya yeye mwenyewe abadilikie kwa njia sahihi inawezekana.
Unachoweza kufanya ni kumuonyesha sababu za msingi kwanini inambidi abadilike na umfanye aamini kwamba kubadilika kwake ni kwa ajili yake na si kwasababu ya kumridhisha mtu fulani iwe wewe ama watoto wake.
Wanaume huwa hawependi kuonekana kama wanafanya vitu kwa ajili ya mtu fulani, wanataka wao waamue wenyewe kubadilika na sio kana kwamba wanalazimishwa na kushurutishwa.
Inawezekana kumbadili mwanamme mavazi na staili ya nywele lakini sio tabia. Na tena sio kwa usiku mmoja shosti.
Inawezekana ukaona kama umembadili lakini kumbe ukawa unaamini uongo, kwa maana kuwa inaweza kuja siku ukagundua kuwa muda wote uliupoteza kwa imani potofu.
Chamsingi nikujua namna ambayo unaweza kuitumia kumfanya aachane na hiyo tabia, na si kwa kumuwekea shonde.
Ipo njia nyingine; Unaweza pia kumuomba Mungu akusaidie katika tatizo hilo ninayo imani kubwa naye atakusaidia Inshaalah. Unaweza pia ukajifunza kusubiri kwa kua naamini taratibu chini ya maelekezo yako ipo siku atabadilika yeye mwenyewe.
Unapotumia nguvu kumbadili mwanamme inawezekana ukawa unaishi kwa matumanini na yote kwa picha ya nje yanaonekana kama ni mabadiliko lakini sivyo.
Kwahiyo kama kweli unataka abadilike kwanza ni kukubali tofauti zenu. Usijaribu kumpindisha kwa nguvu kwa kua kufanya hivyo ni sawa na kutaka kuyanyoosha matege ya mtu mzima. Pili tafuta chanzo cha tabia hiyo najaribu kukidhibiti na kisha mpe nafasi ya yeye mwenyewe kubadilika utaona matokeo.
Wakati mwingine marafiki zake waweza kuwa ndiyo kichocheo cha tabia yake, usiwakurupushe bali muepushe nao kwa njia ambayo yeye hatojua kuwa unamuepusha nao. Unaweza ukamlazimishia urafiki kwa mtu ambaye unajua anaweza kuona tofauti na akabadilika. Hii ni sawa na ule msemo usemao: nionyeshe marafiki zako ntakuambia vile ulivyo.
Na mwisho kabisa zungumza naye taratibu..! Hii kila siku huwa naisema. Mazungumzo bwana ni power. Hata kama kuna tatizo utatuzi utakuja endapo mtazungumza kwa utaratibu na kwa muda unaofaa kupenyeza hayo mazungumzo yako, hakika yanamuingia na usitegemee matokeo hapo kwa hapo. Subiri.
Kutoka gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment